Meya Kapunga akwepa lawama
*Kifo cha ‘King’
wa Chadema chazua utata
Na, Christopher
Nyenyembe, Mbeya
MSTAHIKI Meya
wa Jiji la Mbeya,Athanas Kapunga amekanusha vikali lawama zinazotolewa dhidi
yake juu ya kifo cha Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Itiji,Ezekiel Mwaigoga
(53) aliyefia gerezani .
Kuibuka kwa
lawama hizo kunafuatia mvutano mkali wa kisiasa unaoendelea katika kata ya
Itiji ambayo,Mstahiki Kapunga ndiye diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CCM na
kwamba aliweza kushinikiza ipasavyo,marehemu Mwaigoga maarufu kwa jina la King
afungwe gerezani.
Mstahiki
Meya alielezea kwa undani jana na kufafanua kwa kina mazingira ya kifo cha King
aliyekuwa Mwenyekiti wa mtaa wa Itiji kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kuwa hausiki na kwamba amekuwa akionewa na kusakamwa na kundi la watu
wachache juu ya matukio na mikasa inayotokea kwenye kata yake.
Mahojiano
maalumu yaliyofanywa na Tanzania Daima kuhusu tuhuma hizo,zilimfanya Meya
Kapunga akiri wazi kuwa kwa njia yoyote ile hapaswi kutupiwa lawama za kifo cha
King wala kuingilia uhuru wa mahakama uliomtia hatiani kiongozi huyo wa mtaa na
kusababisha ahukumiwe kifungo cha miaka saba.
“Siwezi
kuhudhuria kila msiba wa mtu,mimi nipo kwenye majukumu mengine,kama mke wangu
amekwenda msibani,watoto wangu wamekwenda,watakuwa wamekwenda kwa niaba yangu
sio lazima niende mimi” alisema Kapunga.
Alisema kuwa
ameshindwa kushiriki kwenye msiba huo kwa kuwa yupo kwenye kikao cha bodi za
mamlaka ya maji kutoka mikoa ya Iringa,Ruvuma,Njombe na Mbeya hivyo itakuwa
vigumu kuwepo mchana kutwa bila kujua taratibu za mazishi.
“Naomba,nawaomba
mnihurumie sana,nioneeni huruma jamani,kweli kila jambo baya linalotokea kwenye
kata yangu ni Kapunga,naiangalia sana afya yangu nimeugua kwa miezi sita siwezi
kushiriki kila jambo,siwezi kuingilia kazi ya Mungu kwa kuwa kila mtu atakufa
tu hata Kapunga siku yake ikifika atakufa” alisema Mstahiki Kapunga.
Alisema kuwa
amechoshwa na lawama nzito zinazoelekezwa kwake na kutoboa siri ya migogoro
kadhaa inayoibuliwa kwenye kata ya Itiji,maeneo ya Nonde kuwa imekuwa kata
inayosifiwa kwa vitendo vya ushirikina(uchawi) kuliko kufikiria masuala ya
maendeleo.
“Wewe ni mkazi
wa jiji hili,hii kata yetu ni uchawi tu,tunaacha kuzungumzia mambo ya barabara,maji,shule
tunagombana kwa mambo ya upuuzi,hao wanaonisakama walikuwa wapi kumwekea
marehemu wakili,walikuwa wapi kumtibu mtu waliyepigana nae,ebu waulize”
alilalamika Meya huyo.
Wakati Meya
huyo akionekana kuguswa na lawama za kigo cha King,jana katika mazishi hayo kulitanda gumzo zaidi wakilalamika kuwa
marehemu King hakupaswa kutupwa gerezani kwa kosa la kupigana na kuhukumiwa
kifungo cha miaka saba jela bila shinikizo la Meya huyo ambaye wanadai alikuwa
na uhasama mkubwa wa kisiasa na marehemu King .
Binti wa
marehemu,Irene Ezekiel alisema kuwa familia yao imepokea kwa mshituko mkubwa
kifo cha baba yao ambaye kabla ya kukutwa na dhahama hiyo aprili 24 mwaka huu
alikuwa mtu mwenye afya njema.
Baadhi ya
ndugu waliozungumza na Tanzania Daima na majirani walikuwa wakisubiri taarifa
za uchunguzi wa kifo cha King huku wakiendelea na taratibu za mazishi.
King
aliyefariki juzi katika gereza la Ruanda jijini humo amezikwa jana katika makaburi
ya Nonde ambako umati mkubwa wa watu walihudhuria kifo hicho,alizikwa kwa
heshima zote za Chadema kwa kuwa alikuwa kiongozi kupitia chama hicho.
No comments:
Post a Comment