Kocha
Msaidizi wa Azam, Kalimangonga Ongara akizungumza na waandishi wa habari katika
ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhusu pambano lao na Yanga la
Ngao ya Hisani litakalofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kushoto ni Meneja Masoko wa Shirika la Bima ya Taifa (NIC), Elisante Maleko na Meneja
Biashara wa TFF, Peter Simon.
Na Mwandishi Wetu
Ligi Kuu Tanzania bara itakayoanza Septemba 20, inazinduliwa leo
katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya
bingwa mtetezi, Azam FC na Yanga iliyomaliza msimu uliopita nafasi ya pili.
Akizungumzia
mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kally Ongara, alisema kwao Ngao ya
Jamii, ni kombe muhimu ambalo wanalisaka kuingia katika orodha ya mataji yao kabatini,
hivyo wanaipa uzito.
“Hii ni
mechi iliyobeba taswira yetu ya msimu ujao kwani kupitia mechi hii, tutaweza
kujua mwelekeo wa kikosi chetu katika mbio za kutetea taji la Ligi Kuu.
Tulichofanya mwaka jana, kila timu inaweza. Lakini kutetea, ndio jambo gumu
kwetu,” alisema Ongara.
Alisema, wanawaheshimu
Yanga kama moja ya timu kongwe nchini, lakini kwa suala la kupigania ushindi,
wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na ushindi na kutwaa taji hilo kwa mara ya
kwanza katika historia yao.
Ongara aliyasema
hayo jana alipomwakilisha bosi wake, Joseph Omog katika mkutano huo wa makocha uliofanyika
Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuelekea mechi hiyo ambapo hata
hivyo upande wa Yanga hawakufika.
Kabla ya
mkutano huo, Azam FC ilitumia ukurasa wake wa Facebook kuandika kauli ya Omog akisema
ni mechi muhimu, hivyo vijana wake watapambana kuibuka na ushindi kuyafikia
malengo yao.
“Ni mechi
muhimu! Kocha Mkuu wa Azam FC, Joseph Omog, ameutaja mchezo wa Ngao ya Jamii
dhidi ya Yanga kuwa ni muhimu. Omog amesema ni muhimu kwa timu yake kushinda
mchezo huo, ili kuimarisha morali ya timu kabla ya kuanza kwa ligi,” ukurasa
huo ulisomeka.
Kupitia ukurasa
huo, Omog raia Cameroon, aliongeza kuwa amewapa wachezaji wake kila kitu
kitakachowawezesha kushinda mechi hiyo, hivyo kazi imebaki kwao kushinda na
kuleta furaha kwa timu hiyo.
Azam
inacheza mechi hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo, ambapo miaka miwili ilicheza
kama makamu bingwa na mara zote ilipoteza dhidi ya mabingwa Simba na Yanga,
wakati leo inacheza kama bingwa, hivyo kubebwa na historia ya Ngao ya Jamii.
Kwa upande
wa vikosi, wakati Yanga ikitarajia kuwakosa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Andrey
Coutinho walio na majeruhi, Azam watashuka dimbani bila nahodha wao John Bocco
‘Adebayor’ na Waziri Salum ambao ni majeruhi.
Kwa upande
wake Meneja Biashara wa TFF, Peter Simon, alisema kuwa maandalizi ya mechi hiyo
yamekamilika na tayari wamepokea maombi mbalimbali ya mgawo wa asilimia 10 ya
mapato kwa taassisi za kijamii.
“Tumepokea
maombi kutoka Chama cha Wasioona Tanzania, Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata)
na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS). Na baada ya mechi tutaona ni kwa
namna gani tutawasaidia katika maombi yao,” alisema Simon.
Yanga wao
wametumia tovuti kuandika kuwa kikosi chao kinajivunia rekodi nzuri katika
mechi za Ngao ya Jamii, na watashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa
bao 1-0 katika mechi hiyo msimu uliopo, kwa bao la Salum Telela ‘Essien.’
Kwa mujibu
wa tovuti hiyo, Maximo atakayeiongoza Yanga mara ya pili katika dimba la Taifa,
amesema vijana wake wapo katika hali nzuri jambo ambalo linampa wigo mpana wa
kikosi kuchagua nani amtumie katika mchezo huo.
Hadi sasa
Maximo ameiongoza Yanga katika mechi nne za kirafiki na kufanikiwa kushinda yote;
dhidi ya Chipukizi FC (2-0); dhidi ya Shangani FC (2-0); dhidi ya KMKM (1-0) na
1-0 dhidi ya Thika United ya Kenya.
Katika
mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana asubuhi Uwanja wa Shule ya Sekondari
Loyola, nyota pekee aliyeshindwa kufanya mazoezi, ni Jerson Tegete,
anayesumbuliwa na nyonga
Kuhusu Mbrazil
Coutinho, alifanya mazoezi mepesi chini ya daktari Dk. Suphian Juma.
No comments:
Post a Comment