HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 14, 2014

MISS TANZANIA 2013 AAHIDI MAKUBWA MASHINDANO YA UREMBO YA DUNIA

 Mkurugenzi wa Lino International Agency Limited, Bw. Hashim Lundenga (kulia) akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu safari ya Mrembo wa Tanzania wa mwaka 2013 kuelekea katika Mashindano ya Urembo wa Dunia (Miss World 2014) nchini Uingereza.
 Mshindi wa Mashindano ya Urembo Tanzania kwa mwaka 2013, Happiness Watimanywa (kushoto) akieleza jambo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu safari yake ya kwenda kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Urembo wa Dunia yatakayoanza mapema tarehe 14 Desemba, 2014.
 Baadhi ya Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano kuhusu safari ya Miss Tanzania 2013 nchini Uingereza kwenda kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya Urembo wa Dunia yatakayoanza mapema tarehe 14 Desemba, 2014. (Picha na Benedict Liwenga, MAELEZO-DSM)

Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
 
MREMBO wa Tanzania wa mwaka 2013, Happiness Watimanywa ameahidi kuing’arisha Tanzania katika mashindano ya ulimbwende ya Dunia yatakayofanyika mapema mwezi ujao huko nchini Uingereza.
 
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, mlimbwende huyo amewaeleza waadishi kuwa, kutokana na uzoefu wa kazi zake alizokuwa akifanya kwa jamii kwa muda kipindi cha mwaka mmoja ikiwemo misaada ya hali na mali anayoipata toka  Bodi ya Utalii Tanzania pamoja na wahisani wengine nchini amewaahidi Watanzania kuibuka na ushindi katika kinyang’anyiro hicho huko nchini Uingereza ili kuitangaza Tanzania.
 
Alieleza kuwa, tayari Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza utakuwa tayari kumpokea pindi atakapowasili nchini humo kwa lengo la kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya ulimbwende yatakayowahusisha walimbwende toka Ulimwengu  mzima.
 
“Nimejifunza mambo mengi hasa kipindi wakati nasafiri sehemu mbalimbali nchini pamoja na kufanya kazi za kusaidia jamii katika kipindi chote, hivyo nawaahidi watanzania ushindi katika mashindano hayo yatakayofanyika huko Uingereza pia mnipigie kura zenu za wingi”, alisema Watimanywa.
 
Naye Mkurugenzi wa Lino International Agency Limited, Bw. Hashim Lundenga ambao ni waandaaji wa Miss Tanzania, alisema kuwa mashindano ya Urembo wa Dunia ni mashindano ya Kimataifa ambayo yanawakutanisha walimbwende toka nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania, hivyo alitoa wito kwa watanzania wote kuunga mkono kwa kumpigia kura nyingi mwakilishi ambaye ndiye mrembo wa Tanzania kwa mwaka 2013, Hapinness Watimanywa ili ajinyakulie taji hilo la dunia ili aweze kuipa sifa Tanzania kimataifa.
 
Mashindano ya Urembo ya Dunia yanatarajiwa kufanyika mapema tarehe 14 Desemba, 2014 huko nchini Uingereza ambapo mrembo huyo wa Tanzania anatarajia kuanza safari yake ya kuelekea nchini humo tarehe 15 Novemba, 2014 tayari kwa ajili ya mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment

Pages