MKAZI wa Kata ya Kilole wilayani Korogwe Tanga, Anna Tindwa
(54), amemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi kuingilia kati kitendo cha Halmashauri ya wailaya hiyo
kuchelewesha kumlipa fidia ya shamba lake kwa zidi ya miaka tisa.
Fidia anayodai imetokana na Serikali ya Mtaa wa Kwamngumi katika
kata hiyo kulichukua shamba lake mwaka 2006 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari
ya Kata Kilole.
Akizungumza katika jijini Dar es Salaam, Anna, alisema hadi sasa hajui kuna sababu gani inayofanya asilipwe fidia
hiyo wakati wenzake wanne wamekwishalipwa.
Alisema, amefikia hatua hiyo ya kumtaka waziri amsaidie, kwasababu
tangu imefanyika tathimini ya kwanza ya mazao ikiwa ni pamoja na nyumba yake ni
muda mrefu hata hivyo haelezwi sababu inayochelewesha fidia hiyo,hadi leo hajui
atalipwa shilingi ngapi.
Anna, alitaja mazao ambayo yalikuwemo katika shamba hilo kuwa ni
minazi, miembe, michungwa na nyumba ambapo hivi sasa mali hizo zote
zinaharibika.
Alisema, kuharibika kwa mali hizo kunatokana na serikali kumzuia
kufanya shughuli zozote za maendeleo katika shamba hilo tangu mwaka 2006.
“Kinacho nisikitisha kunahatari nikazulumiwa mali zangu kwa sababu
hivi sasa baadhi ya mazao yamekwisha haribiwa kwa mfano miembe, michungwa na
mifenesi imekatwa wakati hatujalipwa haki yetu.
“Kwa kuthibitisha hilo angalia baada ya kutufanyia tathimini ya
kwanza ambayo ilikuwa sahihi sasa wamekuja kufanya nyingine ambayo kuna baadhi
ya mazao yameishaharibiwa hivyo kupunguza thamani ya fidia, hii siikubali
nataka itumike ile ile ya kwanza,”alisema Anna.
Anna, alisema yeye ni mjane ambaye hana mtu wa kumsaidia kutokana
na mazingira hayo alitegemea angelipwa fidia hiyo mapema ili ikamsadie katika
ujenzi wa makazi mapya.
“Naomba nilipwe fidia kwani ni haki yangu inanisikitisha, ni muda
mrefu nimekuwa nikifuatilia fidia ya malipo bila mafanikio kwani napigwa
danadana katika kila ofisi za halmashauri ya korogwe sasa ndio maana nimeamua
kumuandukia barua waziri Profesa Anna Tibaijuka,”alilalamika Anna.
Aliongeza kwa kusema kuwa anamuomba waziri huyo amsaidie katika ulipwaji
wa fidia hiyo, ili iweze kumsaidia katika ujenzi wa nyumba yake ambayo paa lake
limeezuliwa na upepo.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhusu ucheleweshaji
huo, Lewis Kalinjuna:Tatizo hilo nimelisikia sikia, lakini nitalifuatilia
vizuri ili ni mjue huyo mama niweze kumsaidia.
Kuhusu ucheleweshaji wa ulipaji fidia hiyo kwa muda wa miaka nane,
Mkurugenzi huyo, alisema haoni kama kuna ucheleweshaji wowote bali alimtaka
Anna aendelee kusubiri.
No comments:
Post a Comment