Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe akichangia mjadala wa sakata la Escrow mjini Dodoma. (Na
Mpiga Picha Wetu)
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka akichangia
mjadala wa sakata la Escrow mjini Dodoma. (Na Mpiga Picha Wetu)
Wakazi wa jiji la Mbeya wakifuatilia michango ya wabunge
kuhusu sakata la Escrow mjini Dodoma. (Picha na Christopher Nyenyembe, Mbeya)
Muhongo, Werema ‘wavuliwa’ nguo
*Kamati ya
Zitto yaanika uongo wao, mawaziri
warukana
*Yadai
Mwanasheria Tanesco amebambikwa kesi ya mauaji
Na Waandishi Wetu
KAMATI ya
Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC), imeanika uongo wa Waziri wa Nishati
na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Fredrick Werema, ikionesha walivyotoa taarifa za uongo kuhalalisha uchotwaji wa
fedha zaidi ya sh. bilioni 306 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow zilizokuwa
zimehifadhiwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hatua hiyo
ilitokana wa viongozi hao kutetea kwa nguvu zote kwamba fedha hizo zilikuwa za
watu binafsi (makampuni mawili ya IPTL na Tanesco), na hivyo kupingana na
ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya
Kuzui na Kupamabana na Rushwa (Takukuru) zilizothibitisha kwamba fedha hizo ni
za Umma.
Katika kujibu
hoja za wabunge, PAC kupitia kwa wasemaji wake Dk. Khamis Kigwangala, Luhanga
Mpina, Deo Filikunjombe na mwenyekiti wake, Zitto Kabwe walisema kuwa viongozi
hao waliingilia majukunu yasiyo yao na kutumia taarifa za uongo kutetea kampuni
ya IPTL.
Walisema kuwa
haijapata kutokea katika historia ya nchi kwa serikali kuwa na waziri kama Muhongo anayesema uongo kwa kiwango kikubwa kiasi
hicho tena kwa kuurejea mara kwa mara ndani ya Bunge.
Walisema kuwa
kutokana na uongo na upotoshaji wa viongozi hao, umeisababishia serikali hasara
ya mabilioni kupitia kampuni hiyo, jambo linaloashiria kulikuwa na harufu ya
rushwa katika suala hilo
hasa ikizingatiwa uharaka uliyotumika kuhamisha fedha hiyo BoT licha ya
tahadhari kubwa iliyowekwa na Gavana.
Zitto
Katika
kujenga hoja yake, Zitto alianza kwa kuwasifu wabunge wenzake wa kambi ya
upinzani wa vyama vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akisema
waliweka tofauti zao kando na kuungana naye kutetea maslahi ya Taifa.
“Kwa muda
sasa nimekuwa na mgogo na chama changu cha Chadema, lakini katika hili tumeweka
tofauti kando, tumekaa pamoja na kujadili kama
taifa. Kwa mara ya kwanza nimehudhuria kikao cha Ukawa...nimewamiss sana wenzangu,” alisema.
Zitto alianza
kwa kuwaondoa shaka baadhi ya wabunge wa CCM waliombeza na kumbambika tuhuma za
kuhongwa, akisema hawajui uadilifu na mchango wake kwa taifa.
Alisema
kwamba fedha hiyo ya Escrow ilinyemerewa kuporwa tangu mwaka 2008 na 2009
wakati PAC ilipoleta hoja ya IPTL iondolewe chini ya mufilisi.
“Siwezi
kuwajibu wote walioniparua maana hawajui nilichokifanya kwa nchi hii. Wakati
fulani nikiwa bungeni alikuja Balozi wa Uingereza akiwa na ujumbe wake, akitaka
kufanya ushawishi ili Benki ya Standard Chartered ilipwe fedha hizo, lakini
niliwakatalia kwa sababu hawakuwa na kibali cha Waziri wa Sheria na Katiba
wakati ule; mh. Chikawe unakumbuka...labda unikane,”alisema.
Zitto
alifafanua kuwa inashangaza kuona waziri Muhonga amekuwa akihadaa Umma kwamba
ghara za umeme zinapungua na hasara ya Tanesco inaendelea kupungua, huku akitoa
takwimu za hasara iliyopatikana tangu waziri huyo aingie madarakani.
“Waziri
Muhongo alipoingia alikuta Tanesco inapata hasara ya sh. bilioni 43 lakini
mwaka mmoja tu 2012, Tanesco ilipata hasara ya sh. bilioni 117 na hadi kufikia
Desemba mwaka 2013 hasara ni sh. bilioni 467,” alisema.
Zitto alisema
kwa kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekiri kuwepo kwa utakatishaji, ukwepaji
kodi, nyaraka za kughushi zilizowasilishwa na Harbinder Singh Sethi, njia
rahisi ni mtambo wa IPTL kutaifishwa na kumilikiwa na Serikali.
Kuhusu kauli
ya Mwanasheria wa Tanesco, Godwin Ngwilimi ambaye waziri Muhongo alidai kuwa
aliomba kuacha kazi mwenyewe baada ya kubaini kwamba alifanya makosa ya kwenda
kuichunguza kampuni ya PAP nchini Malaysia bila idhini ya AG, Zitto
alisema taarifa hizo sio za kweli.
Huku
akionesha barua ya AG iliyomruhusu kufanya kazi hiyo, Zitto alisema kuwa
mwanasheria huyo alishinikizwa na Bodi ya Tanesco kuandika barua kuacha kazi
baada ya kuleta ushauri ambao haukutakiwa kwa sababu watuhumiwa tayari walikuwa
wameishagawana fedha za Escrow.
“Kijana huyu
alifanya kazi nzuri ya kizalendo kwa sababu alibaini kuwa Sethi ndiye PAP na
Sethi ndiye IPTL, na sasa amefunguliwa kesi ya mauaji ili kushughulikiwa,
serikali imlinde,” alisema Zitto na kuongeza kuwa;
Benki za nje
kama Stanbic imekwishachukua hatua za kinidhamu kwa kuwafukuza kazi wakurugenzi
wake waliohusika katika sakata hilo, kwamba hata
serikali ya Tanzania
kupitia BoT inatakiwa kuwaandikia barua Stanbic warejeshe fedhe hizo kwa sababu
miamara hiyo ilifanyika kwa uzembe wao.
Zitto
alihitimisha akiahidi kujipeleka kwenye Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na
Madaraka ya Bunge ili kuhojiwa kwa tuhuma za kuhusishwa kuhongwa fedha hizo za
Escrow akisema ni uzushi unaopaswa kudhibitishwa.
“Mimi ni
mwanasiasa na nina ngozi ngumu, wote mnajua miongoni mwa tuhuma zinamhusisha
mama yangu mzazi ambaye ametangulia mbele ya haki, hivyo naomba mnishughulikie
mimi, muacheni mama yagu apumzike,” alisema Zitto na kububujikwa na machozi. Chanzo cha Habari-Tanzania Daima, Novemba 29.
No comments:
Post a Comment