HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 13, 2015

CUF WATII SHERIA BILA SHURUTI WASITISHA MAANDAMANO YAO

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahimu Lipumba akitoa tamko la kusitishwa kwa maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanywa leo na Jumuiya ya Vijana (JUVICUF). Kushoto ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Hamidu Babal. (Picha na Francis Dande)
 Askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) wakiwa wameimarisha ulinzi jirani na Makao Makuu ya CUF jijini Dar es Salaam leo.

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof.Ibrahimu Lipumba amewasihi vijana wa chama hicho kuacha kufanya maandamano kama walivyokuwa wamepanga hapo awali.

Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho Dar es Salaam leo, Prof. Lipumba alitoa rai hiyo ya kusitisha maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanywa na Jumuiya ya Vijana (JUVICUF) kama ilivyowataka Jeshi la Polisi.

Alisema baada jeshi kuzia maandamano yao leo asubuhi alizungumza na Kamanda wa Kikosi Maalum Kamishina Suleiman Kova kuwa hawatafanya kama walivyoahidi kwa maelezo yao.

“Nilizungumza na Kova asitume jeshi lake kukamata watu hovyo kupiga watu risasi ,kuumiza hakuna sababu kwani sisi maandamano hatufanyi tena ,”alisema Prof. Lipumba.

Alisema licha ya kuzuiwa na Jeshi la Polisi lakini hoja ya vijana wa CUF ilikuwa na msingi kwa kuwa muda uliopangwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kuandikisha daftari la wapiga kura ni mdogo.

“Vijana walikuwa na hoja ya maana kwa kuwa wao ndio wengi wanatakiwa kuandikishwa katika daftari lakini muda uliotengwa ni mdogo sana kuweza kumaliza watu mil 23 wataibua vurugu mpya,”alisema Prof.Lipumba

Alisema ni jambo lisilo la kawaida kwa vituo 4015 halafu NEC iandikishge kwa siku 12 ,hi si kweli.

Alisema kunahitajika kwa vifaa (BVR) 8000 lakini hadi sasa vimepatika 250 tu ambavyo inaonesha kuwa bado hawajajiandaa kufanya zoezi hilo.

Alisema kuna wapiga kura wengi kuliko sensa ambayo imefanyika mwaka 2012 hivyo kuna haja serikali itambue hilo.
Hata hivyo alishangaa tume ya uchaguzi kufanya kazi kwa usiri mkubwa kiasi cha kwamba kinawafanya wananchi washindwe kufahamu taarifa zao.

Alisema hata ukifungua mtandao wa Tume ya uchaguzi kwa sasa utakutana na taarifa za mwaka 2001 jambo ambalo si sahihi kuwa hivyo.

Naye Mwenyekiti wa Vijana taifa Hamidu Bobali alisema kuwa wamemuheshimu mwenyekiti wao kwa kusitisha maandamano lakini sio sababu ya kuliogopa jeshi hilo.

Alisema Jeshi la Polisi halina nguvu kikatiba ya kuzuia maandamano yasifanyike na kwamba kukosa mwenyekiti wao kuwakataza wangeandamana.

“Jeshi linatakiwa kutambua kuwa watu sio wale wale kwa sasa hali imebadilika jeshi haliwezi likawaburuza wananchi na kama NEC haijajipanga itaweza kuvuruga nchi na hata kuiingiza nchi katika hali ya machafuko,”alisema Bobali.

Kutokana na CUF kutangaza kufanya maandamano hayo jeshi la polisi lilijipanga kila kona wakionekana wanapita pita na magari yao aina ya Landcruiser huku wakiwa wamebeba silaha.

Katika ofisi za tume ya uchaguzi (NEC) magari ya machozi yalikuwa yametanda na mengine kuranda randa katika maeneo hayo katika kufanya ulinzi.

No comments:

Post a Comment

Pages