Matokeo
ya kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni yamewaacha wanafunzi na wazazi wengi
kwenye majonzi huku wengine wakiwa na furaha. Hii ni kutokana na idadi ya
wanafunzi waliomaliza kuwa na matokeo ya wastani katika mitihani yao.
Pamoja na hilo, kubwa ni kuangalia namna
bora ya kusonga mbele kwa wale ambao hawakufanya vema wakijipanga upya
kuangalia ni yepi ya kufanya ili kuweza kusonga mbele baada ya jitihada zao
zilizotangulia kutofanikiwa wakati wale waliofaulu vizuri wakiweka mipango na
mikakati madhubuti itakayowawezesha kuendelea zaidi.
Jambo la kwanza analopaswa kulitambua
mwanafunzi ni kukubali matokeo aliyoyapata. Kuukana ukweli huu hakutakuwa na
msaada kwake. Ni wazi zinaweza kuwapo kasoro za hapa na pale katika masuala ya
usahihishaji lakini mchango wake katika matokeo ya jumla unaweza usiwe mkubwa
sana.
Kwa muhtasari, matokeo ya kidato cha nne
unaweza kuyagawa katika makundi yaliyopangwa katika Muundo wa wastani wa alama
katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA) ambayo ni daraja la ‘A’ kundi la fauli Uliojipambanua (Distinction) litakuwa na
alama kati ya 3.6-5.0, ‘B’ Kundi
la Kundi la ufaulu mzuri (Merit)
litakuwa na alama kati ya 2.6.3.5, ‘C’ kundi la ufaulu wa wastani (Credit) litakuwa na alama
kati ya 1.6-2.5, ‘D’ Kundi
ufaulu hafifu (Pass)
0.3-1.5 na ‘F’ Kundi
la ufaulu usioridhisha (Fail)
0.0-0.2.
Aidha unaweza kuyagawa katika makundi
manne ya walio na sifa za kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi;
wasio na sifa za kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi lakini wana
fursa za kuendelea na vyuo vingine; na waliofeli kabisa amabo wanakosa sifa za
kuendelea na masomo kwa vigezo vya ufaulu wa kidato cha nne.
Kujiunga kidato cha tano na vyuo vya
ufundi
Awali ya yote ifahamike kuwa wanafunzi
wanaochaguliwa moja kwa moja kujiunga na kidato cha tano au vyuo vya serikali
ni wale wanaotoka shuleni (school candidates) na si watahiniwa wa kujitegemea
(private candidates).
Kadhalika wanafunzi wanaochaguliwa moja
kwa moja katika vyuo vya ufundi mfano Dar es Salaam Institute of Technology
(DIT), Arusha Institute of Technology (AIT) na kama hivyo, huwa na sifa sawa na
wale wanaochaguliwa kuijunga na kidato cha tano katika michepuo ya sayansi.
Idadi ya wanafunzi hawa huwa si kubwa sana.
Mwanafunzi aliyefaulu kwa Distiction na
Merits ana nafasi kubwa ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano
au chuo cha ufundi katika shule na vyuo vya serikali. Aidha hata waliopata Credit
na Pass wana nafasi ya kuchaguliwa. Si tukio la kawaida mwanafunzi aliyepata
divisheni F kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano au chuo cha ufundi.
Mara nyingi changamoto wanayokuwa nayo
wanafunzi waliofaulu kwa viwango vya juu ni aina ya michepuo na shule za
kuendelea nazo. Ni jambo la kawaida kukuta kijana akifaulu masomo mengi na
kisha kusoma mchepuo ambao hana mapenzi nao sana. Hili husababishwa na
mazingira ya ujazaji fomu za michepuo ya kuendelea nayo baada ya kuhitimu
masomo. Hutokea kuwa mchepuo anaoupenda sana ana shaka ya kufanya vizuri na
hivyo kuchaguwa michepuo mingine. Ama kwa upande wa shule, hutegemeana na
nafasi, ufaulu wa wanafunzi na idadi ya wanafunzi walioomba katika Shule
husika.
Baadhi ya wanafunzi wanapokosa michepuo au
shule walizoomba huhangaika na kutumia muda mwingi wakitaka kubadilisha. Uzoefu
unaonyesha kwamba ni sehemu ndogo za sana ya wanafunzi hao ambao hufanikiwa.
Ushauri wetu ni kwamba endapo kijana atachaguliwa katika shule asiyoipenda na
hakuna sababu za kiafya za kumfanya asiende katika shule hiyo pengine kutokana
na hali ya hewa, au kachaguliwa mchepuo asioupenda na familiya yake haina uwezo
wa kumsomesha shule binafsi, basi atulizane katika hicho alichopata na ajikite
zaidi katika masomo kwani anaweza pia kufanikiwa katika fursa hiyo aliyoipata.
Changamoto nyingine ambayo huwakuta vijana
wa kundi hili ni kuanza kusoma tuisheni za masomo ya kidato cha tano kabla ya
uchaguzi kufanyika. Utata wa jambo hili ni kama tulioueleza hapo juu wa
mwanafunzi kuchaguliwa mchepuo tofauti kabisa na masomo anayosoma. Kwa mfano
kuna kijana tunayemfahamu akisoma masomo ya mchepuo wa Economic, Geography na
Mathematics (EGM) lakini akachaguliwa mchepuo wa History, Kiswahili na Language
(HKL). Tofauti iliyoje! Katika hilo inashauriwa kuwa kama mwanafunzi hana
hakika ya kusoma katika shule binafsi, asianze masomo hayo mpaka baada ya
uchaguzi wa kidato cha tano kufanyika. Na ikibidi kujisomea asome vitu vya
jumla kama masomo ya lugha, kompyuta nk.
Kwa wale waliokwisha amua au lazima wasome
katika shule binafsi, ni muhimu kufanya utafiti juu ya ubora wa shule hizo
kitaaluma, maadili na stadi nyingine za maisha. Aidha ni muhimu kufuatilia juu
ya kiwango cha ada, muda wa kuchukuwa na kurejesha fomu za maombi, tarehe ya
usaili na ya kufungua shule. Hutokea mwanafunzi akapoteza muda na hatimaye
kuhangaika kutafuta shule wakati shule nyingi zimeshasimamisha kupokea
wanafunzi.
Kuna wanafunzi waliopata Pass na Credit
ambao hawatapata nafasi ya kujiunga na kidato cha tano. Hata hivyo vijana waliopata
Pass na sehemu ndogo ya waliopata Credit huwa wanapata sifa na wanaweza
kujiunga na kidato cha tano katika shule binafsi endapo uwezo wa familiya
unaruhusu. Hii ni kutokana na kanuni za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
ambazo zinamruhusu mwanafunzi kuendelea na masomo ya kidato cha tano endapo
amefaulu katika kiwango cha angalau alama C kwa masomo matatu au zaidi hata
kama masomo aliyofaulu hayatengenezi mchepuo wowote mfano Civics, Biology na
English huku akiwa amepata alama D au chini yake katika masomo mengine.
Endapo familiya itamudu kumsomesha
kidato cha tano kati shule binfasi, ni vema kijana akapata ushauri wa wazazi,
walimu na wazoefu wengine juu ya mchepuo stahiki inayomfaa. Mara nyingi
wanafunzi wa aina hii huwa wanashindwa kutofautisha baina matashi ya nafsi na
uwezo binafsi wa kimasomo. Kwamba kijana tuliyemtaja hapo juu asome CBG au HGL
ni suala linalohitaji tafakuri pamoja na mhusika.
Kujiunga na vyuo vya Ualimu
Kuna wanafunzi waliopata Pass na hata
Credit ambao hawatachaguliwa kujiunga na kidato cha tano lakini watachaguliwa
kujiunga na vyuo vya ngazi ya Diploma mfano vyuo vya Ualimu. Kwa mujibu wa
kanuni zilizopo sasa, kiwango cha ufaulu cha mwisho kuchukuliwa ni Credit.
Pamoja na kujaza nafasi za masomo ya Ualimu, mwanafunzi atapaswa kuomba rasmi
nafasi hizo kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi au katika vyuo binafsi
baada ya matokeo kutoka na nafasi kutangazwa rasmi. Aidha kutokana na uchache
wa nafasi katika vyuo huwa si wote walio na sifa wanaoweza kuchaguliwa serikalini
lakini nafasi ni nyingi sana katika vyuo binafsi.
Kujiunga na Vyuo Vingine
Wapo vijana ambao licha ya kuwa na sifa za
kuchaguliwa katika vyuo vya ualimu, huwa hawachagui au hawaendi hata baada ya
kuchaguliwa kwasababu zao binfasi. Kama uwezo wa familia unaruhusu na mnaona
kusoma ualimu si kipaumbele chenu haina tatizo. Hata hivyo, ni vema kuangalia
fursa zilizopo na uwezo wa familia kiuchumi. kijana anapaswa kufahamu
kufahamishwa kuwa si busara kwa familia yenye uwezo duni wa kiuchumi, kama
zilivyo familia nyingi za kitanzania, kumsomesha kijana katika ngazi hii kwa
gharama kubwa wakati kuna wengi wanahitaji kuendelezwa kitaaluma katika
familia.
Wale wote waliokosa nafasi ya kujiunga na
kidato cha tano, vyuo vya ufundi, vyuo vya kawaida au vyuo ualimu, fursa pekee
waliyonayo ni kujiunga na vyuo vingine vinavyotoa kozi mbalimbali kama,
biashara, utawala, ufundi, nk. Vyuo kama College of Business Education (CBE),
Tanzania Institute of Accountancy (TIA), Institute of Social Work (ISW),
Institute of Information Technology (IIT) ni mifano michache katika ya vyuo
vingi vilivyopo. Changamoto kubwa katika vyuo hivi ni uwezo wa kuzimudu gharama
zake za mafunzo hayo.
Mwanafunzi aliyefeli kabisa na kupata
Sifuri (0), hana fursa yoyote katika zote zilizotajwa hapo juu. Hata hivyo
anakuwa amepata cheti cha kuhudhuria masomo (leaving certificate) ambacho huwa
na msaada fulani katika maisha kwa kuna wakati huhitajika vijana waliomaliza
kidato cha nne bila kujali ufaulu wake.
Pia kuna fursa zinazohitaji vijana
waliomaliza shule ya msingi ambazo bado zinaweza kutumiwa na vijana hawa. Kwa
mfano kuna fani mbalimbali zinazotolewa na vyuo vya VETA kama ufundi, udereva,
usafi,utunzaji bustani, upishi nk ambazo zinaweza kutumiwa vema na vijana ambao
hawakufaulu mitihani ya kidato cha nne.
Ni muhimu kutaja hapa kwamba si waliofeli
tuwanaoweza kuzitumia fursa za mafunzo ya VETA bali hata wale waliopata
divisheni Pass na hata Credit ambao ama hawakupata fursa za kuchaguliwa kidato
cha tano au familiya zao hazimudu kuwasomesha katika shule au vyuo vya
kujilipia.
Kurudia Mitihani
Wanafunzi wengi wanaofanya vibaya katika
mitihani yao, jambo la haraka linalowajia vichwani ni kurudia mitihani. Ndio
maana siku hizi vituo vinavyotoa mafunzo kwa wanaorudia mitihani vimekuwa
vikiongezeka kila kukicha. Ni kwakuwa soko linakuwa na wateja wameongezeka.
Pamoja na kuunga mkono na kuheshimu juhudi
za wanaotoa mafunzo hayo, tungependa tutanabahishe kwamba ni ili kuepusha
upotevu mwingi wa muda na pesa, ni vema mwanafunzi akawa akijiandaa kurudia
mitihani huku akijufunza ujuzi mwingine.
Uzoefu unaonyesha kuna wanafunzi
wanaorudia mitihani na matokeo yao kuwa mabaya kuliko ya mwaka uliotangulia.
Aidha kuna wanafunzi waliorudia mitihani zaidi ya mara moja na bado
hawakufanikiwa kupata alama C au zaidi (credits) tatu walizohitaji ili
wajiunge na kidato cha tano.
Endapo mwanafunzi atajiandaa kurudia
mitihani huku anapata ujuzi mwingine mfano udereva, ufundi,nk anakuwa katika
nafasi nzuri ya ajira hata asipofaulu mitihani yake anayorudia. Ni uzuri ulioje
endapo atapata vyote - credits na huku ana cheti cha ujuzi wake.
Jambo hili linawezekana endapo kijana
ataugawa vizuri muda wake chini ya muongozo wa familia kwa mfano asubuhi
akienda chuoni kupata ujuzi na jioni akienda tuisheni kwa ajili ya kurudia
mitihani. Aidha endapo mwanafunzi hatofanikiwa kupata credits, anaweza kuanza
kazi huku ajiandaa taratibu kurudia mitihani yake. Wengi wamefanikiwa kwa
utaratibu huu.
Kukata rufaa juu ya matokeo
Wapo wanafunzi ambao wanakuwa hawakuwa
hawakuridhika na matokeo waliyopata wakiamini hawakutendewa haki katika
usahihishaji pengine kwa kuzingatia rekodi za matokeo yao katika mitihani ya
shuleni au kwa jinsi walivyofanya mitihani.
Kwamba hatupingi jambo hili ndivyo pia
tungependa kusisitiza kuwa wakati ukikusudia hilo ni vema ukaendelea na mipango
mingine ya kujiendeleza kama tulivyoitaja hapo juu. Hii ni kwasababu ni
wanafunzi wachache sana ambao matokeo yao hubadilika baada ya mitihani yao
kusahihishwa upya. Aidha unaweza kupoteza muda mwingi ukisubiri hatma ya rufaa
yako na kisha majibu kuja usivyotarajia.
Ufadhili wa Masomo
Hutokea wanafunzi waliopata nafasi za
masomo katika shule binafsi au vyuo vinavyohitaji kujilipia wakawa hawana uwezo
wa kujisomesha na hivyo kuhangaika huku na kule kutafuta ufadhili. Ukweli ni
kuwa ni wachache sana ambao hufanikiwa. Hii ni kutokana na kutokuwa na taasisi
rasmi zinazotoa ufadhili katika viwango hivi ya elimu nchini.
Pamoja na kutokatishana na tamaa, ni vema mtu unapokuwa
katika hali hiyo kutafuta shughuli itakayokuwezesha kujenga nguvu za kiuchumi
na kisha kuweka akiba kwa ajili ya kujisomesha. Unaweza kuweka malengo ya
kusoma huku ukifanya kazi. Endapo shughuli zako hazikupi fursa ya kusoma huku
ukifanya kazi, unaweza kuahirisha kusoma hadi kipindi fulani baada ya
kujiimarisha kiuchumi. Endapo hilo litakuwa gumu kulitekeleza, familia iangalie
uwezekano wa kuuza sehemu ya rasilimali endapo inazo na ambazo hazitaithiri
familia nzima endapo zitauzwa.
Tuhitimishe kwa kusema, matokeo vyovyote
yawavyo hayawezi kuwa ndio mwisho wa maisha. Siku zote wanaofanikiwa ni wale
wanaotazama mbele huku wakijifunza kwa yaliyowatokea. Walofaulu washukuru huku
wakijipanga; waliofanya vibaya wasubiri huku wakijifuza. Tumia vizuri kila
fursa unayoipata bila kujali udogo wake. Jifunze kwa wengine, uliza, pata
miongozo kwa waliokutangulia, na amini kuwa ipo siku ufanikiwa. Washindi
hawaachi, na wenye kuacha hawashindi.
KUVUNJIKA KWA KOLEO SI MWISHO WA UHUNZI
Kwa Msaada zaidi wa ushauri na namna bora
ya kusoma tafadhali wasiliana nasi kwa namba 255 767 488856
au barua pepe marshk86@hotmail.com
No comments:
Post a Comment