WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amewataka
wahamiaji haramu waliovamia kwenye mapori ya akiba, kuondoka mara moja kabla
hatua kali za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Pia amewaagiza askari wa wanyamapori nchini kukamata na
kutaifisha mifugo yote ya wahamiaji haramu inayokamatwa kwenye mapori hayo ya
akiba na fedha hizo zitumike kwenye ujenzi wa maabara na ununuzi wa madawati katika
shule zilizopo jirani na mapori hayo.
Akizungumza na wafugaji pamoja na askari wa wanyamapori katika
Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, Waziri Nyalandu alisema, kumekuwa na wimbi kubwa
la wahamiaji haramu kutoka nchi jirani za Rwanda, Kenya, Burundi na Uganda
ambao wameingia na mifugo yao kwenye mapori ya akiba katika wilaya hiyo.
Alisema rasilimali zilizopo katika nchi hii ni mali ya Watanzania
hivyo mgeni yeyote anayetaka kuingia na kufanya shughuli zake hapa nchini, ni lazima
afuate sheria, taratibu na kanuni za nchi.
Amepiga marufuku kwa askari wa wanyamapori nchini kuwapiga risasi
ng’ombe kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria.
Alisema ni marufuku kwa askari wote kuwatesa raia
wanapowakamata wakati wakifanya shughuli
za ujangili, ufugaji au uhalifu wa aina yoyote ndani ya hifadhi kwani nchi hii inaendeshwa
kwa misingi ya sheria za haki za binadamu na utawala bora.
Amesisitiza kuwa, yeye kama waziri mwenye dhamana hatamvumilia
askari yeyote atakayethubutu kuvunja sheria kwa makusudi ilhali akijua utaratibu
anaopaswa kuchukua pindi anapomkamata mtuhumiwa.
Ameahidi
kukutana na wafugaji wote nchini wanaotokea kwenye maeneo yenye migogoro na
uhifadhi wakiwapo wabunge wao kwa lengo la kutafuta suluhu ya migogoro kati ya wahifadhi
na wafugaji.
No comments:
Post a Comment