HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 06, 2015

NYUMBA 354 ZAATHIRIKA NA MVUA ZANZIBAR

 Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya kukabiliana na Maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Mzee  Salhina Abdi Mkufau wa Shehia ya Jang’ombe ambye nyumba yake imebomoka baada ya kuzibuka kwa shimo kubwa pembezoni mwa kuta ya nyumba hiyo. Nyuma ya Balozi Seif  ni Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe Mheshimiwa Salum Suleiman Nyanga. Picha na –OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akikiongoza Kikao cha dharura cha Kamati ya Taifa ya kukabiliana na maafa Zanzibar kilichokutana ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kuthathmini athari ya mvua zilizoleta maafa Zanzibar.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Inakadiriwa kwamba kwa Taarifa za awali zaidi ya Nyumba 354 zenye wakaazi wapatao elfu 2,117 zimeathirika vibaya kufuatia Mvua kubwa zilizonyesha kuamkia Tarehe 3 Mei 2015  katika Kisiwa cha Unguja.

Kwa mujibu wa Taarifa na Utafiti wa mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar  umebainisha kwamba mvua hizo kubwa zimefikia Milimita 172.2    kiwango kikubwa kuwahi kutokea katika Historia ya Zanzibar  ikilinganishwa na kile kilichowahi kuripotiwa hapa Zanzibar cha  Tarehe  7 Mei mwaka 1972 kilichofikia Milimita 114.

Kikao cha Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na maafa Zanzibar kilikutana chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Piliwa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi kilikutana kwa dharura kujadili Taarifa juu ya Tathmini ya athari za Mvua zilizotokea Tarahe 3 Mei 2015.

Akiwasilisha Taarifa ya awali juu ya tathamnini ya athari hiyo Katibu wa Kamati ya Taifa ya kukabiliana na maafa Zanzibar ambae pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohammed alisema athari kubwa zilizojitokeza ni pamoja na kufariki kwa watu watatu, kuchimbika mashimo makubwa katika baadhi ya maeneo pamoja na kukatika katika kwa bara bara.

Dr. Khalid aliyataja maeneo yaliyoathirika na mvua hizo kuwa ni pamoja na Magomeni, Jang’ombe, Karakana, Nyerere, Sebleni, Mwanakwerekwe, Sogea, Welezo, Kisauni, Tomondo, Mombasa, Kinuni, Mtopepo, Chumbuni, Kwahani, Mpendae,Pangawe, Bububu na Kwaalinato,

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ya Kitengo cha kukabiliana na Maafa kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa Mjini Magharibi, Wilaya zake na Majimbo na Shehia husika ilichukuwa hatua mbali  mbali za kujaribu kukabiliana na maafa hayo.

Katibu huyo wa  Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar alizitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwa ni pamoja na kufanya tathmini ya kina kujua idadi kamili ya walioathirika na ukubwa wa athari iliyotokea.

Alifahamisha kwamba Serikali imelazimika kuzihamisha familia  zilizokosa makaazi kwa kuwaweka katika kambi maalum ya muda katika skuli ya Mwanakwerekwe “C”  pamoja na kuwapatia huduma za kibinaadamu  ikiwemo kuwafariji wafiwa kwa kuwapatia ubani kwa kila familia.

Wakichangia Taarifa hiyo wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na maafa Zanzibar wameshauri kufanywa kwa Tafiti za Kisayansi juu ya mwenendo wa maji ili kujua sababu za atahri za mvua katika maeneo yaliyoathirika.

Wajumbe hao walisema ukosefu wa ushirikiano baina ya Taasisi za umma zinazopaswa kutoa maamuzi pamoja na kuendekezwa undugu kwa baadhi ya viongozi katika kusimamia maamuzi magumu ndio sababu kubwa inayowafanya baadhi ya watu kuwa masugu katika utekelezaji wa sheria za Nchi.

Mkurugenzi wa Idara ya Majenzi Zanzibar Mhandisi Ramadhan Mussa Bakari alisema Jamii inapaswa kuheshimu njia za Kimaumbile zinazopitisha maji katika maeneo yote nchini hasa yale ya Mkoa wa Mjini Magharibi ili kupunguza baadhi ya maafa yanayoweza kuepukwa.

Mhandisi Ramadhan alisema ujenzi holela usiozingatia mipango Miji unaofanywa na baadhi ya Watu hasa katika Maeneo ya Mabonde na michirizi inayopitisha Maji ya mvua  na mito huchangia maafa wakati zinapotokea mvua kubwa.

Akitoa nasaha zake Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na maafa Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza ushirikiano ulioonyeshwa na Wananchi katika maeneo mbali mbali ya maafa ambao umesaidia kuwahifadhi wenzao katika majanga hayo ya mvua.

Balozi Seif alisema huo ni uzalendo mkubwa unaopaswa kuendelezwa katika Nyanja zote na kuwaomba wahisani pamoja na watu wenye uwezo wa aina zote kusaidia kuunga mkono juhudu zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na maafa hayo pamoja na kuwapatia msaada wananachi waliokumbwa na kizaazaa hicho.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Taifa ya Kukabiliana na maafa Zanzibar pia waliwaomba wananchi kuendelea kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa Afya katika kujilinda na miripuko ya maradhi  ya kuambukiza yanayoweza kutokea wakati huu.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipta muda wa kuzuru baadhi ya maeneo yaliyoathirika na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Tarehe 3 Mei Mwaka 2015 na kuzifariji familia zilizokumbwa na maafa hayo.

Balozi Seif alizuru shehia ya Kara kana ambayo wakaazi wake wengi wamehifadhiwa katika Kambi ya Dharura ya Mwanakwerekwe “C” baada ya Nyumba zao 80 kuja maji ambapo 37 zimejaa Maji na Tano  zimedidimia na kuvunjika kabisa.

Balozi Seif pia akaangalia athari ya mmong’onyoko wa ardhi uliosababisha kukatika na kudidimia kwa  baadhi ya kuta za Nyumba za Shehia ya Jang’ombe pamoja na Mwanakwerewe.

Akiwafariji na kuwapa pole wananchi waliothirika na maafa hayo Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kuona Wananchi wake waliopatwa na kadhia hiyo  wanarejea katika maisha yao ya kawaida.

“ Hali inatisha sana kutokana na maafa haya. Ukweli umefika wakati Wananchi wenyewe tulazimike kuwa na hadhari za ujenzi katika maeneo ya mabonde na kuacha tabia ya kuhama wakati inapotokea mafuriko na kurejea wakati wa kiangazi “. Alitahadharisha Balozi Seif.

Mapema Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar Nd. Beid Juma alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na Wananachi wa Karakana kwamba Wizara ya Fedha Zanzibar inafikiria kuchukuwa hatua za kuhudumia ujenzi wa mtaro mkubwa wa kutoa maji ya mvua katika eneo hilo.

Nd. Abeid alisema hatua za awali za kufanya tathmini na utafiti zimeanza kuchukuliwa katika ujenzi wa mtaro huo unaotarajiwa kuwa na urefu wa Mita tisa kupitia mkopo wa fedha za ujenzi huo utatolewa na Benki ya Dunia { W B } ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahusika na kulipa fidia kwa nyumba zitakazopita Mradi huo.

Taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar zinasisitiza kwamba muendendo wa pepo bado unaashiria dalili za kuendelea kuwepo kwa mvua kubwa hapa Zanzibar katika mwezi huu wa Mei zinazoweza kusababisha athari za mafuriko.



Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Pages