HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 29, 2015

ROSE MUHANDO KUPAMBA TAMASHA LA AMANI DAR

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Amani, Alex Msama akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu waimbaji watakaotumbuiza katika tamasha hilo litakalofanyika Oktoba 4 kwenye uwanja wa taifa. Kushoto ni Mratibu wa tamasha hilo, Benno John Chelele.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Amani, Alex Msama akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu waimbaji watakaotumbuiza katika tamasha hilo litakalofanyika Oktoba 4 kwenye uwanja wa taifa. Kushoto ni Mratibu wa tamasha hilo, Benno John Chelele.



Na Mwandishi Wetu


MALKIA wa muziki wa Injili nchini na Afrika Mashariki na Kati, Rose Muhando, amethibitishwa kushiriki tamasha maalum la Kuombea Amani Uchaguzi Mkuu litakalofanyika Oktoba 4, jijini Dar es Salaam.

Muhando, anakuwa mwimbaji wa nne kutajwa katika orodha ya watakaopamba tukio hilo linalobeba umuhimu wa aina yake katika kuhimiza na kusisitiza amani na utulivu wakati na baada ya uchaguzi mkuu wenye ushindani mkubwa.

Mwanadada huyo mwenye sauti, uwezo na vipaji vya aina yake katika huduma hiyo ya uimbaji, anaungana na wakali wengine kama Bonny Mwaitege, Christopher Mwahangila na Upendo Nkone.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Alex Msama ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo litakalofanyika mikoa 10 nchini, alisema Rose tayari amethibitisha.

"Maaandalizi ya Tamasha la kuombea amani ya nchi yetu ambayo ni tunu ya aina yake tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu,  yanakwenda vizuri kwani Rose naye ataungana na wengine siku hiyo,” alisema Msama.

Msama alisema Tamasha hilo linalolenga kuwaleta pamoja watanzania bila kujali tofauti zao za dini, kabila, itikadi wala rika, litahudhuriwa pia na viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwamo wale wa kiroho kwa ajili ya kuombea amani uchaguzi mkuu.

Alisema wakiwa waratibu wa matamasha ya muziki wa injili kwa miaka mingi sasa, wameona ni jambo jema kuwaleta pamoja watu kuomba Mungu uchaguzi mkuu uwe wa amani na utulivu.

Msama alisema hilo ni jambo muhimu kwa kuzingatia baadhi ya mitafaruku ya kisiasa imekuwa ikianzia katika harakati za uchaguzi, hivyo ni suala la busara kumwomba Mungu autangulie uchaguzi huo na watu wake.

Alisema siku hiyo maelfu yatakayojitokeza wakiongozwa na watumishi wa Mungu, wataukabidhi mikononi mwa Mungu uchaguzi huo ili uweze kufanyika kwa amani na utulivu bila kuacha makovu na athari kwa wananchi.

                                            Msama alisema, mbali ya kuuombea uchaguzi mkuu, Tamasha hilo pia litatumika kumuaga rasmi Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye amekuwa mdau mkubwa wa muziki wa injili nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages