HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 29, 2015

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR ATEMBELEA MAENEO YA HIFADHI YA MSITU

   Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akitembelea msitu wa hifadhi Muyuni kuangalia maeneo ambayo baadhi ya watu wameamua kulima kilimo chengine mchanganyiko. Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Kilimo na Maliasili Mh. Sira Ubwa Mwamboya na kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dk. Idriss Muslim Hijja.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
 
Tamaa za baadhi ya watu kujimilikisha maeneo ya ardhi kwa nia ya kupata utajiri wa haraka chanzo cha uchafuzi wa mazingira katika hifadhi ya msitu wa Muyuni Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.

Kauli hiyo ilitolewa wanakamati na wananchi wa shehia ya Muyuni “B” ambayo ilionyesha mgongano baina yao wakati wakimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika katika Msitu huo kuangalia maeneo ya Hifadhi ya Msitu ambayo wahusika wanayatumia kwa kilimo.

Eneo la ardhi lililokubalika kutumiwa kuwa hifadhi ya Msitu na Wananchi wote wa  Shehia  Tatu za Muyuni A,B na C kwa takriban miaka 10 limekuwa na mgogoro  wa matumizi kwa miaka minane tangu kutolewa uamuzi wa kila shehia iunde Kamati yake ya Uhifadhi badala ya ile ya pamoja ya shehia hizo.

Wanakamati pamoja na wananchi walisema wamekuwa na malengo ya kuyatumia maeneo hayo na baadae kuyauza kwa vile tayari yamekuwa rasilmali kubwa katika masuala ya uwekezaji vitege uchumi katika sekta ya Utalii.

Walisema tabia ya baadhi ya wananchi wenzao ya kuanza kilimo cha minazi na miti mengine ya matunda na biashara pamoja na kisingizio cha sababu za kushutumiana kwa itikadi za kisiasa imechangia  kuvuruga eneo kubwa la hifadhi hiyo muhimu kwa hatma yao na vizazi vijavyo.

Akitoa nasaha zake kwa wana Kamati pamoja na Wananchi hao wa Muyuni “ B “ Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushauri kuhusiana na mgogoro huo wa hifadhi ya Msitu wa Muyuni hapo baadaye.

Balozi Seif alisema utaratibu maalum utaandaliwa katika kulitafutia ufumbuzi  tatizo hilo kwa kuhusisha Viongozi wa Taasisi za Kilimo, Ardhi na Maingira ambapo wahusika hao watakuwa na uamuzi wa kuwaita watu waliohusika na mgogoro huo katika kuwahoji na kutaka ufafanuzi.

Alisema nia ya Serikali Kuu ni kuona hifadhi ya Msitu wa Muyuni inaendelea kubakia kwa maslahi ya Wananchi wa eneo hilo pamoja na Taifa zima kwa vile eneo hilo tayari limeshatangazwa ndani ya Gazeti la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza  Wananchi hao kwamba Zanzibar ikiwa niongoni mwa baadhi ya Mataifa ya Bara la Afrika imebahatika kuwa na rasilmani nzuri za maumbile lakini baadhi ya watu wamekuwa na tabia mbaya ya kuharibu kwa makusudi rasilmali hizo.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Mali asili Zanzibar Dr. Bakar Ased alisema eneo hilo la hifadhi hivi sasa baadhi ya sehemu linatumika kwa shughuli za kilimo kinyume na lengo lililokusudiwa kwa makubaliano ya Wananchi wenyewe na idhini ya Serikali.

Dr. Ased aliwatanabahisha Wananchi hao kwamba licha ya eneo hilo kulengwa kuwa hifadhi ya misitu  lakini pia wataalamu wa mazingira na hali ya hewa wamefanya utafiti na kutoa ripoti iliyoeleza kwamba  Ukanda wa Kusini ni eneo zima lenye Hewa safi.

Alisema kuvurugwa kwa  hifadhi hiyo  kwa shughuli nyengine za kilimo kunaweza kukasababisha kuwa  chanzo cha uchafuzi wa hali ya mazingira na matokeo yake ni athari kwa viumbe hapo baadaye.

Kuna sehemu kubwa ya Eneo la hifadhi ya misitu la Muyuni ambayo kwa sasa in atumika kwa shughuli za kilimo mchanganyiko kama miembe, Minazi, Mivinje ,Migomba pamoja na mazao madogo madogo ya mizizi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
29/11/2015.

No comments:

Post a Comment

Pages