Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Flugence Ngonyani akipeana mkono mbunge wa Vunjo, James Mbatia
wakati wa hafla ya kukabidhi Kituo cha
Polisi kilichojengwa kwa msaada na Benki ya CRDB katika kata ya Marungu mkoani
Kilimanjaro, mwishoni mwa wiki. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
CRDB, Dk. Charles Kimei. (Na Mpiga Picha Wetu)
NA MWANDISHI WETU, MARANGU
WAKAZI zaidi ya 30,000 wa Kata ya Marangu Mashariki, Wilaya
ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro jana walikabidhiwa kituo kidogo cha
polisi na uongozi wa Benki ya CRDB.
Uwepo wa kituo hicho cha polisi utapunguza uhalifu kwa kuwa
wakazi wa eneo hilo ambao hawajapata kuwa na huduma hiyo hali inayowafanya kufuata
huduma za usalama katika Kituo cha Polisi Himo kilichopo umbali wa kilomita 20.
Akizungumza wakati wa kukabidhi kituo hicho, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB iliyoanzishwa mwaka 1996; Dk. Charles Kimei, alisema
ujenzi huo umegharimu sh. milioni 125 na kubainisha kuwa ni mwendelezo wa sera
ya benki hiyo ya kuisaidia jamii.
“Benki ya CRDB ni mdau wa maendeleo, inathamini usalama wa
raia na mali zao… tunatambua taifa bora ni lile lenye usalama katika shughuli
za uzalishaji mali.
Akitoa shukrani zake kwa niaba ya Jeshi la Polisi mkoani
Kilimanjaro, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Fulgence Ngonyani, alisema ujenzi wa kituo
hicho ni msaada mkubwa katika kuboresha
utendaji wa Jeshi la Polisi kwa kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Ifahamike kuwa kituo hiki ni sehemu ya ulinzi, lakini
jukumu lipo mikononi mwa wananchi. Kazi yetu polisi itafanikiwa iwapo
mtashirikiana nasi kurahisisha utendaji wetu,” alisema Kamanda Ngonyani.
Ujenzi wa Kituo cha Polisi Marangu ni moja ya misaada
inayotolewa na Benki ya CRDB kwa mwaka 2015, ambapo mpaka sasa imetumia zaidi
ya sh. milioni 270 kusaidia jamii.
No comments:
Post a Comment