HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 06, 2015

Kongamano la Shiloh laanza kwa kishindo Mlima wa Moto

Mchungaji  Kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God, Dk. Getrude Rwakatare akiongoza ibada maalum ya kuliombea taifa pamoja viongozi wa serikali ya awamu ya tano wakati wa uzinduzi wa tamasha la Shiloh lililofanyika jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)
Baadhi ya waumini wakiwa katika tamasha la Shiloh.

Na Mwandishi Wetu


MWIMBAJI mahiri wa nyimbo za Injili nchini, Bahati Bukuku yu miongoni mwa watakaopamba Kongamano la Shiloh lililoanza jana katika Kanisa la Mlima wa Moto Assemblies of God Mikocheni B, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwaleta pamoja watu wa Dini na makabila tofauti kuutafakari ukuu wa Mungu na kumshukuru kwa matendo yake makuu kwao na taifa kwa mwaka mzima.

Mbali ya Bukuku anayetamba na vibao mbalimbali vilivyobeba ujumbe murua wa Neno la Mungu, waimbaji wengine watakaohudumu katika Kongamano hilo la siku saba, ni  Goodluck Gozbert, Furaha Isaya, Happy Choir, Joy Bringers, Mass Choir ya Mlima wa Moto, Gideon Mutalemwa  na wengineo wengi.

Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo, Mchungaji Kiongozi Dk. Getrude Rwakatare alisema mbali ya kumshukuru Mungu kwa kuivusha nchi salama katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, litatumika pia kumuombea Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli na serikali ya Awamu ya Tano.

“Tumekuwa tukiandaa Kongamano hili la Shiloh kila mwaka kwa ajili ya kufanya maombi na maombezi kwa siku saba kuelekea kuumaliza mwaka. Lakini, kwa mwaka huu tutalitumia Kongamano hili kumuombea Rais Dk. Magufuli na viongozi wengine wa Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema Mchungaji Rwakatare.

Alisema, wateule wa Mungu hawana budi kusimama katika zamu yao kwa niaba ya Watanzania kumshukuru Mungu kwa hali ya amani na utulivu iliyopo nchini, pia kumshukuru Mungu kwa kuwapatia Rais mzuri, pia kuzidi kumkabidhi mikononi mwa Mungu azidi kumpa hekina na maarifa katika uongozi wake.

Aliongeza, mbali ya Kongamano kubeba ajenda hiyo, pia kusanyiko hilo la watu kutoka dini na makabila tofauti watumia siku hizo saba kumfakari huyo Mungu sambamba na mambo mengine mengi ambayo mara nyingi huambatana na tukio hilo ambalo hufanyika mara moja kwa mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013.

Alisema, ingawa lilizinduliwa majira ya saa 3;00 asubuhi, kwa siku za kawaida yaani kuanzia leo Kongamano hilo la aina yake litakuwa linaanza majira ya saa 9 alasiri ili kutoa fursa kwa watu wengi kushiriki baada ya kutoka katika majukumu mengine ya ujenzi wa taifa.

Kongamano hilo ambalo pia linahudhuriwa na Askofu Danstan Maboya na watumishi wengine wa Mungu kutoka mikoa ya Singida, Shinyanga, Dodoma Mwanza, Kilimanjaro na wengineo, ni mara ya tatu kufanyika tangu lianzishwe kwa lengo la kutoa fursa watu wa dini na makabila mbalimbali kumshukuru Mungu kwa mambo makuu aliyowajalia kwa maka mzima.

No comments:

Post a Comment

Pages