Afisa
Mdhamini wa ZSTC Pemba Abdulla Ali Ussi akitoa maelezo baada ya Magunia ya Karafuu Kavu kukamatwa na Kikosi cha
KMKM katika Ufukwe wa Bahari ya Chanjaani Mtambwe ambazo zilikuwa katika
harakati za kutaka kusafirishwa kwa njia ya Magendo. Anaemsikiliza ni Kamanda
wa KMKM zone ya Pemba, Silima Hija Hija.
Baadhi
ya Wafanyakazi wa Shirika la ZSTC wakipita mbele ya Rais Mhe. Dkt. Ali Mohmaed
Shein wakiwa wamebeba bango lenye ujumbe wa kupinga magendo ya zao la karafuu
katika maazimisho ya siku ya Wafanyakazi duniani, Mei Mosi 2015.
Na
Ali Mohamed, Zanzibar
Magendo ni vitendo viovu vinavyohusisha uingizaji au usafirishaji
wa bidhaa au mazao kwa njia zisizo halali/kisheria kwa lengo la kukwepa kodi na
kukiuka sheria ambapo ni njia haramu ya kufanya biashara. Sababu kuu za magendo
ni tamaa ya utajiri, ujinga na kukosa uzalendo.
Ni dhahiri kuwa magendo yana athari kubwa kwa maendeleo ya nchi na
Wananchi wake, huikosesha serikali mapato ambayo ndio yanayohitajika katika
kuimarisha huduma za jamii kama vile utoaji wa elimu, afya, maji safi na
salama, ujenzi wa miundombinu ya barabara na huduma nyengine muhimu.
Karafuu
ni zao kuu la uchumi wa Zanzibar linalosaidia upatikanaji wa fedha za kigeni na
kuiwezesha Serikali kuimarisha huduma za jamii. Katika kipindi cha miaka ya
1980 na 2010 zao hili lilikuwa katika changamoto kubwa ya kusafirishwa kwa
magendo. Baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu walikuwa wakisafirisha zao hili kwa
magendo kwenda katika nchi za jirani.
Katika wakati huo usafirishaji magendo wa zao la karafuu ulikuwa
mkubwa kiasi cha kuzifanya nchi hizo za jirani kuwa wauzaji wakubwa wa zao la
karafuu kwa zaidi ya tani 2,000 katika soko la dunia huku ikizingatiwa kuwa
katika nchi hizo hakuna mikarafuu inayolimwa.
Wakati nchi hizo zikionekana kuuza karafuu kwa kiwango hicho,
uzalishaji wa zao hilo kwa Zanzibar ulishuka kutoka tani 9,952 hadi tani 2673
katika kipindi cha miaka kumi, sababu moja ikiwa ni karafuu za Zanzibar
kusafirishwa kwa magendo kwenda katika nchi hizo za jirani.
Katika kipindi hicho cha mwaka 2000 hadi 2010, Zanzibar ilipoteza
kiasi cha dola za kimarekani milioni 16, sawa na TZS bilioni
34.7 kutokana na usafirishaji karafuu kwa magendo.
Kwa
mujibu wa sheria ya ZSTC ya mwaka 2011 kifungu cha 9 (a) Wakulima na
Wafanyabiashara wa zao hilo la karafuu wanatakiwa kuuza karafuu zao Serikalini
tu kupitia Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) ambayo ni taasisi pekee
iliyopewa mamlaka ya kununua na kuuza karafuu, hivyo kufanya magendo ya karafuu
ni makosa.
Kulikuwa
na sababu nyingi zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya watu ikiwemo suala la bei
ya karafuu kuwa ndogo na kusababisha watu kuamua kuziuza karafuu zao kimagendo
nje ya nchi kwa lengo la kutafuta bei nzuri.
Kwa
lengo la kuimarisha, kulinda ubora na kuwahamasisha Wakulima kuuza karafuu zao
Serikalini kupitia vituo vya ununuzi vya ZSTC badala ya kusafirisha kwa
magendo, mikakati mbali mbali ilipangwa na kutekelezwa na Serikali.
Mwaka 2011 Serikali ilitoa ahadi na kuitekeleza ahadi hiyo ya
kuwalipa Wakulima wa zao la karafuu asilimia 80 (80%) ya bei ya karafuu ya soko
la dunia. Karafuu za daraja la kwanza zinanunuliwa kwa bei ya TZS 14,000 kwa
kilo badala ya TZS 5,000 kwa kilo, bei iliyokuwepo mwaka 2010. Ongezeko
hili ni sawa na asilimia 180.
Kadhalika, vituo vipya vya ununuzi na uuzaji wa karafuu
vimejengwa, vituo vya zamani vimekarabatiwa ambapo idadi kamili ya vituo vyote
ni 35 Unguja 3 na Pemba 32, huduma zote muhimu zimeimarishwa kwenye vituo hivyo
na ulinzi pia umeimarishwa zaidi katika kudhibiti magendo.
Mkakati mwengnie uliochukuliwa ni kwa Shirika la ZSTC kujipanga
vyema katika suala la upatikanaji wa kifedha kwa wakati na kulipa fedha taslim
kwa Wakulima wa zao la karafuu na kuhakikisha hakuna Mkulima anaekopwa karafuu
zake anapokwendwa kuuza.
Utekelezaji wa mikakati hiyo imesaidia sana kufanikiwa kudhibiti
magendo ya karafuu, hivi sasa Wananchi wanauza karafuu zao katika vituo vya
ununuzi vya ZSTC. Ni jambo la kuwashukuru na kuwapongeza Wakulima, Wananchi na
Vikosi vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri walioifanya ya kushirikiana na
Serikali katika kupambana na magendo ya karafuu.
Pamoja na mikakati na jitihada hizo zilizochukuliwa na Serikali
kudhibiti magendo ya karafuu kufanikiwa kwa kiwango kikubwa lakini
inaonekana kuwa bado wapo watu wachache wanaendeleza biashara hiyo haramu.
Katika msimu wa mavuno mwaka 2015/2016 gunia 33 za karafuu kavu na gunia 31 za
makonyo zimekamatwa ambazo zilikuwa zinasafirishwa nje.
Lakini kabla Mkulima hajafikiria suala la kuuza karafuu zake kwa
njia ya magendo, anapaswa kwanza ajiuulize masuali yafuatayo;-Ni nini
anachotaka zaidi ilhali karafuu zimeongezwa bei na bei hiyo ni kubwa zaidi ya
huko anakokwenda kuuza kwa magendo?
Pia kwa nini anafanya magendo llhali pamoja na bei nzuri lakini
pia faida ya karafuu ikirudishwa ndani ya nchi ndio hupatikana elimu bora kwa
mwanawe, afya bora kwake, barabara nzuri kwa wote, maji safi kwa kila mtu na
maendeleo kadhaa wa kadhaa?
Inakuwaje mtu anajitia katika magendo ya karafuu ilhali uwezekano
wa kupoteza maisha yake ni mkubwa au uwezekano wa kukamatwa na kufungwa na
kupoteza utumishi wake kwa familia yake na kuitia katika mateso, kwa nini
anafanya hivyo?
Ni kwa sababu gani za msingi watu ambao wanauwezo wa kupata kiasi
kikubwa cha fedha kwa kuuza karafuu zao serikalini waingie katika tombola ya
kukosa kabisa kwa kujaribu kuingia kwenye magendo na kuhatarisha mali zao kwa
kuzama baharini au kufilisiwa na kubaki katika umaskini kwa kukosa fedha za
Serikali na zile ambazo walizitarajia kuzipata kwa kuuza magendo huko nchi za
jirani?
Ni wazi kuwa anachokosa mtu huyo ni uzalendo na uwezo mzuri wa
kufikiri.
No comments:
Post a Comment