Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
imeipongezaSerikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa
kujenga jengo zuri la tatu la abiria (TB III)
litakaloboresha zaidi huduma za usafiri wa anga.
Pongezi hizo zimetolewa na
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Norman Sigalla (Makete) wakati Wajumbe wa
Kamati hiyo walipotembelea jengo hilo katika ziara yao ya kukagua miradi ya
Serikali mwanzoni mwa wiki.
Jengo hilo linajengwa katika
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kwa Euro milioni 254
(sh. Bilioni 560) za mkopo kutoka Benki ya HSBC ya Uingereza na CRDB kwa
dhamana ya Serikali ya Tanzania na Uholanzi.
Tayari TAA imeshamlipa
Mkandarasi wake, Bam International ya Uholanzi, Euro milioni 96 baada ya
kukamilisha asilimia 60 ya kazi. Jengo hilo linajengwa kwa awamu mbili ambapo
awamu ya kwanza ipo katika hatua za mwisho.
Mwenyekiti Sigalla na Wajumbe
wengine wa Kamati hiyo walieleza kuridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na
Serikali kujenga jengo hilo linalotarajiwa kukamilika Desemba 2017.
Baada ya kufurahishwa na kazi
hiyo nzuri na kushauri uboreshaji zaidi wa utendaji, wabunge waliahidi
kuisukuma Serikali iiwezeshe zaidi TAA kifedha ikamilishe miradi yake kwa
wakati.
Walisema hayo baada ya kupokea taarifa za
utendaji na miradi ya TAA kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mhandisi
George Sambali na Mkurugenzi anayesimamia Mradi wa TB III, Mhandisi Mohammed
Millanga.
Pia walipokea taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha aliyeeleza uhaba wa fedha
wanazopewa unavyowaathiri katika kuendesha shughuli nyingi za kiwanja hicho
ambacho ni kitovu cha mapato ya TAA.
TAA inayosimamia viwanja 58
vya ndege vya Serikali Tanzania Bara, hukusanya zaidi ya sh. Bilioni 67 lakini
hupewa sh. Bilioni 17 tu kwa ajili ya kujiendesha huku JNIA ikipata sh. Milioni
700 tu kwa mwezi ukitoa za mishahara.
Taarifa za watendaji TAA zilionesha maendeleo ya
miradi ya ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege inayoendeshwa na
kusimamiwa na TAA, jengo la TB III, ukarabati JNIA, changamoto zake kubwa na
mipango ya Serikali kuzitatua.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA,
Mhandisi Sambali alieleza dhamira ya TAA kuwa na kiwanja kipya cha ndege nje ya
Dar es Salaam au kupanua JNIA kwa kuongeza njia zaidi za kurukia ndege ifikapo
2030.
Hata hivyo, aliwaeleza
wabunge changamoto ya TAA kutekeleza dhamira hiyo kuwa ni ulipaji fidia kwa
wananchi na reli ya TAZARA kupanua eneo la sasa la JNIA au kupata zaidi ya dola
milioni 500 kuanzisha kiwanja kipya nje ya Dar es Salaam.
Wabunge waliitaka TAA kufanya
tathmini ya gharama za upanuzi wa JNIA kwa kulipa fidia wananchi na kuhamisha
reli ya Tazara au kujenga kiwanja kipya
nje ya Dar es Salaam ili kuangalia uwiano kwa lengo la kuishauri Serikali
mapema zaidi kabla ya 2030.
Wabunge walilalamikia ukosefu
wa ndege za kutoa huduma na zilizopo kutoza nauli kubwa wakati Serikali
inaboresha zaidi miundombinu.
Mhandisi Sambali alieleza
ukosefu wa ndege unatokana na ushindani wa kibiashara wa mashirika ya ndege
ambapo mengine hayaji kwa kukosa abiria wanaounganisha safari za nje.
Pia alieleza Serikali
kutokuwa na shirika imara la ndege kufuatia ATCL kuwa na ndege moja tu
kumefanya asilimia 90 ya abiriawatumie nchi za jirani kuunganisha safari za nje.
Kufuatia maelezo hayo,
wabunge waliitaka Serikali inunue ndege nne ili ATCL irudi hewani kutekeleza agizo la Rais Dkt.
John Magufuli.
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani alisema wamepokea rai ya
wabunge akisisitiza dhamira ya Serikali ni kununua ndege.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA UHUSIANO
MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA)
MACHI 30, 2016
No comments:
Post a Comment