HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 30, 2016

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamchagua Spika

 Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid  akila kiapo  cha Utii cha kulisimamia baraza hilo mara baada ya kupigiwa kura kutoka kwa wajumbe wa baraza hilo huko Chukwani nje kidogo ya mji wa zanzibar.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Kikao cha kwanza cha baraza la Tisa la uwakilishi Zanzibar kimeaza leo kwa kumchagua spika wa baraza hilo ambaye atakitumikia chombo hicho kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Wajumbe 76 walishiriki kumpigia kura Mgombea pekee wa nafasi hiyo ambaye ni Zubeir Ali Maulid kutoka chama cha mapinduzi (CCM).

Shuhuli hiyo ya kumchagua spika ilifanyika huko katika Jengo la Baraza Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Akimtangaza Spika huyo katibu wa Baraza hilo Yahya Khamisi Hamad alisema uchaguzi huo umefuata taratibu zote za kisheria za chombo hicho kutunga sheria Visiwani hapa.

Alisema kura 75 zote zilimchagua spika huyo na kura moja kumkataa.

Hamad alisema kutoka kuchaguliwa  kwa zaidi ya 90% ni inshara tosha wajumbe kwamba wana imani na spika huyo.

“Baada ya kuonesha imani hii sasa ni muda wa kumpatia mashirikiano ya kiutendaji ili malengo chombo yaweze kufikiwa “ ,alisema Hamad.

Mara baada ya kula kiapo Spika wa Baraza la wawakilishi Zanzibar Zubeir Ali Maulid  aliwaomba wajumbe wa  chombo hicho kufanyakazi na wananchi wote majimboni bila ya kujali itikadi za Kisiasa.

Alifahamisha kwamba kufanya hivyo kutaisaidia amani iliyopo Zanzibar kuendelea kuwepo  kutokana na wananchi wote kuonekana sawa.

Alisema maendeleo ya nchi hayachagui na kudai kwamba sasa ni wakati wao wajumbe wa chombo hicho kujenga uaminifu kwa wale waliowachagua na hata ambao hawakuwachagua.

“Lazima tufanya kazi zetu bila kumwangalia mtu anatoka chama gani hapo amani yetu itaendelea kusitawi” alisema Spika huyo.

Sambamba na hilo Maulid aliwoamba wajumbe hao kumpatia mashirikiano ya kila hali kila wakati yanapohitajika.

Jina Zubeir Ali Maulid kutokana chama cha mapinduzi (CCM) limepigiwa kura likiwa pekeyake kutokana na vyama vyengine kutowasilisha majina ya kugombea nafasi hiyo na hivyo kupitishwa kwa kura zote.

Mara ya kula kiapo Spika Maulid aliaza kazi yake ya mwanzo kwa kuwalisha kiapo cha utii wajumbe wote wa baraza hilo ambapo wa mwanzo kuaza kuapa alikuwa makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mwakilishi wa Jimbo la Kitope Wilaya ya Kaskzini B Unguja Balozi seif Ali Idd na kuatiwa na wengine 76.

Maulid ataongoza chombo hicho kilichozoeleka kuwa na  sura ya upinzani kikiwa na wajumbe kutoka chama ncha Mapinduzi Pekee kutokana na Chama Kikuu cha Upinzani visiwani hapa kususia uchaguzi wa marejeo uliofanyika machi 20 baada ya ule wa Oktoba 25 mwaka jana kufutwa.

No comments:

Post a Comment

Pages