HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 15, 2016

DK. ABDALLAH POSSI MGENI RASMI SIKU YA WATOTO WENYE USONJI

 Mwenyekiti wa Chama cha Kuhudumia Watu Wenye Usonji Tanzania (NAPAT) Dkt.Stella Rwezaula(wa tatu kulia) akiongea na waandishi wahabari kuhusu matembezi ya hiyari kuadhimisha siku ya usonji Aprilli 16, kushoto ni  Katibu wa Chama cha Kuhudumia Watu Wenye Usonji (NAPAT) Bi. Ella Mgalla na wengine ni wajumbe.(Picha na Lorietha Laurence-Maelezo)

Na Lorietha Laurence-Maelezo

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Dk.Abdalla Possi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika matembezi ya hiyari ya kuazimisha siku ya watoto wenye usonji  Aprili 16 mwaka huu.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Chama cha Kuhudumia Watu Wenye Usonji Tanzania (NAPAT) Dkt.Stella Rwezaula ameeleza kuwa lengo la matembezi hayo ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu watu wenye matatizo ya Usonji.

“Jamii imekuwa ikiwanyima uhuru watu wenye usonji kwa kuwafungia ndani na hivyo kuwanyima haki zao za msingi ikiwemo kupata elimu ” alisema Dkt.Rwezaula.

Aliongeza kuwa watu wenye matatizo ya usonji wanapopatiwa msaada wa haraka na unaostahili ikiwemo huduma ya afya husaidia kuimarisha hali zao na baadaye kuwa msaada katika jamii yake.

“Usonji ni tatizo linalotokana na hitilafu katika ukuuaji wa ubongo wa mtoto na kupelekea mtoto kuwa na matatizo katika mawasiliano  na mahusiano ya kijamii na utambuzi  lakini linapogundulika haraka inasaidia kuimarisha hali ya mtoto“ alisema Dkt.Rwezaula.

Naye  Katibu wa Chama cha Kuhudumia Watu Wenye Usonji (NAPAT) Bi. Ella Mgalla ametoa wito kwa wazazi  kuwasaidia watoto wenye usonji  kwa kuwapeleka  katika shule maalum  ili waweze kupata elimu.

Pia ameeleza kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni ukosefu wa waalimu maluum wa kuwafundisha watoto wenye usonji pamoja na upungufu  wa shule maalum  ambapo mpaka sasa kuna shule 8 Tanzania nzima.

“Ninaiomba serikali iweze kutusaidia kwa kutoa mafunzo maalum kwa waalimu ambao watakuwa wakiwahudumia watoto wenye matatizo ya usonji na kuongeza idadi ya shule  ambapo kwa sasa ni mikoa minne tu inayotoa huduma hiyo ikiwemo Dar es Salaam shule mbili, Arusha shule nne, morogoro shule moja na Mwanza shule moja” alisema Bi.Mgalla.

Chama cha  Kuhudumia Watu Wenye Usonji (NAPAT) kimeanzishwa mwaka 2012 kikiwa kinajumuisha wanachama 53 ambao ni wazazi, walezi na waalimu wa watoto wenye usonji.

No comments:

Post a Comment

Pages