Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala) wameomba ushirikiano kutoka kwa wabunge wenzao wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusaidia kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuhusu fursa za mtangamano (Integration) wa Jumuiya.
Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania katika EALA, Makongoro Nyerere, aliwaambia wabunge wa kamati za Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na ile ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika kikao cha pamoja jana jijini Dar es Salaam kuwa miongoni mwa fursa zitokanazo na mtengamano wa Afrika Mashariki ni pamoja na zile za biashara na masoko.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake tisa wa EAlA, Makongoro alizitaja fursa nyingine kuwa ni za elimu, uwekezaji, ajira na kujiajiri, kwenda popote katika Jumuiya, uhuru wa kuishi popote katika nchi wanachama kwa wale wenye shughuli maalum, kuboreshwa kwa miundombinu, maonesho ya wajasiriamali na maonesho ya utamaduni na fursa zinazotolewa kwa familia (Dependants).
Alisema Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki inajengwa katika mfumo wa ushindani wa soko na kwamba kila fursa iliyopo katika Jumuiya inapatikana kwa ushindani miongoni miongoni mwa wananchi wa nchi wanachama.
"Hivyo, Watanzania kama raia wa nchi zingine wanachama ni lazima wachangamkie fursa na kuzitumia. Ili kushindana, Watanzania wanatakiwa kujiamini na kuacha kujiona wanyonge ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani akili tunazi, uwezo tunao na nguvu tunazo," alifafanua.
Akichangia katika mkutano huo, Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Allan Kiula, alisema ni vema elimu kuhusu mtangamano wa Afrika Mashariki, hususan kuhusiana na fursa za kibiashara, ikatolewa pia kwa wafanyakazi wa taasisi zinazofanya kazi kwenye maeneo ya mipakani, kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara kutokana na utendaji wao usioridhisha.
Alisema watumishi katika vituo vya mipakani wamekuwa wakiwakatisha tamaa wananchi wanaofanya biashara kiasi cha kuwafanya waendelee kutumia njia za panya.
Naye mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema) alisema Tanzania bado ina kazi kubwa katika ushindani ndani ya Jumuiya akitolea mfano wa Kenya ambayo imefikia uchumi wa kati kwa kuwa na viwanda vya kutosha wakati nchi yetu ndio inafikiria kufufua na kuanzisha viwanda.
Alisema kuna hatari ya Tanzania kubakia kuwa soko wakati nchi kama Kenya zinapambana kufanya uzalishaji mkubwa wa viwandani na kuimarisha ubora wa bidhaa zake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajabu aliwataka Watanzania kutafuta mbinu za kuwa wabunifu zaidi katika ushindani ndani ya Jumuiya ili kuweza kufanikiwa kukamata fursa za mtangamano.
Wabunge wa Afrika Mashariki ambao wapo katika shughuli za kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu fursa za mtangamano wa Afrika Mashariki wamesema siku za usoni wanatarajia kufanya mkutano na wabunge wote ili kubadilishana nao uzoefu kuhusiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa Wabunge wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania,
(EALA), Makongoro Nyerere akifafanua jambo wakati wabunge kutoka EALA
walipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ulinzi na Usalama
pamoja na Kamati ya Viwanda Biashara na
Mazingira jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kadumu
ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajabu na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Dk. Dalali Kafumu. (Picha
na Francis Dande)
No comments:
Post a Comment