Mshambuliaji Shiza Ramadhan Kichuya wa timu ya Mtibwa Sugar ya
Morogoro amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Machi kwa Ligi Kuu ya
Vodacom msimu huu wa 2015/2016.
Kichuya alionyesha kiwango cha juu katika mwezi huo uliokuwa na
raundi nne, hivyo kuisaidia timu yake kushinda mechi mbili kati ya tatu
ilizocheza.
Katika mechi hizo ambazo zote Kichuya alicheza, alifanikiwa kufunga
mabao mawili kati ya matano yaliyofungwa na timu yake. Alifunga dhidi ya
Coastal Union kwa ushindi wa mabao 3-0, na JKT Ruvu Stars ambapo Mtibwa
Sugar ilishinda mabao 2-1.
Uwezo aliouonyesha kwa mwezi huo ulisababisha Kocha wa Taifa Stars,
Charles Mkwasa amwite kwa mara ya kwanza kwenye kikosi chake kwa ajili
ya mechi dhidi ya Chad iliyofanyika Machi 23, 2016 jijini N'Djamena.
Washindani wa karibu wa Kichuya walikuwa washambuliaji Mbaraka Yusuf
wa Kagera Sugar, na Abdulrahman Mussa wa JKT Ruvu Stars ambao pia
waling'ara kwa upande wa timu zao kwa mwezi huo.
Kichuya ambaye huu ni msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu, kwa
kunyakua tuzo ya mchezaji bora kwa Machi atazawadiwa kitita cha sh.
1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom.
Wachezaji bora wa miezi mitatu iliyopita ni kiungo
Thaban Kamusoko wa Yanga (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Yanga
(Januari 2016) na mshambuliaji Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons
(Februari 2016).
No comments:
Post a Comment