HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 24, 2016

MICHEZO YA MEI MOSI, Chaptele wa Uchukuzi SC aibuka bingwa mara saba

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MWENDESHA baiskeli Chaptele Muhumba wa Uchukuzi SC, jana alitwaa ubingwa wa saba wa mashindano ya Mei Mosi ya kilometa 35 kwa wanaume yaliyoendelea kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.

Chaptele, ambaye hana mpinzani alianza kutwaa ubingwa katika mashindano yake ya kwanza mwaka 2010 yaliyofanyika Morogoro kitaifa, na baadaye kufululiza kutwa ubingwa ikiwa ni mara mbili zaidi mkoani Morogoro, na mara moja-moja kwenye mikoa ya Mbeya, Tanga na Mwanza.

“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kutwaa ubingwa huu tena, bila yeye hakuna zaid ya Mungu, na pia huu mchezo naupenda na upo damuni na ninafanya mazoezi sana ndio maana sipotezi namba yangu ya kwanza,” alisema Chaptele ambaye mara baada ya kumaliza alivua jezi yake na kubaki na fulana ya ndani aliyoandika ‘NI YESU TU, HAPA KAZI TU,-JPM’.

Lakini, mchezaji huyo aliyemaliza kwa kutumia muda wa 1:27:42 aliwataka waandaaji kuhakikisha wanaongeza askari wa usalama wa barabarani, ili kuzuia madereva wakorofi wanaoingilia msafara wao, ambapo unahatarisha usalama wao.

“Askari wa usalama wawili tu hawatoshi, kama mlivyoona magari makubwa malori yanatupita na mara ghafla yalikuwa yakirudi upande wetu na wengi tuliingia uoga,” alisema Chaptele.

Katibu Mkuu wa Kamati ya mashindano hayo, Award Safari alisema suala lililolalmikiwa na wachezaji wa baiskeli ataliwasilisha kwenye kikao cha viongozi wote wa timu, ambacho hufanyika mara baada ya kumalizika kwa michezo ya siku husika.

Chaptele alifuatiwa na Peter Ngalu wa TPDC aliyetumia muda wa 1:30:43 na Irimin Tarimo wa Tanesco alishika nafasi ya tatu kwa 1:40:51, wakati kwa wanawake bingwa ni Naomi Kimaro wa TPDC katumia muda wa 57:03, huku mshindi wa pili ni Bertha Wilson wa Ujenzi katumia 58:19 na Salome Luvanda wa Tamisemi akiwa wa tatu kwa muda wa 59:26.

Katika soka timu  ya Uchukuzi SC ilipata ushindi wa chee baada ya Mambo ya Ndani kushindwa kutokea uwanjani. Uchukuzi ndio inaongoza kwenye kundi B kwa kuwa na pointi saba, ikifuatiwa na GGM wenye pointi nne.

Nao TPDC waliwashinda UDOM kwa magoli 2-1. Magoli yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Daruwesh Shija katika dakika ya 13 na 54, na bao pekee la UDOM lilipachikwa na Ally Lutavi katika dakika 23.

Kwa upande wa kamba kwa wanawame na wanaume Uchukuzi SC waliweza kuibuka washindi, ambapo wanawake waliwavuta bila huruma Ukaguzi kwa mivuto 2-0, na wanaume waliwachapa Tamisemi kwa mivuto 2-0.

Katika mchezo wa draft wanaume Ally Salehe wa Uchukuzi SC aliibuka mshindi wa pili, baada ya Salum Simba wa Tamisemi kuwa bingwa na Haji Chillo wa UDOM kushika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa draft wanawake mchezaji Stella Limbumba wa Tanesco alitwaa ubingwa, akifuatiwa na Joyce Kimondi wa Ujenzi na Chausiku Hamisi wa CDA akiwa wa tatu.

Michuano hii inaendelea leo kwa upande wa soka timu ya GGM kuumana na Ukaguzi, huku UDOM wakikutana na Tamisemi, nao CDA wakiwakaribisha Mambo ya Ndani; wakati katika netiboli Tanesco itacheza na CDA .
 Thea Samjela wa Uchukuzi SC (kuilia) akichuana na Regina Mutimangi wa TPDC katika mchezo wa bao.
Omar Said wa Uchukuzi SC (kushoto) akicheza bao dhidi Hamisi Rahis wa Tanesco.
Ally Sule wa Uchukuzi SC(kushoto) akicheza mchezo wa fainali dhidi ya Salum Simba wa Tamisemi. Simba aliibuka bingwa.
 Timu ya wanawake ya kamba ya Uchukuzi SC wakiwavuta wenzao wa Ukaguzi kwa mivuto 2-0.
  Timu ya wanaume ya Uchukuzi SC wakiwavuta wenzao wa Tamisemi kwa mivuto 2-0.
   Bingwa wa baiskeli kwa wanawake Naomi Kimaro wa TPDC akimaliza mbio za kilometa 20 zilizoanzia Chigongo na kumalizikia makaburi ya Nkuhungu
 Chaptele Muhuimba wa Uchukuzi SC akimaliza mbio za baiskeli za kilometa 35 kwa kutumia muda wa 1:27:42.

No comments:

Post a Comment

Pages