MKE wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa amewaomba wananchi
wa wilaya ya Ruangwa kuwaombea dua viongozi wa taifa, Rais Dk. John Magufuli,
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili waweze
kufanya kazi zao kikamilifu.
Amesema kazi nzito inayofanywa na viongozi
hao ya kuhakikisha nchi inakuwa salama na inasonga mbele kimaendeleo ni shughuli
ngumu na inahitaji nguvu ya Mungu, hivyo ni vema wananchi wakawaombea dua ili kazi
hiyo iweze kuwa na tija kwao na taifa kwa ujumla.
Mke wa Waziri Mkuu ameyasema hayo jana
alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji
cha Chinongwe wilayani Ruangwa, ambapo amewaomba mwananchi hao wajitahidi
kuwaombea dua viongozi hao ili malengo yao ya kuwaletea maendeleo yatimie.
Mary ambaye ameongozana na Waziri Mkuu
Majaliwa ambaye ni mbunge wa Ruangwa, katika ziara yake ya kuwashukuru wananchi
waliomchagua kwa nafasi ya ubunge na kisha Rais Dk Magufuli kumteua kuwa kushika wadhifa huo.
"Nawashukuru sana wananchi kwa kuwa kura
zenu ndiyo zilizosababisha Mheshimiwa Majaliwa ambaye ni mbunge wetu kuteuliwa
kuwa Waziri Mkuu, hivyo nawaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana,” amesema mke
wa Waziri Mkuu.
Amesema licha ya kuongezewa majukumu atahakikisha
anaendelea kushirikiana na wanaruangwa ili waweze kuendeleza shughuli za
maendeleo katika wilaya hiyo na kwamba wasiwe na wasiwasi kwani hata wasahau kwa
kuwa anawapenda na kuwaheshimu.
No comments:
Post a Comment