TIMU ya Uchukuzi SC imesema haina wachezaji mamluki
watakaowatumia katika mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza Jumatatu (Aprili 18),
kwenye viwanja vya Jamhuri mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa Uchukuzi SC, Mohamed Ally, alisema
jijini hapa kuwa hawawezi kutumia mamluki kwani ni moja ya masharti na kanuni
ya mashindano hayo, kwani hairuhusiwi kutumia wachezaji ambao sio waajiriwa wa
taasisi au wizara zinazoshiriki kwenye mashindano hayo.
“Tumekuwa tukishiri haya mashindano na mengine mengi
yanayoshirikisha taasisi za serikali na moja ya masharti makubwa ni kutotumia wachezaji
wasiokuwa wafanyakazi halisi wanatambulika kama mamluki, hili tulisimamia kwa
kuhakikisha wafanyakazi waajiriwa katika idara mbalimbali ndio wanaocheza
katika mashindano haya” alisema Ally.
Ally alisema wanawachezaji wengi wenye viwango vya
juu, ambao wanauhakika wa kufanya vizuri kwa kuchukua ubingwa katika michezo
mbalimbali baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu.
“Tuliweka kambi kwa takribani miezi miwili huku
tukifanya mazoezi kwenye viwanja vyetu vilivyopo kando kando ya uwanja wa ndege
wa Kimataifa wa Julius Nyerere na baadaye tukacheza mechi za kirafiki na timu
mbalimbali za soka ikiwemo Amadori Boys ya Pugu Sekondari,” alisema Ally.
Naye kocha wa timu ya netiboli ya Uchukuzi SC,
Judith Ilunda alisema hana hofu na wachezaji wake kutokana kufanya mazoezi ya
kutosha kwa kucheza mechi tatu za kitafiki na timu za Uhamiaji na Cargo.
“Tunauhakika wa kutwaa kombe kwa sababu tumefanya
maandalizi kabambe na tuna wachezaji wazoefu, wakiwemo waliowahi kuchezea timu
ya taifa na wengine bado wapo katika timu hiyo ya taifa,” alisema Ilunda
mchezaji wa zamani wa timu machachari ya Bandari na timu ya taifa.
Aliwataja baadhi ya wachezaji hao wazoefu ni pamoja
na Matalena Mhagama, Mwadawa Hamisi, Subira Jumanne, Mary Kajigili na Sharifa
Mustafa.
Meneja na kocha wa timu ya soka ya Uchukuzi SC, Robert
Damiani alisema wapo tayari kwa mashindano kutokana na maandalizi kamambe
waliyoyafanya wakiwa jijini Dar es Salaam.
Kocha wa timu ya riadha wa Uchukuzi SC, Kingsley
Marwilo alisema atakuwa wachezaji watatu wa marathoni, ambao ni Scolastica
Hasiri, Ramadhani Mwakilongo na Leonard Julius.
Timu ya Uchukuzi SC, ambayo inashiriki kwenye
michezo ya soka, netiboli, riadha, baiskeli, kuvuta kamba, karata, bao na
vishale, mwaka jana ilitwaa vikombe 13 kati ya hivyo vitano vilikuwa vya
ubingwa wa kwanza, na vilivyosalia vilikuwa vya ushindi wa pili na tatu.
Wachezaji wa timu ya netiboli ya Uchukuzi SC wakifanya mazoezi ya viungo kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Wachezaji wa timu ya netiboli ya Uchukuzi SC wakisikiliza maelekezo ya kocha Judith Ilunda (mwenye fulana nyeupe)
Mchezaji Subira Jumanne wa
Uchukuzi SC akiwahi mpira.
No comments:
Post a Comment