Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya netiboli ya Uchukuzi SC jana ilianza vyema mchezo
wake wa kwanza kwa kuwaicharaza CDA ya Dodoma katika mashindano ya Mei Mosi
yanayoendelea mkoani Dodoma.
Uchukuzi SC inayoundwa na wachezaji wakongwe, akiwemo
mfungaji mahiri wa timu ya Bandari na Taifa, Matalena Mhagama waliwapeleka puta
wapinzani wao ambapo hadi mapumziko walikuwa mbele kwa magoli 11-6.
Katika mchezo huo uliokuwa umetawaliwa na rafu za hapa na
pale na kulalamikiwa mara kwa mara na wachezaji wa Uchukuzi SC, ulimalizika kwa
mfungaji Matalena kufunga magoli 16 na Tatu Kitula akifunga saba, wakati
wapinzani wao Tatu Fungo nma Margeth Nicholaus kila mmoja akifunga magoli nane.
Kocha Mkuu wa Uchukuzi SC, Judith Ilunda alisema wamepata
ushindi huo wa kwanza kutokana na kufanya mazoezi ya pamoja ya muda mrefu,
pamoja na kwamba wapinzani wao walikuwa ni wazuri na wenye uzoefu mkubwa.
“Wengi waliocheza na kikosi change ni wakongwe wapo
niliocheza nao mimi kwenye mashindano mbalimbali, hivyo wameweza kutumia
ukongwe wao lakini tuliwazidi mbinu kutokana na timu yetu kuundwa na chipukizi
wengi,” alisema Ilunda.
Lakini, alilalamikia maamuzi ya waamuzi waliocheza mchezo
huo kuwa mengi yamepitwa na wakati kutokana na sheria kubadilika mara kwa mara.
“Hawa waamuzi wamekuwa wakichezeshakwa sheria nyingi za
zamani na kusababisha mvutano, hivyo wanatakiwa wabadilike kwa kujisomea mara
kwa mara ili kuondoa mkanganyiko kwa timu zinazocheza,” alisema Ilunda.
Hatahivyo, waamuzi Mariam Makisi na Caroline Paulo wote wa
Dodoma, kwa nyakati tofauti walisema wamechezesha mchezo huo kwa kanuni na
sheria za mchezo huo, lakini wameshangazwa na malalamiko ya kuwa wamechezesha
kwa sheria za zamani.
“Unajua timu za Dar es Salaam siku zote zinajifanya kujua
sheria zaidi, na wangeweka wazi ni wapi waamuzi tulipopindisha sheria,” alisema
Makisi.
Wakatihuohuo, timu ya Tamisemi iliwafunga TPDC kwa magoli
6-1 katika mchezo wa soka uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri.
Wafungaji wa Tamisemi ni Mwigane Yeya kafunga magoli mawili,
wakati waliofunga moja-moja ni Hamis Shedafa, Hamad Majura, Nelson Richard na
Phillipo Oden; wakati bao la kufutia machozi la TPDC lilifungwa na Shija
Dalushi.
Katika mchezo mwingine wa soka, timu ya Tanesco ilipata
ushindi wa chee baada ya wapinzani wa CWT ya Dodoma kushindw kutokea uwanjani.
Mfungaji wa CDA Dodoma, Tatu Fungo akiuwahi mpira
katika mchezo wao wa netiboli wa Kombe la Mei dhidi ya Uchukuzi SC. Uchukuzi
walishinda kwa magoli 23-16.
Mchezaji Mwadawa Hamisi wa
Uchukuzi SC (GK) akiangalia mwenzake wa kumrushia baada ya Tatu Fungo wa
CDA kufunga bao katika michuano ya Mei Mosi. Uchukuzi walishinda magoli
23-16.
No comments:
Post a Comment