HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 14, 2016

WAGONJWA WA KIPINDUPINDU WAONGEZEKA ZANZIBAR

Na Talib Ussi, Zanzibar

Wakati Zanzibar inazidi kukumbwa na ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu dawa za kutibu maradhi hayo zinadaiwa kupungua kwa kiasi kikubwa katika Hospital na makambi ya wagonjwa hao  visiwani hapa.

Habari zimebaini kuwepo kwa wagonjwa wengi wanaopelekwa hospitalini huku madaktari wakiwa na upungufu mkubwa wa madawa ya kutibu maradhi hayo.

Kutokana na hali hiyo Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzaia alifanya ziara maalumu visiwani hapa kwa kuzungumza na watendaji wa Wizara ya Afya pamoja na wanahabari hapo katika Jengo la wizara ya Afya juu ya hali hiyo kupanda kwa kasi maradhi hayo na kuzitembelea kambi wagonjwa wa kipindu pindu.

Mkurugenzi Kinga na ELimu ya Afya Zanzibar,  Dk. Mohamed Dahoma alisema kwa sasa hali inazidi kuwa mbaya kwani jana  walipokea wagonjwa 20 tofauti na siku za nyuma ambapo walikuwa wanapokea  wagonjwa kati ya  10 hadi 15 kwa siku katika kambi mbali mbali ikiwemo ya Chumbuni.

Alieleza kuwa  jumla ya Kambi 17 za wagonjwa wa kipindupindu zimefunguliwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Dk. Dahoma amesema kisiwa cha Unguja kimekuwa na wagonjwa wengi  zaidi wa kipindupindu  asilimia 52.3 na Pemba ni asilimia 47.3 huku Mkoa Mjini Magharibi ukiongoza ukifuatiwa na Mkoa Kaskazini Pemba.

“Hali hii ni mbaya sana kwani  wagonjwa 2703 waliogunduliwa na maradhi haya tayari  34 wamefariki ikiwa ni  sawa na asilimia 1.3 na vijana wenye umri kuanzia miaka 17 ndio walioathirika zaidi” alieleza Dk. Dahoma.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzaia Dkt. Rufaro Chatora amezishauri taasisi za Serikali, taasisi za kiraia na watu  binafsi kila mmoja kutekeleza wajibu wake katika kukabiliana na maradhi ya kipindupindu nchini.

“Maradhi  ya kipindupindu yanapotokea katika nchi moja yanagusa nchi nyingi duniani kutokana na watu kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyengine katika harakati zao za maisha kwa maana hio lazima tuwe waangalifu” alisema Chatora.

Dkt. Chatora ameeleza hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano na watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na waandishi wa Habari katika ziara yake ya kuangalia hali ya maradhi ya kipindupindu Zanzibar tokea yalipoanza mwezi Septemba mwaka jana hadi hivi sasa ambapo  watu 2703 wamepata ugonjwa  huo kudai hii hali hiyo inatia ghofu.

Ugonjwa huu ni rahisi kutibika iwapo kila mtu atatimiza wajibu wake na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuacha  kutumia vitu visivyo salama ambayo ni moja ya chanzo kikubwa cha kupata maradhi hayo.

No comments:

Post a Comment

Pages