· TFF yasaini mkataba wa miaka mi5 na Azam Media Ltd
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), leo limesaini
mikataba miwili na Kampuni ya Azam Media Ltd, ya Haki za Matangazo ya
Televisheni ya michuano ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL) na Ligi ya
Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 (U-20 National League).
Mikataba hiyo iliyosainiwa kwa mpigo, ina thamani ya Sh.
Bil. 2, kwa kipindi cha miaka mitano, ambayo ilitiwa saini jana Makao Makuu ya
Azam Media Ltd na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam
Media, Rhys Torrington.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusainiwa kwa mikataba
hiyo, Malinzi alisema TFF inapenda kuishukuru Azam Media kwa kuendelea kuunga
mkono jitihada za shirikisho lake kunyanyua maendeleo ya soka Tanzania, kwa
kuitikia maombi yao na kukubali kutoa udhamini.
Malinzi aliyataka makampuni mbalimbali nchini hasa
yanayotoa huduma za kijamii zinazohusisha wanawake na watoto, kujitokeza
kudhamini michuano hiyo, ambayo hadi sasa inapotarajiwa kuanza kuchezwa,
haijapata Mdhamini Mkuu wa Mashindano.
Alibainisha kuwa, kutokana na Azam Media Ltd kuingia
mkataba wa Haki za Matangazo kwa kipindi cha miaka mitano kuonyesha ligi hizo,
kampuni na taasisi zingine zijitokeze na kuitumia fursa hiyo kama chachu ya
kujitangaza kupitia udhamini wa michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment