*Asifu amani iliyopo
nchini, upendo wa Watanzania
*Asema mahujaji wa Tanzania
hawana rekodi za uovu
WAZIRI wa Mambo ya Dini wa Saudi Arabia, Dk. Saleh Ali Sheikh amesema
Tanzania ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine kutokana na amani iliyopo.
Ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumapili, Mei 27, 2018) wakati
akitoa nasaha kwa wageni walioshiriki futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.
“Ninaomba nipelekewe shukrani zangu kwa
umma wa Watanzania kutokana na upendo walionao. Ukiwaona ni watu wa amani,
furaha na upendo na hili linathibitishwa na amani iliyopo nchini mwenu,”
alisema.
Alisema uwepo wa amani na upendo
miongoni mwa wananchi ni kielelezo tosha cha kazi kubwa inayofanywa na viongozi
wa dini ambao ndiyo wanawalea Watanzania. “Kilichofanyika leo ni daraja kati ya
Tanzania na Saudi Arabia, ni asubuhi njema ambayo pia ni dalili kwamba kuna
mchana mwema unakuja,” alisema.
Alimshukuru Waziri Mkuu kwa ukaribisho
aliopewa kushiriki futari nyumbani kwake na kuongeza kuwa hicho ni kitendo cha
udugu na utu na kitazidi kujenga mahusiano baina ya nchi hizo mbili.
Alisema
tabia hizo njema ni urithi kutoka kwa maulamaa waliotumwa na Mungu ambao kazi
yao kubwa ilikuwa ni kuwatengeneza watu wawe na tabia njema na siyo
kuwafundisha junsi ya kurusha ndege.
“Matendo haya yanaonekana wazi kwa
Watanzania kwani hata wakati wa hijja kuna nchi nyingi zinakuja kule kwetu,
lakini haijawahi kuripotiwa kuwa hujaji wa Tanzania ameingia katika utovu wa
adabu,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa alimshukuru Waziri huyo na ujumbe wake kwa kuitembelea Tanzania na
kushiriki kwenye mashindano ya 19 ya kuhifadhi Quran Afrika.
Waziri Mkuu alisema amefarijika na
uamuzi wa Waziri huto wa Saudi Arabia na ujumbe wake wa watu 16 kuamua kuongeza
siku zaidi za ziara yao hapa nchini hadi Jumatano (Mei 30, 2018) badala ya
kuondoka Jumatatu (Mei 28, 2018) ili waweze kutembelea vituo vya watoto yatima
na kuona maeneo mengine jijini Dar es Salaam.
“Tumefarijika na ahadi uliyoitoa pale
uwanjani kwamba mwaka kesho utahakikisha kwamba Sheikh Mkuu wa Msikiti wa Makkah,
Sheikh Abdul Rahman Abd al Aziz al Sudais anakuja nchini kuhudhuria mashindano
ya 20 ya kuhifadhi Quran tukufu,” alisema.
Viongozi wengine
waliohudhuria futani hiyo ni Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally
na Rais wa taasisi ya Al-Hikma, Sheikh Sharif Abdilkadir Al-Ahdal, na Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mstahiki
Meya wa Kinondoni wa Meya wa Temeke.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
MEI 28, 2018.
No comments:
Post a Comment