HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 27, 2016

SMZ YAVIAGIZA VYOMBO VYA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA KUFANYA KAZI KWA UADILIFU

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeviagiza vyombo vyote vinavyosimamia udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya kufanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa ili kurahisisha utekelezaji wa mipango ya udhibiti wa janga hilo linaloonekana kuwa sugu hapa Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea kwenye Majengo yake yaliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema dawa za kulevya bado ni tatizo sugu duniani kote ikiwemo Zanzibar linaloendelea kuiathiri sana jamii hasa kundi kubwa la Vijana ambalo ndio nguvu kazi kubwa inayotegemewa na Taifa.

Alisema  katika kupambana na changamoto hiyo ya dawa za kulevya Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ndani na nje ya Nchi inajitahidi kupambana na janga hilo kwa kuchukuwa hatua za  kuondoa usafirishaji na usambazaji, matumizi na athari zinazotokana na matumizi ya dawa hizo.

“ Jumla ya wanafunzi 1,620 Nchini tayari wamepatiwa taaluma juu ya athari za dawa za kulevya zikiwemo ziara za mafunzo kama hayo kwa shehia 16 za Unguja na Pemba kupitia program inayosimamiwa na Tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa Dawa za kulevya “. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na udhibiti wa Dawa za kulevya imeandaa muongozo wa kuwazawadia watoa Taarifa kuhusu uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya ambapo muongozo huo unasubiri vikao vya Tume kwa ajili ya kupatiwa mapendekezo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili Vijana ikiwemo dawa za kulevya na ukosefu wa ajira Serikali kupitia mfuko wa uwezeshaji Wananchi kiuchumi imeshatoa mikopo mia 307 yenye thamani ya shilingi Milioni Mia 467,278,000/- ili isaidie shughuli za uzalishaji.

Alisema mikopo hiyo inayolengwa kwa wananchi wenye kipato kidogo itawajenga uwezo wananchi na hasa Vijana ili waweze kujiajiri na kuajirika ikieelekezwa zaidi katika shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na kazi za mikono kwa ajili ya kujiajiri na kupunguza umaskini.

Balozi Seif alieleza kuwa vituo viwili vya mafunzo ya amali Makunduchi kwa Unguja na Daya Kisiwani  Pemba vinaendelea kujengwa  sambamba na upanuzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia, Chuo cha Maendeleo ya Utalii na kituo cha elimu Mbadala Wingwi Mtemani ili kuwajnga vijana kitaalum na kiujuzi utakaowawezesha kuingia katika soko la ajira kwa uhakika.

Akizungumzia suala la Mazingira Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema utunzaji wa mazingira ni suala la lazima na ni muhimu kulitekeleza ili kuleta maendeleo endelevu na kupunguza umaskini.

Balozi Seif alisema Mataifa na taasisi mbali mbali ulimwenguni zimekuwa zikitoa kipaumbele katika suala la kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi ili kupunguza athari zinazotokana na hali hiyo.

Alisema  kwa kutambua umuhimu huo Serikali imekuwa ikihimiza Wananchi kutunza maeneo ya misitu na kuotesha miti kwa wingi maeneo ya wazi ikiwemo fukwe za bahari pamoja na kuachana na tabia ya kukata miti ovyo na uchimbaji wa rasilmali zisizorejesheka.

 Kuhusu hali ya kisiasa iliyopo hivi sasa Nchini Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kusimamia amani ya Taifa hili.

Alisema hali ya uvunjifu wa amani visiwani ilionekana kuchezewa na baadhi ya watu kwa kuchoma moto mali za Serikali na za Wananchi wenzao vikiwemo vituo vya afya, mashamba ya mikarafuuj na nyumba za makaazi hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa Zanzibar.

Alisema uvunjifu huo pia ulikwenda sambamba na kujitokeza kwa baadhi ya  wananchi kususiana na kubaguana kutokana na tofauti za kisiasa katika shughuli mbali mbali za kijamii na kiuchumi.

Hata hivyo Balozi Seif  alisisitiza kwamba Serikali itaendelea kuchukuwa hatua madhubuti za kuhakikisha hali ya umoja, amani na utulivu inaendelea kuwepo katika maeneo yote nchini.

Balozi Seif aliwaomba Wananchi waendelee kushirikiana katika shughuli zao za kijamii pamoja na kutoa ushirikiano kwa viongozi wa ngazi zote za Serikali katika kuidumisha hali ya Umoja.

Alieleza kwamba kudumishwa kwa mazingira hayo ya ushirikiano yatatoa nafasi ya kudumu kwa ongezeko la mapato yaliyotokana na kukuwa kwa uchumi wa Zanzibar na kufikia asilimia 6.6% mwaka 2015 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 4.0% kwa nchi nyengine zinazoendelea na asilimia 3.4%  kwa nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara.

Hata hivyo alisema kasi hiyo inaashiria kupunguwa kidogo ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0.mwaka 2014, wakati pato halisi la Taifa kwa mwaka 2015 limeonekana kuongezeka na kufikia thamani ya shilingi 2,308.0 Bilioni  ikilinganishwa na thamani ya shilingi 2,133.5 Bilioni mwaka 2014.

Balozi Seif aliwashukuru washirika wa maendeleo na Nchi rafiki ambazo zinaendelea kuchangia katika kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika mwaka wa fedha wa 2015/2016.

Pia alizipongeza taasisi zisizo za kiserikali, jumuiya ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma za kijamii na kuleta maendeleo katika Taifa hili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameliomba Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuidhinisha jumla ya shilingi Bilioni Thalathini na Tano,mia Tisa na Tisini na Mbili Milioni, na sabini na sita elfu { 35,992,076,000/- } kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Taasisi zake kwa ajili ya kutekeleza program zilizoainishwa katika bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2016/2017.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
27/5/2016.

No comments:

Post a Comment

Pages