HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 05, 2016

TCRA yatoa mafunzo ya matumizi ya huduma za mitandao kwa Wizara ya Habari

Na Jacquiline Mrisho MAELEZO

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa mafunzo ya matumizi ya huduma za mawasiliano kwa watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kupata muongozo utakaowasaidia kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Akifungua mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika leo Jijini Dar es salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Nuru Mllao amewataka watumishi wa wizara hiyo kuzingatia mafunzo hayo ili kuepuka matatizo ya mitandao ya kijamii wakati wakuteleza majukumu yao.

"Tumegundua kwamba watumishi wanahitaji muongozo juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, hivyo tunashkuru sana uongozi wa TCRA kukubali kutoa mafunzo kwa watumishi wetu"alisema Bi.Nuru.

Aidha Bi Nuru ametoa rai kwa TCRA kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wa wizara nyingine kwa kuwa watumishi wote wanatakiwa kupata miongozo juu ya matumizi sahihi na usalama wa huduma hizo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi James Kilaba, alisema kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yameongezeka hivyo kuchangia kuongezeka kwa changamoto za matumizi mabaya ya mitandao hiyo.

Kwa upande wa huduma za mawasiliano ya simu, Mhandisi Kilaba alisema kuwa mawasiliano ya simu yanakua kwa kasi nchini hali ambayo inaongeza matumizi mabaya ya mawasiliano ya simu.

"Idadi ya laini za simu kwa miaka 12 iliyopita ilikuwa ni milioni 2.3 lakini hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu idadi ya laini ni takribani milioni 40, wananchi ni wengi wanaotumia huduma za mitandao na wengi wao wanaitumia vibaya”alisema Muhandisi Kilaba.

Mhandisi Kilaba alielezea kuwa mafunzo hayo yataegemea kwenye nyanja za kukua kwa sekta ya mawasiliano na changamoto zake pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia katika matumizi ya mitandao ya kijamii.

Alisisitiza kuwa kupitia mafunzo hayo watumishi wataweza kujua matumizi sahihi ya mitandao hasa katika shughuli zao za kiofisi.

Katika kuzingatia usalama wa mawasiliano yao, TCRA imewashauri watumishi pamoja na wananchi kwa ujumla kutotumia nywila (password) moja kujiunga kwenye mtandao zaidi ya mmoja.
Aliwataka kutoweka nywila ambazo zinahusisha mambo binafsi ambayo yanajulikana kwa watu wengi ili kuzuia mtu mwingine asipate urahisi wa kubuni kuingia katika mtandao wa mtu mwingine.

No comments:

Post a Comment

Pages