*Asema wataendeleza elimu kwa mtoto wa kike
WAZIRI MKUU wa Norway, Bibi Erna Solberg amesema nchi yake iko tayari kuisaidia Tanzania katika suala la kuendeleza elimu kwa mtoto wa kike.
Bibi Solberg ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Mei 12, 2016) alipokutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kufanya naye mazungumzo ya ana kwa ana kwenye mkutano wa siku moja wa Wakuu wa Nchi ulioitishwa kujadili suala la kupambana na rushwa duniani.
Akizungumza na Waziri Mkuu kwenye ukumbi wa Lancaster House, jijini London, Uingereza, Bibi Solberg alisema: “Malengo yetu kwa Tanzania ni kuendeleza elimu kwa mtoto wa kike,” na kuongeza kuwa mbali ya kuwa ni mdau wa maendeleo kwa miaka mingi, asilimia kubwa ya fedha za bajeti zinazotolewa na nchi hiyo kwa ajili ya misaada ya maendeleo zinaelekezwa Tanzania.
“Sasa hivi kuna Serikali mpya iliyoingia madarakani. Tengenezeni ajenda zenu na mzilete ili tuone ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mkutano wa kupambana na rushwa, Bibi Solberg alisema ameufurahia mkutano huo sababu umetoa fursa kwa watu kulizungumzia kwa uwazi tatizo la rushwa. “Watu waliouwa hawalizungumzii suala hilo, hivi sasa wameanza kulijadili na kupanga mbinu ya kukabiliana na janga hilo kubwa,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa aliishukuru Serikali ya Norway kwa misaada ambayo imekuwa ikiipatia Tanzania kwa kipindi kirefu.
Waziri Mkuu Majaliwa alimhakikishia Waziri Mkuu wa Norway kwamba fedha zote za misaada zinazotolewa kwa Serikali ya Tanzania ziko salama na zitatumika kwa uwazi na kwa malengo yaliyopangwa.
“Malengo ya Serikali ya sasa ni kuleta maendeleo ya kiuchumi lakini pia nchini mwetu kuna amani na usalama kwa sababu kama hakuna amani ina maana hakuna usalama,” alisema Waziri Mkuu.
Alimhakikishia Bibi Solberg kuwa Tanzania ni salama na wala hawana haja ya kutilia shaka juu ya uwepo wa amani. Pia alimtaka awahimize wawekezaji kutoka kwao waje kuwekeza kwenye uchakataji wa gesi ya kimiminika (LNG) kwa sababu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Katika mkutano huu, Waziri Mkuu amefuatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Valentino Mlowola, wataalamu wa sekta ya rushwa na wanasheria.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, MEI 13, 2016.
No comments:
Post a Comment