Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda umeanza matayarisho ya kutengeneza mfano wa uzalishaji wa Sukari (Sample) baada ya kukamilisha kwa matengenezo makubwa ya Kiwanda hicho yaliyokwenda sambamba na ufungaji wa mashine zitakazozalisha sukari katika kiwango kikubwa zaidi.
Meneja wa Kiwanda hicho Bwana Vicky Patel alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar akiuongoza ujumbe wa Viongozi Watatu wa Kiwanda hicho walipofika kumuonyesha mfano wa uzalishaji huo.
Bwana Vicky Patel alisema kwamba uzalishaji wa Sukari katika kiwanda hicho unatazamiwa kuanza rasmi MWEZI Julai mwaka huu katika kiwango cha ujazo wa kilo moja, Tano na 50 wakilenga kuanzia kulitumia soko la ndani ya Tanzania.
Alieleza kwamba Uongozi wa Kiwanda hicho tayari umeshajipanga pia kununua miwa kwa wazalishaji wadogo wadogo waliopatiwa mkopo wa fedha na Uongozi huo katika hatua ya awali ya matayarisho ya kuanzisha mashamba yao.
Meneja wa Kiwanda cha Sukari Mahonda alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Sukari itakayozalishwa na kiwanda hicho imepewa jina la Kisiwa linalofaana na mazingira halisi ya Zanzibar kuzungukwa na maji sehemu zote.
Akiangalia sampuli hiyo ya Sukari ya Kiwanda cha Sukari Mahonda Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alielezea hafaja yake kutokana na hatua ya maandalizi ya uzalishaji iliyofikiwa na Uongozi wa Kiwanda hicho.
Balozi Seif alisema uzalishaji wa Sukari ndani ya Visiwa vya Zanzibar unaweza kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa sukari unaotokea baadhi ya wakati na kuwasumbua Wananchi walio wengi ndani ya eneo la Tanzania.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/6/2016.
No comments:
Post a Comment