HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 01, 2016

Mfuko wa sheria yatoa ruzuku bilioni 18 kwa mafunzo ya wasaidizi wa sheria

Na Mwandishi Wetu

MFUKO wa msaada wa kisheria (LSF) umetoa ruzuku kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 18 kwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha utoaji wa msaada wa kisheria kwa ajili ya  mafunzo kwa wasaidizi wa sheria 4,000 nchi nzima.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Afisa Mtendaji, Bi Scholastica Jullu amesema kwamba ruzuku imetolewa kuanzia 2012 kwa mashirika hayo ili kuweza kutoa mafunzo kwa wasaidizi wa sheria katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi hasa wa vijijini.

“Dhumuni la uanzishwaji wa mfuko huu ni kulinda haki za binadamu kupitia ujengaji uwezo wa kisheria na kuongeza upatikanaji wa huduma za kisheria kwa watu masikini na wanajamii wengine walio katika hatari ya kukosa haki zao hususani wanawake nchini,” aliongeza Bi Jullu.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, LSF imechangia katika kukuza na kulinda haki za binadamu huku ikiweka msisitizo katika ulinzi w haki za wanawake na makundi maalum.

Amesema kwamba kutokana na mafunzo waliopata wasaidizi wa kisheria nchini imewezesha upatikanaji wa huduma za usaidizi wa sharia kwa watanzania takribani milioni thelathini na tano (35 milioni).

Alifafanua kwamba katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013 mpaka mwaka 2015 takribani watu 90,000 walipata huduma za msaada wa kisheria na watu 300,000 walifikiwa na elimu ya sheria nchini nzima.

Mambo ambayo wasaidizi wengi wa sheria wanayokutana nayo ni matatizo ya ardhi, ndoa, mirathi, watoto na jinsi ambao asilimia 80 yalishughulikiwa na asilimia 9 tu yalipelekwa kwenye vyombo vingine vya utoaji haki kama vile mahakama, mabaraza ya usuluhishi, serikali za mitaa na polisi.

Bi Jullu alisisitiza mchakato umeanza kwa wadau wa sheria, mashirika yasiyo ya kiserikali na serikali ili kuja na sheria itakayowatambua wasaidizi wa kisheria kwenye mifumo ya serikali.

Kwa upande wake, msaidizi wa kisheria kutoka wilaya ya ilala, Bi Beatrice Bange amesema kwamba changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa watanzania wengi kuhusu huduma za wasaidizi wa kisheria na msaada wa kisheria.

Aliongeza kwamba matatizo mengi anayokutana nayo katika wilaya ya ilala ni ndoa, mirathi na matatizo ya ajira kwa wafanyakazi wa kada ya chini.

Utafiti uliofanywa na shirika hilo mwaka jana ulionyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watanzania hawana uelewa kuhusu msaada wa kisheria na uwepo wa wasaidizi wa sheria.

No comments:

Post a Comment

Pages