WARATIBU wa Mbio
za Watoto za Azania Bank Kids Run 2016, wamemtangaza Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, kuwa mgeni rasmi wa mbio hizo
zitakazofanyika Jumapili Juni 5 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam leo, Mratibu wa Azania Bank Kids Run 2016, zinazodhaminiwa
na Benki ya Azania, Wilhelm Gidabuday, amesema kuwa Naibu Waziri Wambura
atakuwa mgeni rasmi katika kinyang'anyiro hicho kitakachokuwa na kategori tano.
Gidabuday amebainisha
kuwa, maandailizi yote ya Azania Bank Kids Run 2016 yanaenda vema, ikiwamo
idadi kubwa ya wazazi na walezi kujitokeza kusajili watoto wao, huku akiwataka
wengi kutumia siku mbili zilizobaki kuhakikisha wanawapa vijana wao nafasi.
"Mbio hizi
zinazotarajia kushirikisha zaidi ya watoto 2,000, zinatarajia kufanyika
Jumapili Juni 5, 2016 kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, zikihusisha watoto chini
ya miaka 16, ambako Naibu Waziri Wambura atakuwa mgeni rasmi," amesema
Gidabuday.
Amewasisitiza
wazazi, walezi na wadau kujitokeza kusajili watoto wao na kwamba fomu bado
zinapatikana katika matawi yote ya Benki ya Azania, Ofisi za Baraza la Michezo
la Taifa (BMT) zilizoko Samora Avenue na Ofisi za Shirikisho la Riadha Tanzania
(RT).
Gidabuday
ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia wazazi na walezi wa watoto watakaoshiriki
Azania Bank Kids Run 2016 kuwa, usalama wa watoto wao wakati wa shindano
utakuwa kipaumbele chao na kuwatoa hofu ya uslama wakati wa kukimbia.
"Barabara
zote zitakazotumiwa na watoto kukimbilia zitakuwa na uangalizi maalum ikiwa ni
pamoja na gari za huduma ya kwanza na matibabu kwa watakaohitaji kupatiwa
huduma hizo," amesema Gidabuday katika mkutano na wanahabari Dar es
Salaam.
Kwa upande wake,
Ofisa Masoko Mwandamizi wa Azania Bank, Othman Jibrea, amezitaja zawadi za
washindi mbalimbali wa mbio hizo, huku akiweka msisitizo kwa kutawaka wazazi
kuendelea kusajili watoto wao kuwa sehemu ya tukio hilo la kihistoria.
"Mshindi wa
kwanza mbio za Kilomita 5 ni Sh. 200,000, mshindi wa
pili Sh.
150,000 na mshindi wa tatu sh. 100,000, pamoja na medali, begi lenye vifaa vya shule na sare za michezo, wakati mshindi wa nne
hadi wa 10 watapata kifuta jasho cha sh. 15,000," amesema.
Katika mbio za
kilomita 2, Jibrea ametaja zawadi kuwa ni sh. 100,000 kwa mshindi, huku
atakayeshika nafasi ya pili akitarajiwa kulamba sh. 75,000 na wa tatu
kujitwalia sh. 50,000, kategori ambayo pia washindi wa nne hadi wa 10 watapata
kifuta jasho cha sh. 15,000.
Aidha,
amebanisha kuwa, kategori ya mbio za kilomita moja mshindi atatwaa sh. 75,000,
huku wa pili akibeba sh. 50,000 na wa tatu akijishindia sh. 40,000, ambako pia
washindi wa nne hadi wa 10 watapata kifuta jasho kama kilivyotajwa hapo juu.
Pia kutakuwa na
mbio za mita 50 na 100, ambazo zitakimbiwa na watoto chini ya miaka mitatu,
ambako washindi washindi wote watafunguliwa akaunti katika Benki ya Azania,
itakayokuwa na kianzio cha sh.15,000, sanjari na begi la shule lenye vifaa
vyote muhimu.
No comments:
Post a Comment