Na Talib Ussi, Zanzibar
KAIMU Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa
za Kulevya Zanzibar, Dk. Mahmoud Ibrahim Mussa, amesema matumizi ya dawa hizo ni
janga linaloathiri vijana na kupoteza mwelekeo ambao husababisha kufanya uamuzi
usio sahihi na kuzitaka taasisi husika na wazee kushirikiana kuondoa tatizo hilo.
Mussa aliyasema hayo katika shamrashamra za mafunzo
ya watendaji wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya
kuadhimisha Siku ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Duniani.
“Mtumiaji wa dawa za kulevya huathirika ubongo, hivyo
hawezi kuacha kutumia dawa hizo ili kuongeza kiwango, hali inayosababisha kutoweza
kufanya kazi yoyote yenye kuleta manufaa kwake wala kwa taifa,” alieleza Dk.
Mussa.
Alisema kuwa matumizi ya dawa hizo yanakuwa ni chanzo kikuu cha
maambukizi makubwa ya virusi vya ukimwi, hasa kwa watumiaji wa njia ya
kujidunga sindano, hivyo kusababisha jamii kupoteza nguvu ya taifa.
Dk. Mahamoud alitanabaisha kuwa kinga ya msingi ya kuachana na matumizi
ya dawa za kulevya imo ndani ya familia ambayo inatakiwa kumkubali muathirika
ili aweze kuachana na kilevi hicho, kwa kumpa huduma nzuri bila ya kumnyanyapaa.
Aidha, ameshauri kutafuta njia ya kudhibiti utumiaji wa dawa za
kulevya katika vyuo vya mafunzo kwa wafungwa, kwani imebainika kuwa baadhi yao
hutumia dawa hizo wakati wakitumikia vifungo vyao.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameiomba jamii kutoa ushirikiano
mkubwa kwa vyombo vya kudhibiti dawa za kulevya ili kuweza kuwafichua na
kuwadhibiti wale wote wanaoingiza, wanaosambaza, watumiaji, pamoja na kutoa
elimu hiyo kupitia skuli mbalimbali ili kuhakikisha jambo hilo linadhibitiwa
nchini.
No comments:
Post a Comment