HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 22, 2016

GEPF yawakumbuka bodaboda

NA KENNETH NGELESI, MBEYA

KATIKA mkakati wa kuboresha maisha kwa madereva wa pikipiki (bodaboda) nchini, Mfuko wa Mafao ya Kustaafu (GEPF), umeanzisha mpango wa kuiwezesha jamii hiyo kuishi maisha bora na yenye malengo endelevu.

 
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za mfuko huo Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano, Aloyce Ntukamazina, alisema kuwa mpango wa kuwawezesha madereva wa pikipiki uliopewa jina la ‘Bodaboda Scheme’ unatarajiwa kuzinduliwa Juni 23, mwaka huu katika mkutano wa wadau wa mfuko huo utakaofanyika kila mwaka na mwaka huu utafanyika jijini Mbeya.
 
Ntukamazina alisema mfuko umekuja na mpango huo mpya baada ya mafao mapya manne yaliyozinduliwa mwaka jana; Fao la Uzazi, Mkopo wa Elimu, Mkopo wa Kuanza Maisha na Mkopo wa Kujikimu iliyowalenga zaidi vijana wanaoanza kazi kuonyesha mafanikio makubwa.
 
Alisema ili kuendelea kuwezesha jamii ya vijana ambayo kimsingi ndiyo nguvu kazi ya taifa, mfuko umeona haja ya kutanua wigo wa fursa kwa kada hiyo ambapo sasa kupitia Juma la GEPF wameamua kuutambulisha rasmi mfuko wa mafao wa Bodaboda Scheme.
 
Alisema kupitia mafao hayo madereva wa bodaboda wataweza kunufaika kupitia kujiwekea akiba na pia fursa ya kupata mkopo muda mfupi tu baada ya kuwa mwanachama wa GEPF.
 
“Baada ya kuanzisha mifuko kadhaa huko nyuma, sasa tumekuja kivingine kabisa, tumewalenga wajasiriamali ambao hawapo katika mfumo rasmi wa ajira, ambao takwimu zinaonyesha ndiyo nguvukazi kubwa ya taifa. 

Kwanza tumeangalia kundi la sekta ya usafirishaji na hapa tunawalenga zaidi madereva wa bodaboda, Bajaj na madereva wa daladala,” alisema Ntukamazina.
 
Alisema kupitia Bodaboda Scheme pia madereva wa bodaboda wataweza kujiwekea akiba itakayowapa fursa ya kupata mafao yao kama ilivyo kwa wastaafu wa ajira zilizo rasmi, hatua itakayowapa wakati mzuri baada ya kustaafu kazi yao.
 
Aidha, Ntukamazina pia alisema GEPF ina mkakati wa kuwawezesha madereva hao kujiunga katika Fao la Afya ili kuwawezesha kupata matibabu pale wanapopatwa na matatizo ya kiafya, ikiwamo majeraha ya ajali sambamba na familia zao.

No comments:

Post a Comment

Pages