MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA), Hafsa
Mossi aliyeuawa leo kwa kupigwa
risasi majira ya saa nne asubuhi Maeneo ya Mutanga kwenye mji Mkuu wa
Burundi, Bujumbura.
Na Mwandishi Wetu, ARUSHA
MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA) wa Burundi, Hafsa
Mossi, ameuawa kwa kupigwa risasi kifuani na watu wasiofahamika maeneo ya
Mutanga karibu na nyumbani kwake kwenye mji mkuu wa Bujumbura, Burundi.
Mossi ambaye aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa Shirika la
Habari la Kimataifa la BBC, Idhaa ya Kiswahili alipigwa risasi leo saa nne asubuhi na kuwahishwa katika hospitali
ya jeshi na kubainika kuwa amefariki dunia.
Msemaji wa Polisi wa Burundi, Pierre Nkurikiye, amenukuliwa
na vyombo mbalimbali vya habari akithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Taarifa zinasema kuwa mbunge huyo alipigwa risasi baada ya
kusimamisha gari lake llilokwanguliwa na gari lingine na kisha watu hao
kummiminia risasi na kukimbia kusikojulikana.
Wakati wa uhai wake Mossi alishika nyadhifa mbalimbali
serikalini kabla ya kuwa mbunge wa EALA kuanzia Juni mwaka 2012 ambapo kabla ya
hapo alikuwa Waziri wa Ofisi ya Rais anayeshughulikia masuala ya Afrika
Mashariki kwa miaka miwili kuanzia 2009 mpaka 2011.
Pia alihudumu kama Waziri wa Mawasiliano, Habari, Uhusiano na
Bunge na msemaji wa Serikali 2005 mpaka 2007.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amenukuliwa na vyombo vya
habari akielezea mauaji hayo yametekelezwa na waoga wabaya.
Katibu Mkuu wa EAC, Liberat Mfumukeko, alituma salamu za
rambirambi kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa ‘Twitter’ akielezea masikitiko
yake juu ya kifo cha kiongozi huyo.
Mbunge wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Adam Kimbisa alisema
kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kiongozi huyo ambaye wamekuwa
wakishirikiana naye katika kutekeleza majukumu ya uwakilishi wa wananchi wa EAC.
Msemaji wa serikali ya Burundi, Burundi Willy Nyamitwe alielezea
masikitiko yake juu ya kifo cha kiongozi huyo ambaye alikuwa mwanachama wa chama
tawala cha CNDD-FDD.
Mosi aliwahi kuwa mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika
Utangazaji la Uingereza (BBC).
Mossi atakumbukwa kwa kuwa mtetezi wa haki za wanawake pia ni
mwanasiasa wa kwanza kuuawa tangu kuanza kwa machafuko nchini Burundi mwaka
jana .
Hata hivyo, tangu Aprili mwaka 2015, Burundi imekuwa ikiandamwa
na matukio ya mauaji ya kupigwa risasi ya maofisa wa juu wa jeshi akiwemo Jenerali
Athanase Kararuza, Meja Didier Mihimpundu, Kanali Darius Ikurakure na Kanali
mstaafu Colonel Jean Bikomagu.
Mauaji hayo yametokea
siku moja baada ya sintofahamu kuibuka kwenye mazungumzo ya kutafutia suluhu
mgogoro wa Burundi kutokana na hatua ya ujumbe wa Serikali ya nchi hiyo
ukiongozwa na Waziri wa mambo ya nje, Alain Nyamitwa kutishia kususia.
Walitishia kususia awamu ya pili ya majadiliano hayo yaliyoanza juzi jiji hapa
wakipinga hatua ya Mwezeshaji wa mazungumzo hayo, Rais Mstaafu wa Tanzania,
Benjamin Mkapa ya kuwaalika watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika na jaribio la
kumpindua Rais Nkurunziza.
Hafsa
Mossi enzi za uhai wake.
No comments:
Post a Comment