Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna'ashariyyah Tanzania, Sheikh Hemedi Jalala ametoa salamu za sikukuu kwa kusema jumuiya ya Shia inaungana na Wakristo katika kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, tukio hilo ni la maana kubwa ya kimaadili inayovuka mipaka ya kidini.
Ameeleza kuwa Krismasi ni kipindi kinachohusishwa na upendo, kujitolea, huruma na maadili ambayo ni muhimu kwa mshikamano wa kijamii na utulivu wa taifa.
Sheikh Hemedi Jalala akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa salamu za heri ya sikukuu njema na salamu za pekee kwa Wakristo watakaoadhimisha Sikukuu ya Krismasi Desemba 25,2025 ulimwenguni kote.
"Kwa Wakristo wanaoadhimisha Sikukuu ya Krismasi, ni budi taifa kutumia kipindi hiki cha sherehe kuimarisha amani, umoja na mshikamano na kuendeleza heshima na kuheshimiana siyo kutengeneza chuki na kubaguana kwani Mungu ni Mmoja aliyetuumba itikadi zetu za Kidini tuziweke pembeni" Amesema Shekh Jalala
Hata hivyo amebainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanakuja katika wakati nyeti kwa nchi, kufuatia msongo wa kijamii na kihisia uliosababishwa na matukio ya Oktoba 29 hivyo kipindi hiki kinapaswa kutumika kama fursa ya uponyaji na maridhiano, akiwahimiza wananchi kuachana na misuguano na kukumbatia mazungumzo na uelewano
Hata hivyo amebainisha kuwa Tanzania haibagui raia wake kwa misingi ya dini, kabila au mwonekano, akieleza kuwa kanuni hiyo ni moja ya nguvu kubwa za taifa. Kudumisha hali hiyo, alisema, kunahitaji juhudi endelevu, hasa katika nyakati za mvutano wa kijamii au kisiasa.
Kwa Upande wake Mshauri wa Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna'ashariyyah Tanzania, Mzee Azim Dewji akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari wakati akitoa salamu za heri njema na salamu za pekee kwa Wakristo wanaoadhimisha Sikukuu ya Krismasi katika Msikiti wa Ghadiir, uliopo Kigogo Post, jijini Dar es Salaam.
Amesema vijana wana jukumu muhimu katika kuulinda mustakabali wa taifa na wanapaswa kuhimizwa kukataa vurugu, migawanyiko na kutovumiliana.
Sambamba na hayo amebainisha kuwa jumuiya ya Shia inaungana na Wakristo katika kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo, tukio alilolitaja kuwa na maana kubwa ya kimaadili inayovuka mipaka ya kidini. Alieleza kuwa Krismasi ni kipindi kinachohusishwa na upendo, kujitolea, huruma na maadili ambayo ni muhimu kwa mshikamano wa kijamii na utulivu wa taifa.
"Miongo kadhaa, Tanzania imekuwa ikiheshimika kwa utamaduni wake wa kuishi kwa amani kati ya watu wa dini, tamaduni na asili tofauti. Alisema umoja huo umekuwa nguzo ya utambulisho wa taifa na umechangia kulinda sifa ya Tanzania kama nchi ya amani katika eneo ambalo mara nyingi hukumbwa na migogoro" Amesema Azim Dewji
Sanjari na hayo amewasisitiza vijana kuwa wana nafasi kubwa katika kuamua hatima ya taifa na lazima wahamasishwe kukataa vurugu, migawanyiko na kutovumiliana.
“Krismasi hii iwe ukumbusho kwa vijana wetu kuhusu sisi ni nani kama taifa watu waliojengwa juu ya misingi ya amani, heshima na mshikamano. Kulinda taswira hiyo kunahitaji mchango wa kila raia,” Alisema Sheikh Jalala.
Alisema dhamira ya jumuiya ya Shia katika kukuza mahusiano ya amani kati ya waumini wa dini tofauti. Alisisitiza kuwa imani haipaswi kamwe kutumika kama chombo cha kugawanya watu, bali iwe msingi wa ushirikiano na mazungumzo ya kidini yanayolenga kujenga jamii yenye haki na jumuishi.
Pia amewahimiza Watanzania kusherehekea sikukuu kwa uwajibikaji, wakitanguliza amani, usalama na heshima kwa wengine. Alieleza matumaini yake kuwa msimu wa Krismasi utapita kwa utulivu na kusaidia kurejesha imani na mshikamano katika jamii
Aidha Jumuiya ya Shia Ithna'ashariyyah inawatakia Watanzania wote Krismasi njema yenye amani na furaha, akionyesha imani kuwa roho ya umoja na huruma inayohusishwa na sikukuu hiyo itaendelea hata baada ya sherehe na kuchangia amani ya kudumu na maendeleo ya taifa.




No comments:
Post a Comment