Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Bodi ya Wadahamini ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (0RCI) imetakiwa kujiwekea mkakati wa kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitatu hakuna Mtanzania yoyote anayekwenda kutibiwa saratani nje ya nchi kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye vifaa na miundombinu ya kisasa na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache Afrika iliyopiga hatua kubwa kwa kuwa na huduma ya kisasa katika kutibu saratani.
Kauli hiyo imetolewa naWaziri wa Afya Mohammed wakati akizindua bodi hiyo ambapo kabla ya kuzindua, alikagua miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na ORCI, ikiwemo ununuzi na ufungaji wa mashine tatu mpya za kisasa za matibabu ya saratani (LINAC na Cobalt), upatikanaji wa mashine za kisasa za uchunguzi na matibabu ikiwemo PET CT, uanzishaji wa kinu cha kuzalisha dawa za nyuklia (Cyclotron) kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya saratani pamoja na ujenzi wa jengo jipya la huduma za kimataifa linalolengakuimarisha huduma kwa wagonjwa wa ndani na nje ya nchi.
Waziri Mchengerwa ameipongeza Menejimenti ya ORCI kwa kutekeleza maelekezo aliyoyatoa Disemba mwaka jana wa kuitaka menejimenti hiyo kuzifunga mara moja mashine tatu za uchunguzi wa PET zilizokuwa hazijafungwa ambapo hadi mwezi februari mwaka huu zitakuwa zikitoa huduma baada ya mafundi kutoka Marekani na Ujerumani kukamilisha kazi hiyo.
Aidha Waziri Mchengerwa katika ziara hiyo aameongea na wagonjwa waliokuwa wakipatiwa huduma ambao kwa niaba ya wagonjwa hao Bi. Justina Allen amemshukuru Rais Samia kwa kuboresha huduma za Tiba Mionzi katika kipindi kifupi cha utawala wake kwenye hospitali hiyo.
“Kwa sasa tunamshukuru Mhe. Samia kwa kuboresha huduma ya tiba ya mionzi kwenye hospitali hii kwa kwa sasa tunapata matibabu bure kwa sisi masikini baada ya kufuata utaratibu. Katika hali ya kawaida tusingeweza kumudu gharama hizi” amefafanua Bi Justina.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Dkt. Diwani Msemo amesema kuwa mara baada ya kukamilika kufunga mashine hizo tatu za mionzi kutasaidia kutatua changamoto ya hali ya sasa ambapo inamchukua mgonjwa kutumia wiki 20 kupata huduma ya mionzi kwa kutumia mashine mbili zilizopo sasa ambapo mashine hizo zikianza kufanya kazi wagonjwa watatumia wiki mbili tu kupata huduma.
Amebainisha kuwa kiwango hicho ni cha hali ya juu kabisa kwani katika bara la Afrika ni nchi chache ambazo zimefikia kiwango hicho huku akifafanua kuwa kwa sasa ni takribani wagonjwa mia mbili wanaweza kupata huduma lakini baada ya mradi huo kukamilika zaidi ya wagonjwa 400 wataweza kutibiwa kwa siku nakufanya kukosekana kwa wagonjwa hivyo kwa sasa wamekuwa na mkakati wa kutafuta masoko nje kutoka nje kwa ajili ya tiba ya mionzi ya kiutalii kwa wagonjwa wa nje ya nchi.
Hata hivyo Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa mageuzi ya kweli ya huduma za saratani hayaishii kwenye majengo mapya, mashine kubwa, au miundombinu pekee bali mageuzi ya kudumu huanzia katika usanifu wa utoaji huduma kwa mgonjwa (service delivery design), na kuendelea kwenye mfumo mzima wa uzoefu wa mgonjwa (patient journey) kuanzia anapoingia mpaka anapomaliza huduma.
Kwa mantiki hiyo,ameitaka Bodi hiyo kuwa bunifu, jasiri, na ivunje mazoea ya zamani na kwamba ORCI inapaswa kuwa kigezo cha ubunifu katika huduma za saratani barani Afrika, kwa kuzingatia ubunifu katika utoaji wa huduma (service delivery design) ili kupunguza muda wa kusubiri, kurahisisha taratibu, na kuongeza heshima kwa mgonjwa.
”ORCI haiwezi kuwa Taasisi ya kawaida.ORCI lazima iwe mamlaka ya Afrika katika saratani.”Amesisitiza Waziri Mchengerwa.
Pia matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo mifumo thabiti ya taarifa za kitabibu (Electronic Medical Records – EMR) na mifumo ya kidijitali ya kupanga huduma, kupunguza urasimu usio wa lazima unaoongeza gharama, ucheleweshaji, na msongo kwa wagonjwa na familia zao.
Waziri Mchengerwa ameitaka Bodi hiyo pia ijiwekee mifumo thabiti ya usimamizi kupitia Kamati za Bodi, huku ikizingatia falsafa ya “eyes on, hands off” – yaani kusimamia kwa karibu bila kukuingilia majukumu ya kiutendaji ya Menejimenti.
Amefafanua kuwa jitihada za Serikali za Awamu ya Sita ni kuinua viwango vya huduma za afya, huku akisema ameshaelekeza hospitali zote kubwa na za rufaa nchini kuhakikisha zinapata ithibati za kimataifa, ikiwemo viwango vya ISO na vyeti vingine vinavyotambulika kimataifa.
Aidha amesema lengo kuu la ORCI ni, na litaendelea kuwa, kutibu, kuokoa maisha, na kuboresha huduma kwa wagonjwa huku akitaka baadhi ya mambo yaende sambamba, si kushindana.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na tiba bora na ya wakati kwa mgonjwa, utafiti unaotokana na huduma halisi na machapisho yanayoboresha miongozo ya matibabu na clinical standards.
Pia ameielekeza Bodi hiyo kuweka mkakati wa kitaifa na wa Afrika wa utafiti wa saratani,kujenga ushirikiano wa kweli na Taasisi zinazoongoza Afrika na duniani, na kuwasilisha mpango mahsusi, unaopimika na unaotekelezeka, wa kuifanya ORCI kuwa Taasisi inayoongoza kwa utafiti wa saratani barani Afrika, ndani ya uongozi wenu wa sasa.





No comments:
Post a Comment