WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ametoa siku moja kwa uongozi wa Manispaa ya Morogoro kutenga maeneo maalumu kwa
ajili ya wafanyabiashara wadogo na kuyatangaza kesho.
“Mbali na kutenga maeneo pia
nawaagiza muwasaidie wafanyabiashara hawa kuunda vikundi kulingana na aina ya
biashara wanazozifanya ili kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi kutoka katika
taasisi za fedha” alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo
hilo leo (Jumatano, Agosti 03, 2016) wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa kituo
cha mabasi Msamvu unaojengwa kwa ubia kati ya Manispaa ya Morogoro na Mfuko wa
Pensheni wa LAPF.
Awamu ya kwanza ya mradi huo
inatarajiwa kufunguliwa Agosti 12 mwaka huu utakuwa ni kituo cha mabasi cha
kwanza cha kisasa Tanzania ambapo Waziri Mkuu amezitaka halmashauri zote
zilizoko makao makuu ya mikoa nchini kuiga mfano huo.
Waziri Mkuu alitumia fursa
hiyo kulipongeza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Morogoro na LAPF kwa kubuni
mradi huo wa kisasa utawezesha abiria kupata taarifa ya basi lilipo na muda
litakapowasili kituoni hapo hivyo kupunguza udanganyifu kutoka kwa mawakala wasiokuwa
waaminifu.
Kwa upande wake Meneja wa
mradi huo Stanley Mhapa alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni 40 ambapo
Manispaa inamiliki asilimia 40 ya hisa na mfuko wa LAPF unamiliki asilimia 60.
“Mafanikio ya mradi huu ni
pamoja na kuiwezesha Manispaa kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka sh 350,000 kwa
siku hadi kufikia sh. milioni 1.7 kwa siku,” alisema.
Mhapa alisema mradi huo
utakapokamilika utatoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za kibenki,
vibanda vya biashara, sehemu za chakula, ofisi na sehemu ya mapumziko ya abiria
na vibanda vya kukatia tiketi.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO,
AGOSTI 03, 2016.
No comments:
Post a Comment