UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote,
naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutupa afya
njema hadi kutufikisha siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge lako
Tukufu tuliouanza tarehe 6 Septemba, 2016.
2.
Nitumie fursa hii pia kukupa pole, Mheshimiwa Spika, kwa
maradhi yaliyokusibu lakini kikubwa nielezee furaha yangu kwa uponyaji ambao
Mwenyezi Mungu amekujaalia na hivi sasa tuko pamoja humu ndani. Tunakuombea kwa
Mwenyezi Mungu uendelee kupata nguvu na afya njema.
3.
Mheshimiwa Spika, tangu tulipokutana
mara ya mwisho, kumekuwepo majanga na matukio mbalimbali ya maradhi, ajali,
ujambazi na matukio mengine ambayo yamesababisha vifo na majeruhi kwa
Watanzania wenzetu, wakiwemo Waheshimiwa Wabunge. Hivyo, ninatoa pole kwa
wafiwa wote na wale wote waliopatwa na majanga kutokana na matukio hayo. Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha
na waliopo hospitali.
4.
Mheshimiwa
Spika, leo tunahitimisha mkutano huu tukiwa tumekamilisha shughuli zote
zilizopangwa
kwenye Mkutano huu. Naomba nitumie fursa hii ya awali kabisa kukupongeza sana
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti na Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote kwa ufanisi mkubwa. Kazi hizo
zilijumuisha kujadili na hatimaye kupitisha Miswada mbalimbali ya Serikali.
Napenda kukiri kwamba mijadala ya mkutano huu ilikuwa ya uwazi na hoja
zilizotolewa zililenga kuiletea maendeleo nchi yetu. Kutokana na michango
mizuri ya Waheshimiwa Wabunge na yenye tija, ilibidi mara kadhaa vikao vyetu
kuendelea hadi usiku nje ya muda wa kikanuni. Nawapongeza sana!
TUKIO LA JANGA LA TETEMEKO LA ARDHI LILILOTOKEA MIKOA YA
KANDA YA ZIWA
5.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka
kuwa tarehe 13 Septemba, 2016
Serikali iliwasilisha hapa Bungeni taarifa ya masikitiko kuhusu maafa makubwa
yaliyoikumba Nchi yetu tarehe 10 Septemba, 2016 kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea
katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Kagera, Geita, Mwanza na Mara. Tukio hilo ambalo
liliathiri zaidi Mkoa wa Kagera lilitokea siku ya Jumamosi majira ya saa 9.27
alasiri, ambapo Mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi, lenye nguvu ya
mtetemo wa kipimo cha 5.7, kwa kutumia skeli ya “Ritcher”. Tetemeko hilo
limesababisha vifo vya watu 17 na
majeruhi 253. Napenda nitumie nafasi
hii kwa mara nyingine kuwapa pole wafiwa wote na wale waliopata majeraha
mbalimbali. Tunaomba Mungu aziweke roho za Marehemu mahali pema peponi. Amina. Kwa
wale waliopata majeraha, tunamuomba Mungu awaponye haraka.
6.
Mheshimiwa Spika, tukio hilo
limesababisha uharibifu mkubwa sana wa nyumba, vituo vya afya, shule pamoja na
miundombinu ya barabara. Aidha, shule nne
za Nyakato, Ihungo, Kashenge na Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo, nyumba za
walimu, kumbi za shule na mabweni. Nyumba 840 zimeteketea kabisa, na nyingine 1,264
kupata nyufa. Kwa sasa uongozi wa Mkoa
wa Kagera pamoja na Kamati ya Maafa ya Mkoa na Wataalamu
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wataalamu wa masuala ya matetemeko, na wadau
wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya kiasi cha hasara iliyopatikana.
7.
Mheshimiwa Spika,
kama Bunge lako Tukufu lilivyojulishwa, Serikali kwa kushirikiana na Wadau
mbalimbali, imechukua hatua kadhaa kushughulikia athari za tetemeko hilo ikiwa
ni pamoja na kufanya jitihada ya kurejesha hali ya utulivu, miundombinu
iliyoharibika ili kuirejesha katika hali ya kawaida.
8.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada
mbalimbali zilizofanyika ikiwemo viongozi kutembelea maeneo yenye madhara, mpaka
sasa Serikali imefanya mambo yafuatayo:-
(a)
Kuhusu Chakula: Wananchi wenye
mahitaji ya chakula wameendelea kupatiwa chakula kama vile, unga, mchele na
maharage, sukari na chumvi pamoja na mafuta ya kula. Tathmini ya kubaini
mahitaji halisi ya chakula inaendelea.
(b)
Kuhusu Matibabu: Serikali imeimarisha Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Kagera kwa kupeleka dawa na vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa.
Aidha, Timu ya Wataalam na Madakta 12 wamepelekwa Bukoba kutoka Hospitali ya
rufaa ya Kanda ya Bugando. Napenda kuwashukuru pia wadau mbalimbali ambao
wamechangia eneo hili wakiwemo Medecins
Sans Frontiers, Ubalozi wa China, Jhpiego
(USAID) na Chama cha Wafamasia.
(c)
Makazi: Wananchi waliokosa kabisa hifadhi ya
makazi wamepewa maturubai na mahema kwa ajili ya makazi ya muda. Aidha, waathirika
ambao nyumba zao zimebomoka kabisa, kwa kuanzia kila mmoja ametengewa mabati
20, saruji mifuko mitano, blanketi na mikeka. Pia wapangaji waliokuwa katika
nyumba hizo kila mmoja ametengewa kodi ya pango ya miezi sita ili apate mahali
pa kujihifadhi.
(d)
Kuhusu Shule
zilizoathirika:
Serikali inajenga miundombinu ya muda ya shule kama vile madarasa, mabweni na
vyoo hususani katika shule za sekondari za Ihungo na Nyakato zilizofungwa kwa
muda wa wiki mbili. Tathmini ya kitaalam ikikamilika, mpango wa ujenzi wa
miundombinu ya kudumu itafanyika na maandalizi yanaendelea kupata rasilimali
kwa ajili hiyo.
(e)
Mazishi: Serikali imeshiriki
katika kuwafariji wafiwa na pia kushiriki mazishi kwa kusaidia kutoa jeneza,
sanda, usafiri na kutenga fedha Shilingi milioni 20 za rambirambi kwa wafiwa
ambazo zitatolewa kwao muda wowote kuanzia sasa.
(f)
Barabara: Tathmini ya uharibifu wa barabara
imefanyika na barabara zilizoharibika zitarejeshwa katika hali ya kawaida ili
wananchi waendelee kupata huduma za msingi. Vilevile, Serikali inaendelea
kuchukua hatua za kuhakikisha miundombinu ya maji safi na maji taka inakarabatiwa
na kuhakikisha usafi unaendelea kuwa katika viwango stahiki.
Kwa ujumla, Serikali
imejipanga kuhakikisha kuwa taasisi za umma ikiwemo majeshi ya ulinzi na
usalama na rasilimali zake vinatumika kutoa huduma zote muhimu kwa waathirika
katika kipindi hiki.
9.
Mheshimiwa
Spika, hivi sasa
Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kitaalam kupitia Wizara ya Nishati na
Madini, Chuo cha Madini Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kubaini chanzo
cha tukio, kiasi cha athari zilizotokea chini ya miamba na juu ya ardhi.
Tathmini hii ya kitaalamu itatupa picha na mwelekeo wa kushughulikia urejeshaji
wa miundombinu iliyoharibika.
10.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie
nafasi hii kukushukuru sana wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na
Waheshimiwa Wabunge kwa namna mlivyoshirikiana na Serikali katika kushughulikia
janga hili la kitaifa la tetemeko la ardhi Napenda kuwashukuru Waheshimiwa
Wabunge kwa michango yenu ya hali na mali na kwa kututia moyo katika
kushughulikia tukio hili kubwa lililoathiri maisha na shughuli za wananchi pale
mkoani Kagera.
11.
Mheshimiwa
Spika, vilevile, kwa niaba ya Serikali, na kipekee, nitumie fursa hii
kuishukuru Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Waheshimiwa Mabalozi, Wawakilishi
wa Mashirika ya Umma na ya Kimataifa waliopo nchini, viongozi wa vyama vya
siasa na wananchi kwa ujumla, ambao waliitikia wito wa Serikali wa kushiriki na
kusaidia juhudi za Serikali za kuwasaidia waaathirika wa tetemeke la ardhi. Tunawashukuru
sana wote waliotuunga mkono kwa fedha na vifaa mbalimbali.
12.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na jitihada hizo zinazofanywa, Serikali imeshatoa na
inaendelea kukusanya michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali. Hivyo, kwa wananchi na wadau walio tayari
kuchangia wanaweza kutumia Akaunti ya Maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB
yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa
jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode:
CORUtztz kwa kutuma fedha kwa njia ya kawaida au Mobile Banking. Vilevile, michango hiyo inaweza kutumwa kwenye Namba
za simu za mkononi, 0768-196-669 (M-Pesa),
au Namba 0682-950-009 (Airtel Money) au Namba 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Nawaomba
wananchi wote, Sekta Binafsi na Jumuiya ya Kimataifa tuonyeshe mshikamano
kuungana na Serikali katika kusaidia wenzetu walioathirika na tetemeko hilo kwa
kutoa michango ya hali na mali.
13.
Mheshimiwa
Spika, nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali
itaendelea kuratibu michango yote itakayotolewa na kuifikisha kwa walengwa.
Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kuimarisha
uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na majanga ya aina hii na mengineyo.
SHUGHULI
ZA BUNGE
14.
Mheshimiwa Spika, tunahitimisha
mkutano huu tukiwa tumepata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na Kauli
mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali na kusomwa kwa mara
ya pili na pia kusomwa mara ya tatu ni kama ifuatavyo:-
Kwanza: Muswada wa Sheria ya upatikanaji wa Habari
wa mwaka 2016; (The Access to Information
Bill, 2016);
Pili: Muswada wa Sheria ya Uthamini na
Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016; (The
Valuation and Valuers Registration Bill, 2016);
Tatu: Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya
Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016; (The Government Chemist Laboratory Authority Bill, 2016);
Nne: Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa
Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016; (The
Chemist Professionals Bill, 2016);
Tano: Muswada wa Sheria ya Taasisi ya
Utafiti wa Kilimo wa Mwaka 2016; (The
Tanzania Agricultural Research Institute Bill, 2016);
Sita: Muswada wa Taasisi ya Utafiti wa
Uvuvi wa Mwaka 2016; (The Tanzania
Fisheries Research Institute Bill, 2016).
Miswada ya Sheria ya Serikali iliyosomwa kwa mara ya
kwanza ni:-
(a)
Muswada
wa Sheria ya huduma za Hbari za Mwaka 2016 (The
Media services Bill, 2016).
(b)
Muswada
wa Sheria ya marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016 (The Written Laws Micellianeous Amendments)
(No.3) Bill, 2016).
15.
Mheshimiwa Spika, katika Bunge hili,
Serikali ilitoa kauli zifuatazo:-
Kwanza: Kauli
ya Serikali kuhusu hali ya chakula nchini na uzalishaji kwa msimu wa mazao kwa
mwaka 2015/2016; na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017;
Pili: Kauli
ya Serikali kuhusu tukio la tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba,
2016 Mkoani Kagera na Mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa.
16.
Mheshimiwa Spika, kipekee, naomba
kutumia fursa hii kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Wataalam
wake, kwa mchango wao mkubwa katika kuandaa miswada hiyo kwa umakini mkubwa na
hivyo kuwawezesha Waheshimiwa Mawaziri kuiwasilisha Bungeni kwa weledi mkubwa.
Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango
yao mizuri. Serikali itazingatia ushauri na maoni yenu wakati wa utekelezaji.
17.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 110 ya msingi na mengine 222
ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Vilevile,
jumla ya maswali matano ya msingi na ya nyongeza ya
Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu ya kila Alhamisi yaliulizwa na kupata
majibu.
MWENENDO NA MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI
18.
Mheshimiwa Spika, katika siku za hivi
karibuni, kumekuwepo na wasiwasi kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi, hususan
mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa Taifa. Napenda kutumia fursa hii
kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kuwa mwenendo wa
uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika. Aidha, tathmini iliyofanyika
kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya fedha, inaonesha
kuwa Mabenki yetu bado yapo salama, na yana mitaji ya kutosha na mwenendo wa
sekta ya fedha ni wa kuridhisha. Aidha, Wizara ya Fedha na Mipango,
Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ya Taifa ya Takwimu zinafuatilia kwa karibu
kuhusu mwenendo wa Hali ya Uchumi Nchini. Mathalan, tarehe 14 Septemba, 2016
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu, alitoa taarifa kwa vyombo
vya habari kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini ambapo alilihakikishia Taifa
na Jumuiya ya Kimataifa kwamba hali ya uchumi wetu ni shwari kabisa na si mbaya
kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
19.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa hiyo
ya Benki Kuu pamoja na mambo mengine, imebainishwa kwamba katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa uchumi wa
Tanzania umeendelea kuwa wa kuridhisha. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka
2015. Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano,
utangazaji na huduma ya intaneti; kuongezeka kwa uchimbaji na madini. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu katika kipindi hicho ni sekta ya fedha kwa asilimia
13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.
20.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mwenendo huo mzuri wa viashiria vya
shughuli za uchumi, ni dhahiri kwamba mwelekeo wa uchumi katika kipindi kijacho
unatoa matumaini ya uchumi kuendelea kuimarika kama ilivyokadiriwa hapo awali
na kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa Pato la Taifa la asilimia 7.2 kwa mwaka
2016. Hii inachangiwa pia na ukweli
kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri katika kuimarisha uchumi
endelevu; usimamizi thabiti wa rasilimali za umma; na ujenzi wa miundombinu
bora yenye kuimarisha lengo la kujenga
uchumi wa viwanda chini ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
MWENENDO WA UKUSANYAJI WA MAPATO YA SERIKALI KWA MWEZI JULAI NA AGOSTI,
2016
21.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuongeza na
kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali. Katika
mwaka 2016/17, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza
utegemezi wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, Serikali
imeendelea kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi ili kuleta tija kwa Taifa katika
ukusanyaji mapato.
22.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali imelenga kukusanya mapato ya ndani, ikijumuisha mapato ya
Halmashauri, ya jumla ya shilingi trilioni 18.46, sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote ya shilingi trilioni 29.5. Takwimu
za mwenendo wa ukusanyaji mapato zinaonesha kuwa katika kipindi cha kuanzia
Julai hadi Agosti, 2016, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), yalikuwa shilingi trilioni 2.168
ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113, sawa na asilimia 103 ya lengo. Aina za kodi zilizochangia
sana katika ongezeko hilo ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mashine za kielektroniki katika
ukusanyaji wa mapato. Mapato yasiyo ya kodi kwa kipindi hicho yalikuwa shilingi
bilioni 271.1; sawa na asilimia 60
ya lengo la kukusanya shilingi bilioni
448.4. Aidha, mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yalikuwa Shilingi bilioni 45.4; ikiwa ni asilimia 41 ya lengo
la kukusanya shilingi bilioni 110.9.
Napenda kutumia fursa hii kuzihimiza
Wizara na Halmashauri kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
23.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-
Kwanza: Kuendelea kuimarisha usimamizi wa
ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika
maeneo ya biashara, viwandani, migodi, bandarini, kwenye viwanja vya ndege na
maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kodi stahiki zinakusanywa;
Pili: Kusimamia kikamilifu matumizi ya
vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza
ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;
Tatu: Kuendelea kupanua wigo
wa walipa kodi, ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze
kuingia katika mfumo wa kodi;
Nne: Kuimarisha ufuatiliaji wa mapato
yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali na Halmashauri zote
nchini; na
Tano: Kuendelea kuchukua hatua za
kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.
MPANGO
WA SERIKALI WA KUHAMIA DODOMA
24.
Mheshimiwa Spika, tarehe 23 Julai,
2016 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi hapa Dodoma
alieleza kuhusu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukamilisha mchakato na
ahadi ya Serikali ya kuhamia katika Mji wa Makao Makuu – Dodoma. Aidha,
Mheshimiwa Rais alirejea kauli hiyo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa Maadhimisho
ya Siku ya Mashujaa Nchini ambayo yalifanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza katika
Viwanja vya Mashujaa, mjini Dodoma. Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa anatarajia
kwamba Serikali yake yote itakuwa imehamia Dodoma katika kipindi cha miaka minne
na miezi minne, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2020.
25.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwamba Mpango wa sasa wa Serikali
wa kuhamia Dodoma ni mwendelezo wa utekelezaji
wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 iliyozingatia agizo
lililotolewa tarehe 1 Oktoba, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa Chama cha TANU.
Hivyo, hatua zinazochukuliwa sasa na Serikali ya Awamu ya Tano ni mwendelezo tu wa
utekelezaji wa mipango ya awali iliyokuwa inatekelezwa mwaka hadi mwaka na
Serikali za Awamu zilizopita, kuanzia Awamu ya Kwanza lilipotolewa tamko hilo
mwaka 1973; chini ya Uongozi wa Rais wa
Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
26.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza
azma hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano, baada ya tamko la Mheshimiwa Rais Dkt.
John Pombe Magufuli la tarehe 23 Julai 2016, yafuatayo yamefanyika:
Kwanza: Tarehe
26 Julai, 2016 nilikutana na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma (Viongozi wa Chama na
Serikali wa Mkoa na Wilaya, Wazee maarufu, Viongozi wa Madhehebu ya Dini na
Wadau mbalimbali) ili kuwajulisha kuhusu mkakati wa sasa wa Serikali wa kuhamia
Dodoma. Aidha, niliutaka Uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuwasilisha mapendekezo ya
mpango kazi wa kutekeleza uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma;
Pili: Katika
kipindi cha siku 14, Uongozi wa Mkoa wa Dodoma uliwasilisha kwangu Taarifa ya
Serikali kuhamia Dodoma kama ilivyokusudiwa. Aidha, tarehe 15 Agosti, 2016 Mkoa
uliwasilisha Mpango huo katika Kikao cha Baraza la Kazi la Mawaziri pamoja na
Makatibu Wakuu na kupata ushauri na maoni yao ya kuuboresha;
Tatu: Serikali imeunda Kamati Ndogo chini
ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji
wa Makao Makuu Dodoma (CDA) kwa lengo la kufanya mapitio ya upatikanaji wa
Ofisi na Makazi na miundombinu muhimu. Kamati hiyo inashirikisha Taasisi
mbalimbali za Serikali zilizopo Dodoma na Kitaifa, zikiwemo TBA, DUWASA,
TANROADS, TEMESA, TANESCO, SUMATRA, TTCL, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji;
Nne: Aidha, Serikali imeunda Kamati ya
Kitaifa ya Makatibu Wakuu ambao wanaratibu zoezi zima na utaratibu wa Serikali
kuhamia Dodoma;
Tano: Tarehe 1 Septemba, 2016, Serikali
ilikutana na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Fedha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na
Watendaji Wakuu wa Taasisi za Sekta Binafsi zinazohusika na ujenzi wa
miundombinu nchini. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kupata mawazo ya Sekta
Binafsi, Taasisi za Fedha na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuisaidia Serikali
kuboresha mikakati ya kuhamia Dodoma kwa kuzingatia kuwa Serikali peke yake
haiwezi kukamilisha jambo hili. Katika kikao hiki tumekubaliana kwamba kuanzia
sasa kuwepo na vikao baina ya Makatibu Wakuu na Wadau wa Sekta Binafsi, angalau
mara moja kwa mwezi chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa
Kamati hiyo akiwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kikao hicho kitakuwa cha
mashauriano na kupeana mrejesho wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhamia
Dodoma kwa kuzingatia mchango wa sekta ya umma na sekta binafsi katika ujenzi
wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii, uwekezaji na uzalishaji biashara na
huduma mbalimbali;
Sita: Serikali
pia imeunda Kamati Maalum ya Wataalam Washauri itakayoshirikiana na CDA kufanya
Mapitio ya Mpango Kamambe (Master Plan)
wa Mji wa Dodoma ili kubaini mahitaji halisi ya sasa na siku zijazo katika upeo
wa miaka 50 na zaidi. Zoezi hili litahitaji ushirikishwaji mkubwa wa jamii na
sekta binafsi. Lengo la Serikali ni kuwa na mji uliopangwa vizuri na unaozingatia
vigezo mbalimbali vya Kimataifa.
27.
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha
Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inatambua jitihada kubwa
zilizofanywa na Serikali za awamu zilizopita zilizoongozwa na Chama cha
Mapinduzi za kuweka miundombinu mbalimbali muhimu ya kufanikisha mpango wa
Serikali kuhamia Dodoma. Tathmini iliyofanywa na OWM, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
pamoja na wadau mbalimbali, inaonyesha kuwa kwa ujumla miundombinu iliyopo
Dodoma kwa sasa ina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya Serikali kuhamia Dodoma
kwa awamu kuanzia mwezi huu wa Septemba, 2016 hadi mwaka 2020.
RATIBA YA SERIKALI
KUHAMIA DODOMA
28.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha
azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa ratiba itakayowezesha
Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi mwaka 2020,
bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka 2016/2017 kama ifuatavyo:
Kwanza: Awamu
ya Kwanza
itakuwa kati ya mwezi Septemba, 2016 na
Februari, 2017. Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu
wote, Manaibu Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza.
Aidha, kila Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na
wakati huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara
nyingine kuhamia Dodoma;
Pili: Awamu
ya Pili
itakuwa kati ya mwezi Machi 2017 na
Agosti 2017. Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali
kuweka katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha watumishi
wake kuja Dodoma;
Tatu: Awamu ya Tatu itakuwa kati ya
mwezi Septemba 2017 na Februari 2018;
ambapo Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya
Wizara.
Nne: Awamu
ya Nne
itakuwa kati ya mwezi Machi 2018 na
Agosti, 2018; na Awamu ya Tano
itakuwa kati ya Mwezi Septemba 2018 hadi
Februari, 2020. Katika kipindi hiki cha Awamu ya Tatu na Nne; Wizara
zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.
Tano: Awamu ya Sita, itakuwa kati ya mwezi Machi,
2020 na Juni, 2020 ambapo Ofisi ya Rais ikiongozwa na Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.
Nazishauri Wizara zote kuanzisha
mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki badala ya kuhama na mafaili kutoka
Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka Dodoma iwe ya kielektroniki.
29.
Mheshimiwa Spika, naomba kutumia
fursa hii kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali wa sekta binafsi na wadau wa
maendeleo wa ndani na nje kuwekeza Dodoma ili kuboresha zaidi miundombinu
iliyopo na kuongeza majengo ya Ofisi na makazi ya Watumishi kuwekeza katika
huduma za afya na elimu, huduma za kibiashara kama mabenki, maduka makubwa (Shopping Malls) na masoko, mahoteli na
maghala. Aidha, napenda kurejea maelekezo niliyoyatoa kwa Mamlaka ya
Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) na Mkoa wa Dodoma na Manispaa
kuhakikisha kwamba Mji Mkuu wa Dodoma unaendelezwa kwa kasi ili kupokea watumishi
wengi na familia zao pamoja na sekta binafsi watakaohamia Dodoma.
30.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza
kuwa Mkoa wa Dodoma na CDA wahakikishe kuwa pamoja na kuandaa maeneo ya makazi
na Ofisi, pia watenge maeneo maalumu ya huduma muhimu kama vile maeneo kwa ajili
ya kituo kikuu cha biashara, bustani, bandari kavu na kuendelea kuongeza eneo
la viwanda na huduma mbalimbali za kibiashara. Aidha, naagiza Mamlaka za
Mipango Miji Mkoani Dodoma na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo wa
kielektroniki wa upatikanaji wa viwanja ambao utatambua mahitaji kwa utaratibu
wa wazi, na bila urasimu usio wa lazima.
Vilevile, nashauri Wakazi wa Mkoa wa Dodoma na Sekta binafsi kutumia fursa hii
kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watumishi
na wageni wanapokuja Dodoma wasipate taabu kutafuta mahali pazuri pa kuishi.
SEKTA YA KILIMO:
Hali ya
Uzalishaji na Upatikanaji Chakula Nchini:
31.
Mheshimiwa Spika, tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya
chakula kwa mwaka 2015/16 iliyofanyika mwezi Juni 2016 inaonesha kuwa
uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa utafikia tani 16,172,841. Aidha, Mikoa 11 kati ya 26 ilibainika kuwa na
ziada ya chakula, mikoa 12 kuwa na utoshelevu wa chakula na miwili (2) uhaba wa chakula. Kutokana na mahitaji
ya chakula kwa mwaka 2016/2017 kuwa tani 13,159,326, nchi itakuwa na utoshelevu
wa chakula kwa wa asilimia 123, sawa na ziada ya tani 3,013,515
kwa mazao yote ya chakula.
32.
Mheshimiwa Spika, tathmini hii ilibaini pia kuwa chakula kingi
aina ya nafaka kilikuwa tayari kimesafirishwa nje ya nchi kutokana na nchi
jirani kutokuwa na mavuno mazuri bila kuzingatia kwanza haja ya utoshelevu wa
ndani ya nchi.
Ili kuhakikisha kuwepo kwa hali ya usalama wa
chakula Nchini na kuepuka baa la njaa hapo baadaye, Serikali imeamua kuwa
kuanzia tarehe 10 Septemba 2016 sehemu ya ziada ya nafaka ya mahindi na mchele
itasafirishwa nje ya nchi kwa vibali vitakavyotolewa kwa ya Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi pekee. Serikali itasimamia ili
kusiwe na upungufu wa chakula nchini.
33.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii
kuwataka Wakuu wa Mikoa yote nchini kuwahamasisha wakulima na wafanyabiashara kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo hususan mahindi na mpunga kwa kuyasindika, kabla ya
kusafirisha nje ya nchi ili yapate bei nzuri zaidi,
na pia kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Utaratibu wa kutoa
ruzuku ya pembejeo za kilimo katika msimu wa 2016/2017
34.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2003/2004 hadi mwaka 2015/2016, Serikali
imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya
chakula, na hususan mahindi, mpunga na mtama. Pia, ruzuku ya pembejeo hutolewa
kwa mazao ya biashara ya korosho, pamba, chai, kahawa na alizeti. Ruzuku hiyo, imekuwa
ikitolewa kwa kutumia mfumo wa vocha na vikundi vya wakulima kukopeshwa
pembejeo hizo kupitia taasisi za fedha na makampuni ya pembejeo za kilimo.
Pamoja na juhudi hizo, kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika kufikia lengo
hilo.
35.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi,
katika msimu wa 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ruzuku ya viuatilifu vya mazao ya kilimo na shilingi
bilioni 25 kwa ajili ya ruzuku ya
pembejeo nyingine za kilimo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 20 ni za kununua tani
21,892 za mbolea kwa kaya 354,928.
Aidha, Serikali italipia asilimia 30 ya
bei ya mbolea kwenye soko, sawa na shilingi 20,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa
mbolea ya kupandia; na shilingi 12,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya
kukuzia.
36.
Mheshimiwa
Spika, ili mbolea hizo ziweze kuwafikia walengwa kwa wakati na kwa bei
nafuu, Kampuni ya Mbolea Tanzania itasambaza mbolea katika vituo vyake 29 nchini na kuiuza kwa Mawakala wa Pembejeo za Kilimo
kwa shilingi 38,000 kwa mfuko wa
kilo 50 kwa mbolea ya kupandia na shilingi 26,000
kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kukuzia. Ninaziagiza
Halmashauri zote kuhakikisha Mawakala wa Pembejeo wanauza mbolea kwa bei
itakayopangwa. Ni imani yangu kuwa wakulima wengi watatumia fursa hii ya kupata
mbolea ya ruzuku kuendeleza kilimo cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara.
SEKTA YA USHIRIKA
Maboresho katika tasnia ya Ushirika
37.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa ushirika, kama chombo cha kuwaunganisha, kuwapa nguvu
na kuwatetea wanachama wao katika kilimo, ufugaji, uvuvi na tasnia nyingine,
unakabiliwa na changamoto nyingi za usimamizi mbovu, ubadhirifu na ufujaji mali
wa baadhi ya viongozi. Changamoto hizo zinawaumiza sana wakulima na kuwafanya wakate
tamaa katika uzalishaji, masoko na uendeshaji wa shughuli zao za kiuchumi.
38.
Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na
changamoto hizo, Serikali itafanya marekebisho makubwa ndani ya Tume ya
Maendeleo ya Ushirika; iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na
kuchukua hatua za kinidhamu kwa watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wa mali
za ushirika. Aidha, baadhi ya Maafisa
Ushirika waliokaa katika kituo kimoja kwa muda mrefu watahamishiwa katika
maeneo mengine.
39.
Mheshimiwa Spika, Serikali itafanya
marekebisho makubwa kwa Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) ambalo
limeshindwa kufanya kazi zake kwa weledi.
40.
Mheshimiwa Spika, katika kufufua
ushirika, Serikali itahuisha Sera ya
Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, na kuijengea Tume ya Maendeleo ya ushirika
uwezo wa kuajiri/kuhamishia watendaji katika ofisi za Mikoa na Halmashauri zote
ili kusimamia vyama vya ushirika; kufanya kaguzi za mara kwa mara, kuondoa
tatizo la upotevu wa rasilimali za vyama; kusimamia upatikanaji wa viongozi
wenye sifa na watendaji wenye weledi wenye kuongoza vyama kwa ufanisi; kupanua
wigo wa shughuli za ushirika katika sekta nyingine za kiuchumi zaidi ya kilimo
ili kuongeza idadi ya vyama vya ushirika nchini na hivyo kuchochea ukuaji wa
kipato kwa wananchi wengi.
SEKTA YA ELIMU
Motisha kwa
Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata
41.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi mzuri na wa
karibu shuleni, Serikali imeanza kutoa posho ya madaraka kwa Walimu Wakuu,
Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata kila mwezi kuanzia mwezi Julai, 2016
ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.09 kimetolewa. Aidha,
mpango mwingine uliopo ni kuwapatia Waratibu Elimu Kata pikipiki ili
ziwawezeshe katika ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za kielimu katika kata
zao nchi nzima. Kwa kuanzia, Waratibu Elimu Kata wa Mikoa 7 ambayo ilikuwa
na ufaulu wa chini katika matokeo ya kuhitimu darasa la saba tayari
wameshapatiwa jumla ya pikipiki 1,015. Mikoa iliyopatiwa pikipiki hizi pamoja
na idadi ya pikipiki ni kama ifuatavyo: - Dodoma
(192); Mara (99), Simiyu (122), Shinyanga (128), Tabora (200), Kigoma (135),
Lindi (139). Mikoa iliyobakia itapatiwa pikipiki chini ya programu ya
Kukuza Stadi za Kusoma na Kuandika ya LANES (Literacy and Numeracy Education Support Program) pamoja na UNICEF.
Upungufu wa Walimu na Miundombinu
42.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa upungufu wa walimu, Serikali imeamua walimu wapya
watakaoajiriwa mwaka 2016 wapangwe shuleni moja kwa moja na kwenye maeneo yenye
upungufu mkubwa wa walimu.
Hali
ya Madawati
43.
Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa tarehe 16 Machi, 2016
Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alitoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 30 Juni, 2016
kusiwepo mwanafunzi anayekaa chini kwa kukosa dawati.
44.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji
wa agizo la Mheshimiwa Rais, kufikia mwezi huu wa Septemba madawati 951,610 kwa
shule za Msingi yalitengenezwa na hivyo kufikia madawati 3,084,781 sawa na asilimia 94.4. Kwa upande wa shule za
sekondari, idadi ya madawati yaliyotengenezwa yamefikia madawati 1,490,488 sawa na asilimia 99.4 na kufanya upungufu kuwa madawati 182,864 kwa shule za Msingi
na 8,380 kwa Shule za Sekondari.
Madawati hayo
yanaendelea kutengenezwa na Mikoa ambayo haijakamilisha inatakiwa iwe
imekamilisha ifikapo tarehe 30 Septemba, 2016.
MAABARA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI
45.
Mheshimiwa
Spika, mahitaji
ya Maabara kwa shule za sekondari ni 10,803.
Maabara zilizopo ni 5,756 sawa na
asilimia 53.2 ya mahitaji. Upungufu
uliopo ni maabara 5,047 ambazo
zingine zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2016/17,
Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imetenga jumla ya shilingi bilioni 18.876 kwa ajili ya umaliziaji
wa maabara 2,135 katika shule za sekondari
kwenye Halmashauri mbalimbali nchini. Serikali inaendelea na ujenzi wa jumla ya
maabara 290 kupitia mpango wa MMES
II katika shule za sekondari 528.
Upungufu utakaokuwepo baada ya kukamilika kwa maabara hizi ni maabara 4,807.
Serikali itaendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuondoa upungufu
huo.
Mitihani
ya Elimu ya Msingi
46.
Mheshimiwa Spika, mtihani wa kumaliza darasa la saba
ulifanyika tarehe 7 hadi 8 Septemba, 2016 nchini kote. Idadi ya watahiniwa 795,761 walisajiliwa kufanya mtihani wa
kumaliza elimu ya msingi mwaka 2016. Aidha, taarifa za awali zinaonesha kuwa
takriban watahiniwa 789,302
walifanya mtihani huo, sawa na asilimia 99.2 ya waliosajiliwa. Taarifa rasmi
itatolewa baada ya Mikoa na Halmashauri kukamilisha kufanya mawasilisho ya
taarifa kamili ya ufanyikaji wa Mtihani huo.
47.
Mheshimiwa Spika, tafsiri ya idadi ya
kubwa ya wanafunzi waliofanya mitihani ya darasa la saba ni kwamba yapo
matarajio kuwa idadi ya wanafunzi watakaoingia kidato cha kwanza katika mwaka
2017 itakuwa kubwa kuliko nafasi zitakazo kuwepo mwanzoni mwa mwaka 2017 katika
shule za Sekondari ikiwa hali ya miundombinu itaendelea kuwa kama ilivyo sasa. Hivyo basi, natoa wito kwa Halmashauri zote
nchini zijiandae kuwawezesha wanafunzi wote watakaofaulu kujiunga na kidato cha
kwanza kwa kuongeza vyumba vya madarasa, madawati, matundu ya vyoo na nyumba za
Walimu.
UHAKIKI
WA VYETI KWA WATUMISHI
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
na zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi ingawa limeendelea kuleta usumbufu
kwa watumishi katika baadhi ya maeneo. Naagiza kwa Wakurugenzi waandae vituo
maalum vilivyo jirani na vituo vyao vya kazi badala ya kuwakusanya kituo kimoja
ili kuwapunguzia adha na gharama. Halmashauri zote zizingatie agizo hili ili
maafisa utumishi waende kwenye vituo hivyo.
JITIHADA
ZA SERIKALI KUIMARISHA USAFIRI WA ANGA
49.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie
fursa hii kuzungumzia kidogo kuhusu jitihada za Serikali za kuimarisha usafiri
wa anga hapa nchini kuanzia mwaka 2016/2017 Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea
na mpango wake wa kuboresha usafiri wa anga hapa nchini. Hatua zinazochukuliwa
ni pamoja na kuendelea kuboresha viwanja vya ndege nchini. Lengo ni kuhakikisha
kuwa kila Mkoa unakuwa na kiwanja cha ndege cha kisasa, chenye ubora unaofaa
kutua ndege.
50.
Mheshimiwa Spika, ili kwenda
sambamba na azma ya Serikali kuhamia Dodoma muda mfupi ujao, kiwanja cha ndege
cha Dodoma kimefanyiwa ukarabati mkubwa ili kuweza kuhudumia ndege zenye uwezo
wa kubeba hadi abiria 90. Sambamba
na hatua hizo, Serikali imedhamiria kuimarisha Kampuni ya Ndege Tanzania
(ATCL), ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya kwa ajili ya kuongeza ufanisi
wa huduma za usafiri wa anga kupitia ATCL.
51.
Mheshimiwa Spika, napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imenunua ndege mbili (2) aina ya Dash 8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria
76 kila moja zitakazotumika kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani
na nchi jirani. Ndege hizo zinatarajia
kuwasili nchini mwezi huu wa Septemba, 2016.
Aidha, taratibu za kununua ndege nyingine mbili zenye ukubwa wa kati (medium haulage aircraft) zitakazokuwa na
uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 110 zimeanza. Ndege hizo zitahudumia soko la kikanda.
52.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua
hiyo Serikali imeanza kazi ya kuiunda upya ATCL. Jana tarehe 15 Septemba, 2016,
Mheshimiwa Rais amefanya uteuzi wa Mtendaji Mkuu mpya wa ATCL. Aidha, mchakato wa
uteuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo unakamilishwa. Vilevile, Serikali
imegharamia mafunzo ya wataalam mbalimbali wakiwemo wahandisi watakaohudumia ndege
mpya. Hatua hizo zitasaidia sana kuboresha shirika letu la ndege na usafiri wa
aga hapa nchini katika kipindi kifupi kijacho.
HALI YA AMANI NA UTULIVU NCHINI
53.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya
ulinzi na usalama vimeendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo
nchini kwa manufaa ya ustawi wa nchi yetu. Usalama wa raia na mali zao
umeendelea kudumishwa kwa kutambua kuwa ni miongoni mwa misingi mikuu ya ukuaji
wa uchumi wa Taifa letu. Kwa namna ya pekee, napenda kutumia fursa hii
kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa weledi.
54.
Mheshimiwa Spika, ili Jeshi la Polisi liendelee kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya
kubaini, kuzuia na kukabiliana na uhalifu Nchini, Serikali itaendelea kuwajengea
uwezo Maafisa, Wakaguzi na Askari na pia kutekeleza mambo yafuatayo:-
Kwanza: Kutabiri
mwelekeo wa uhalifu kwa kutumia takwimu za uhalifu, kumbukumbu za uhalifu
pamoja na mabadiliko ya uhalifu ili kuweza kutambua maeneo korofi, wahalifu
wanaohusika, mahali walipo na namna ya kukabiliana na uhalifu huo.
Pili: Kuyatambua
maeneo nyeti (hotspots) yenye vivutio
vya uhalifu, na kuyapangia ulinzi, misako na doria imara.
Tatu: Kutoa
elimu kwa jamii kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu kwa
kutumia vyombo vya habari, mihadhara, mikutano, maonesho na usambazaji wa
machapisho na vipeperushi.
Nne: Kufanya
misako na doria mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo
mbalimbali nchini.
Tano: Kushirikiana
na wadau wote wa ulinzi na usalama kubadilishana taarifa za kiintelijensia
pamoja na uzoefu katika kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo mipya na kuboresha ya
zamani.
55.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza
kuwa suala la amani, na usalama na utulivu nchini halina mbadala. Nawaomba
tudumishe hali ya amani na usalama ili tufanikishe lengo letu la kukuza uchumi
na kuondoa umaskini.
MICHEZO
56.
Nchi yetu imeendelea
kuwika kimichezo hasa katika soka. Nitumie fursa hii kuwapongeza vijana wetu wa
Serengeti Boys kwa ushindi wao. Hivi sasa timu yetu inajipanga kupambana na
timu ya Congo (DRC) hapo Septemba 18.
HITIMISHO
57.
Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha
mkutano huu leo, napenda nitumie nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na
Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia vizuri na kwa weledi mkubwa vikao vyote
vya mkutano huu. Niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu. Ninashukuru
pia Watendaji wa Serikali kwa kuwasaidia Mawaziri na Naibu Mawaziri katika
kujibu maswali na hoja mbalimbali za Wabunge. Niwashukuru madereva wote kwa
kuwaendesha Mawaziri, Wabunge na Watendaji wote kwa usalama kabisa. Thanx to
wanahabari kwa kuihabarisha jamii juu ya mkutano wetu. Kipekee, nimshukuru
Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah na timu yake kwa kutuwezesha kukamilisha
shughuli zote za mkutano huu kwa mafanikio makubwa.
58.
Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha
mkutano huu leo na kuelekea katika Majimbo yetu, sote tunatambua kuwa msimu wa
mvua za vuli na masika unakaribia.
Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuziagiza Wizara zinazohusika na
usambazaji wa pembejeo kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei
iliyopangwa. Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe kwamba wanasimamia kikamilifu
shughuli za kilimo katika maeneo yao ili kila familia na kaya ianze maandalizi
ya kilimo mapema.
59.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kurejea
katika kusisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya kukuza uchumi katika Taifa
letu. Hivyo, nichukue fursa hii kuwahakikishia wafanyabiashara na wenye viwanda
na wawekezaji kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwapa
ushirikiano wa dhati ili kuendeleza shughuli zao kama ambavyo wamejipanga. Wafanye shughuli zao bila woga au tashishi
yoyote.
60.
Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini si
kwa umuhimu, nitumie muda huu kumwomba Mwenyezi Mungu awalinde na awaongoze
Waheshimiwa Wabunge wote katika safari ya kurejea majumbani kwenu.
61.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo
hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 1 Novemba, 2016, siku ya Jumanne, Saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.
62.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment