HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 13, 2016

MAJALIWA APOKEA ZAIDI YA SH. BIL. 1.4 KWA AJILI YA MAAFA YA TETEMEKO LA KAGERA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Wafanyabishara na Mabalozi wa Nchi Mbalimbali hapa nchini kuwaomba wachangie katika kujenga na kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.Alikutana nao Ikulu jijini Dar es salaam Septemba 13, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa  akipokea hundi ya shilingi milioni 100 kutoka kwa Charge  d' Affairs wa ubalozi wa China nchini, Bw. Haodong Gou  wakati alipokutana na wafanyabiashara na mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini na kuwaomba wasaidie kuchangia ujenzi na ukarabati wa miundombinu iliyoathiriwa na tetemeko laardhi mkoani Kagera.  Mkutano huo ulifanyika Ikulu jijini Dar es salaam Septemba 13, 2016.Katikati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba. (Picha na Odisi ya Waziri Mkuu) 

xxxxxxxx
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea michango wa zaidi ya sh. bilioni 1.4 kutoka kwa mabalozi wa nchi za nje nchini Tanzania na Jumuia ya Wafanyabiashara wa Kitanzania kwa ajili ya kusaidia wananchi waliothirika na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera.

Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi, 10 Septemba, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17 hadi leo na wengine 253 kujeruhiwa. Pia limesababisha maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.

Akizungumza katika hafla ya uchangishaji fedha kwa ajili ya kusaidia wahanga hao leo (Jumanne, 13 Septemba, 2016) Waziri Mkuu amewashukuru kwa michango yao ya fedha na vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko 2,800 ya saruji. Amesema tetemeko hilo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.

Amesema tetemeko hilo limesababisha Serikali kuzifunga shule zake mbili za sekondari za Nyakato na Ihungo kati ya nne zilizoathirika vibaya na  tetemeko hilo.

“Serikali itajitahidi kuhakikisha inarejesha miundombini iliyoharibiwa na tetemeko hilo katika kipindi kifupi ili wanafunzi na wananchi wengine waweze kuendelea na shughuli zao za kawaida,” amesema.

Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka tayari Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri MkuuSera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Muhagama yuko mkoani Kagera akiongoza kitengo cha maafa kufanya thamnili kujua athari zilizosababishwa na tetemeko hilo.

Mawaziri wengine walioko mkoani Kagera wakiendelea kufanya tathmini hiyo ni pamoja na Waziri waUjenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa  Makame Mbarawa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Amesema Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya mkoa wa Kagera imefungua akaunti maalumu katika benki ya CRDB kwa ajili ya kupokea michango kutoka kwa watu mbalimbali. Namba za akaunti hiyo ya Kamati ya Maafa ya Kagera ni CRDB 0152225617300.  

Pia Waziri Mkuu amewapongeza na kuwashukuru waheshimiwa Wabunge kwa kuamua kutoa posho zao za kikao cha leo kwa ajili ya kuchangia wahanga wa tetemeko hilo na kuwaomba wananchi wengine kujitokeza na kutoa michango yao.

Wakati huo huo viongozi wa makampuni ya mafuta ya GBP, Oil Com na Moil wameahidi kujenga shule mbili za Nyakato na Ihungo ambazo sehemu kubwa ya miundombinu yake imeharibika vibaya. Shule hizo zitajengwa katika kipindi cha siku 30.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Waziri Mkuu ilihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi, Dk. Aziz Mlima.

 IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
JUMANNE SEPTEMBA  13, 2016  




No comments:

Post a Comment

Pages