HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 27, 2016

'PANYA ROAD' WAIBUKA UPYA NA KUTESA WANANCHI MOSHI BAA JIJINI DAR ES SALAAM

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar. Simon Sirro
Na Dotto Mwaibale

KUNDI la uhalifu la watoto wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 25 maarufu kama panya road linatishia usalama wa wananchi na mali zao maeneo ya Moshi Baa na vitongoji vingine katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Kufuatia kukithiri kwa vitendo hivyo katika kipindi kisichopungua wiki mbili tayari watoto watatu walikuwa wakidaiwa kuhusika na kundi hilo wameuawa na wananchi wenye hasira kali.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaa leo hii mkazi wa eneo la Moshi Baa Relini aliyejitambulisha kwa jina  la Mwarami Abubakar alisema hali sio shwari katika eneo kufuatia matukio ya kila siku ya kuvamiwa wananchi kujeruhiwa na kuporwa mali zao na kundi hilo.

"Tayari vijana wawili wiki iliyopita wamechomwa moto na wananchi wenye hasira  huku mwingine akipigwa juzi hadi kutolewa utumbo na kufariki papo hapo" alisema Abubakar.

Mkazi mwingine wa eneo la Kwa Mkolemba Khamisi Fadhil alisema kundi hilo limekuwa likifanya vitendo hivyo mchana kweupe na wanatembea kuanzia vijana nane hadi 10 wakiwa na silaha za jadi kama nondo, visu na mapanga na mtu yeyote wanayekutana naye ni  lazima wampige na kumpora.

"Wenye maduka wanalazimika kufunga kuanzia saa moja jioni kuhofia kundi hilo ambalo huvunja milango ya nyumba na kufanya uporaji" alisema Fadhil.

Fadhil alisema maeneo ambayo vijana hao wameshamiri ni Moshi Baa Relini, Kwa Mkolemba, Diwani na Bomba mbili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamishna Msaidizi (ACP), Salum Hamdan alisema polisi imejipanga vilivyokukabiliana na vitendo hivyo katika mkoa wake.

"Kwanza napenda kukuambia kwamba hakuna kundi linalojiita panya road wote tuna wahesabu ni wahalifu kama walivyo wahalifu wengine na hivi ninavyongea na wewe tupo katika siku ya sita ya operesheni ya kukakamta watu wanaojihusisha na uhalifu wa ujambazi wakiwemo wanaouza pombe haramu ya gongo " alisema Kamanda Hamdan.

Aliongeza kuwa katika mkoa wake hivi karibuni utakuwa shwari baada ya askari wake kusambaratisha watu hao wanaofanya vitendo hivyo.

No comments:

Post a Comment

Pages