WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi,
Bw. Godfrey Zambi kuhakikisha anadhibiti wafanyabiashara wanaonunua korosho kwa
njia ya magendo na atakayekamatwa achukuliwe hatua.
Pia amewataka wananchi wa mkoa huo kutouza korosho zao kwa
walanguzi maarufu kangomba na badala yake wazipeleke kwenye masoko rasmi ili
waweze kupata tija.
“biashara ya kangomba ni mwiko atakayekamatwa amebeba korosho za
kangomba atachukuliwa hatua za kisheria na chombo chake cha usafiri
kitataifishwa” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Oktoba 17, 2016)
wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa katika
mikutano iliyofanyika kwenye vijiji vya Mibure, Namakuku, Ng’imbwa, Chienjele,
Mkata, Mitope na Kitandi.
“Marufuku kuuza korosho kwa kangomba kwani mnapata hasara kipimo
kinachotumika si rasmi. Mkoa kamateni na taifisheni korosho na chombo cha
usafiri kitakachotumika kubeba korosho za magendo,” amesema.
Amesema ni vema wakulima wakaachana na biashara ya kangomba kwa
sababu haina tija na badala yake wasubiri na kwenda kuuza korosho zao katika
minada kwa bei nzuri.
“Mwaka huu korosho itauzika kwa bei ya juu zaidi isiyopungua
sh.3500, msikubali kuuza korosho mlizizitolea jasho kwa walanguzi wanaotumia
kangomba kwa sh. 1000 huu ni wizi, kwani kile kipimo cha wanachotumia ni sawa
na kilo mbili, hivyo unapoteza zaidi ya sh. 6000”. amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwasisitiza wananchi hao
kuongeza idadi ya mazao ya biashara na kuanza
kulima alizeti ambapo wataweza kupata faida ya zaidi ya sh. milioni moja
kwenye shamba la ukubwa wa
ekari moja.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi ametoa
miezi miwili kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Bw.
Andrea Chezue kuhakikisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mibure unakamilika.
“Ndani ya miezi miwili Zahanati iwe imekamilika, tuache
kuzungumza sasa ni vitendo tu”amesema.
Awali Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kukamua mafuta ya
ufuta na karanga cha Ilulu kilichoko wilayani Nachingwea na kukuta
kimetelekezwa. Ameagiza uongozi wa kiwanda kumpelekea nyaraka zote za umiliki.
Kiwanda hicho kilibinafsishwa kwa marehemu Abbas Gulamali na sasa kinasimamiwa
na familia yake.
“Nawahitaji Dodoma Oktoba 22 waje na nyaraka zao ili nijue
walipokabidhiwa kiwanda hiki walitaka kufanya nini,” alimuagiza Msimamizi wa
Kiwanda hicho Dinna Mavumbi kuwajulisha wahusika.
Waziri Mkuu alisema haiwezekani kiwanda hicho kilichojengwa kwa
fedha za umma kikatelekezwa bila ya kuendelezwa. Alisema baada ya kupitia
nyaraka zao ataangalia namna ya kurudisha majengo hayo ya kiwanda kwa Serikali. “Hatuwezi kuacha raslimali hii ikiwa
imetelekezwa msituni inaharibika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, OKTOBA 17,
2016
No comments:
Post a Comment