Mshtakiwa wa kesi ya
unyang’anyi wa kutumia silaha, Salum
Njwete 'Scorpion' (katikati), akitoka katika Mahakama
ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusomewa upya
shtaka linalomkabili. (Picha na Francis Dande)
NA JABIR JOHNSON
MSHTAKIWA wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha Salum Njwete (34) ‘Scorpion’ amefutiwa shtaka lake la awali na Mahakama ya Wilaya Ilala, jijini Dar es Salaam leo kisha kesi yake kuanza upya.
Hata hivyo kuanza kwa shtaka lake jipya kumeenda sanjari na kubadilishwa hakimu wa kuisikiliza kesi hiyo.
Mwendesha Mashtaka Munde Kalombola mbele ya Hakimu Mkazi Adelf Sachore aliiomba mahakamani kuwa upande wa mashtaka hawezi kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwa mujibu wa kifungu cha Sheria Na. 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Hakimu aliridhia ombi la mwendesha mashtaka kufuta shtaka lililokuwa likimkabili Scorpion.
Shtaka jipya ambalo Scorpion anashtakiwa nalo ni unyang’anyi wa kutumia silaha alilolitenda Septemba 6 mwaka huu Buguruni Shell kisha kumchoma na kisu mlalamikaji Said Ally Mrisho machoni, mabegani na tumboni.
Awali Mwendesha Mashtaka Chesensi Gavyole mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alimpora mlalamikaji ambaye hakuwepo mahakamani hapo vitu vya thamani na fedha taslimu vyote vikiwa na jumla ya Sh. 476,000.
Mshtakiwa alikana kuhusika na kosa hilo.
Hakimu alisema kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria Na. 148(5)(a)(i) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mshtakiwa hawezi kupata dhamana hivyo atarudishwa mahabusu.
Ikumbukwe Septemba 23 mwaka huu, Scorpion alipandishwa mahakamani hapo na kufunguliwa shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha chini ya kifungu cha Sheria Na. 287A cha makosa ya jinai.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Scorpion aliyejipatia umaarufu ‘Mtoboa Macho’ mnamo Septemba 6 mwaka huu maeneo ya Buguruni Shell jijini hapa alimvamia na kumpora mali na fedha taslimu muathirika Said Ally Mrisho kisha kumchoma na kisu katika macho, mabegani na tumboni huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kesi hiyo ilikuwa chini ya Hakimu Mkazi Adelf Sanchore na Mwendesha Mashtaka Munde Kalombola ambao wameisimamia hadi Oktoba 19 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment