Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 29 Oktoba, 2016
amefanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House) kwa lengo la kufuatilia
utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangili inayofanywa na Kikosi Kazi
kilichoundwa na Wizara hiyo.
Akiwa katika ofisi hizo
Rais Magufuli aliyekuwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja
Jenerali Gaudensi Milanzi ameshuhudia pembe 50 za ndovu zilizokamatwa kati ya
jana Ijumaa na leo Jumamosi Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Dkt. Magufuli
ameoneshwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamebeba pembe hizo na watuhumiwa wanane
wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa biashara haramu ya pembe za ndovu.
Rais Magufuli amewapongeza
askari wote waliopo katika Kikosi Kazi cha kudhibiti na kupambana na biashara
haramu ya pembe za ndovu pamoja na Raia wema wote wanaotoa ushirikiano katika
operesheni hiyo na amewahakikishia kuwa anatambua kazi kubwa wanayoifanya na
anawaunga mkono.
“Nawapongeza sana kwa kazi
nzuri mnayoifanya na ninawahakikishia kuwa ninawaunga mkono, chapeni kazi,
wakamateni wote wanaojihusisha na biashara hii haramu, hakuna wa kumbakiza, awe
mkubwa au nani, kamateni, wala msijali cheo chake, umri wake, dini yake, kabila
lake, umaarufu wake, sheria ni msumeno, watafuteni wote mpaka watu wakiona
tembo wawe wanakimbia wenyewe ili tuokoe wanyama wetu ambao wanaendelea
kutekelezwa.
“Hapa mmekamata pembe 50 maana
yake tembo 25 wameuwawa, haiwezekani maliasili yetu ikawa inapotea hovyo hovyo
kwa sababu ya watu wachache wenye tamaa ya kutaka utajiri wa haraka haraka”
amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
29 Oktoba, 2016
No comments:
Post a Comment