HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA TANO WA BUNGE LA JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 11 NOVEMBA, 2016
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kutumia
fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutufikisha salama siku ya
leo tunapohitimisha Mkutano wa Tano wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 1
Novemba, 2016.
2.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukupa
pole, kwa msiba mzito uliotokea tarehe 7 Novemba, 2016 ambao Bunge lako tukufu,
Serikali na Taifa tumepata kwa kumpoteza Mheshimiwa
Samwel Sitta, mmoja wa
Viongozi mahiri wa Bunge hili katika historia ya nchi yetu. Msiba uliotupata wa
aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa (2005-2010) na Mbunge Mstaafu
wa Jimbo la Urambo Mkoani Tabora ni pigo kwa Taifa letu. Nasi Wabunge kwa
kuwawakilisha Watanzania leo hii muda mfupi ujao tutaaga mwili wa kipenzi chetu
Mheshimiwa Samuel Sitta. Tunamwomba Mwenyezi
Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema Peponi. Amina.
3.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa mjane wa marehemu, Mheshimiwa
Margareth Simwanza Sitta, Mbunge mwenzetu, watoto wake na wanafamilia wote na
marafiki wote kwa ujumla kutokana na msiba mzito uliowapata. Tunamuomba
Mwenyezi Mungu awape subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na siku zote
wamtangulize Mwenyezi Mungu katika kuwaongoza wanafamilia waliobakia.
Sina budi kukiri kuwa Taifa
limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo.
Enzi za uhai wake, Marehemu Mheshimiwa Sitta, alibahatika kufanya kazi na
Marais wa awamu zote nne zilizopita tangu ya kwanza ya Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, akiwa Mbunge kwa miaka 30. Alikuwa ni Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na Mkuu wa Mikoa ya
Iringa na Kilimanjaro, Waziri wa Ujenzi, Waziri aliyesimamia Ustawishaji Makao
Makuu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Afrika Mashariki, Waziri wa
Uchukuzi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.
4.
Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Novemba, 2016 tumeondokewa
tena na Kiongozi wa muda mrefu Serikalini Ndugu Joseph Mungai. Kiongozi huyu ameshika nafasi mbalimbali
katika utumishi wa umma ikiwemo Ubunge na Uwaziri.
5.
Mheshimiwa
Spika, tangu tulipokutana mara ya mwisho, pametokea majanga
mbalimbali yakiwemo maradhi, ajali, na matukio mengine ambayo yamesababisha
vifo na majeruhi kwa Watanzania wenzetu. Sote tunakumbuka tukio la kusikitisha
la watumishi wa Serikali waliopoteza maisha wakiwa
kazini walipovamiwa na wanakijiji wa Makang’wa wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Nalaani mauaji hayo na kuvitaka vyombo vya usalama kuwachukulia hatua wote
waliohusika. Vilevile, katika miezi ya Oktoba na Novemba, kumetokea
ajali za barabarani katika Mikoa ya Mbeya, Pwani, Singida, Lindi, Iringa, na
ile iliyopoteza ndugu zetu 19 mkoani Shinyanga na kwingineko ambako ndugu zetu
walipoteza maisha. Ninatoa
pole kwa wafiwa wote na wale wote waliopatwa na majanga kutokana na matukio
hayo. Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha na waliopo hospitali. Pia niendelee kuwataka Askari wa usalama
barabarani kuhakikisha wanasimamia madereva na watumiaji wa Barabara kuzingatia
Sheria za usalama wa barabarani.
6.
Mheshimiwa Spika, leo tunahitimisha Mkutano
huu wa Tano tukiwa tumekamilisha shughuli zote zilizopangwa. Naomba nitumie fursa hii
kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa
Wenyeviti wa Bunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote kwa
ufanisi mkubwa. Nawapongeza sana!
SHUGHULI ZA BUNGE
7.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu tumepata fursa
ya kujadili, kupokea na kushauri kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa
Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na muongozo wa kuandaa Mpango
na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, katika kipindi hiki,
tumejadili Hoja mbalimbali za Serikali ikiwemo Miswada, Taarifa za Kamati,
Mkataba wa EPA, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Vilevile, Wabunge
walipata majibu ya maswali mbalimbali ya msingi na ya nyongeza yaliyoulizwa na
Waheshimiwa Wabunge na maswali ya Papo kwa Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
8.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Wataalam wake, kwa kazi kubwa ya
kuandaa miswada mbalimbali iliyowasilishwa katika Bunge lako Tukufu. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Serikali itazingatia ushauri na
maoni yenu wakati wa utekelezaji.
MAAZIMIO
9.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge wamepata fursa ya kupokea na kujadili Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Umoja wa Ulaya yaani East Africa
Community – European Union Economic Partnership Agreement. Napenda
kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu mizuri tuliyoipata
wakati wa mjadala wa Mkataba huo. Serikali
itafanyia kazi maoni, ushauri na uamuzi wenu kuhusu Mkataba huo.
JUHUDI ZA SERIKALI ZA
KUWAHUDUMIA WAATHIRIKA WA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA
10. Mheshimiwa Spika, mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 10 Septemba, 2016 lilitokea tetemeko la
ardhi katika eneo la Kanda ya Ziwa na hususan Mkoa wa Kagera. Tetemeko hilo
lilisababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa makazi na
miundombinu ya umma na watu binafsi. Jumla ya Watu 117,721 wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za
kisaikolojia katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa.
Aidha, jumla ya watu 17 walipoteza
maisha na 560 walijeruhiwa.
Vilevile, nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na nyumba 14,595 za makazi
zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa kubwa na hivyo kuzifanya kuwa
hatarishi kwa makazi ya binadamu. Vilevile, maafa haya yalisababisha uharibifu
wa miundombinu ya barabara na majengo ya Serikali 1,718 yaliyoharibika kwa
viwango tofauti.
11. Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, Serikali ilianzisha Kituo cha Operesheni na Kuratibu Maafa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Kagera kwa lengo la kuharakisha huduma. Aidha, Serikali ilitoa matibabu bure
kwa majeruhi wote, kuandaa na kugharamia mazishi ya watu 17 waliofariki ambapo mimi
binafsi nilihudhuria na pia kutoa mkono wa pole wa Shilingi Milioni 17 kwa
wafiwa. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali
iliwahudumia wananchi walioathirika na tetemeko kwa kuwapatia misaada ya
kibinadamu ikiwemo chakula, madawa, nguo, makazi ya muda, vifaa vya ujenzi,
vifaa tiba, vifaa vya shule na huduma ya ushauri wa kisaikolojia. Aidha,
Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na
wadau mbalimbali walifanya Tathmini ya pamoja ya mahitaji ya haraka katika
kukabiliana na Athari za Tetemeko hilo. Ambapo utekelezaji wa masuala muhimu
yaliyoainishwa katika tathmini hiyo unaendelea.
12. Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha wadau, taasisi na wananchi
mbalimbali kuchangia maafa hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Kagera
ilifungua Akaunti pekee Namba
0152225617300 katika Benki ya CRDB Bukoba yenye jina
la “KAMATI MAAFA KAGERA”. Hadi
kufikia tarehe 10 Novemba, 2016
kiasi cha Shilingi 5,427,671,677.32 kilikuwa
kimeingizwa kwenye Akaunti hiyo. Hadi kufikia tarehe 10 Novemba 2016 Salio
katika Benki ni Shilingi 4,296,038,711.79 na matumizi hadi tarehe tajwa yalikuwa
ni Shilingi 1,130,428,347.53. Aidha, Kamati pia ilisajili namba za simu za
mkononi za kupokea michango katika Kampuni za Vodacom (M-Pesa) 0768 196 669, Tigo (Tigopesa)
0718 069 616 na Airtel (Airtel
Money) 0682 950 009 kwa jina la “KAMATI
MAAFA KAGERA”. Hadi kufikia tarehe 10
Novemba, 2016, kiasi cha Shilingi
16,638,747 kilichangwa kupitia
mitandao hiyo ya simu. Hivyo kufanya jumla ya fedha zilizopokelewa kupitia
Benki na Mitandao ya Simu kuwa Shilingi 5,444,310,424.32.
Aidha, Serikali imechangia Shilingi
Billioni Moja katika kukabili janga hilo.
13. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupokea misaada
kutoka kwa Washirika wetu wa Maendeleo, Balozi na hata Nchi marafiki. Mathalan,
tumepokea kutoka Serikali ya Uganda Dola
za Kimarekani 200,000 sawa na Shilingi
Milioni 419.2, Serikali ya India Shilingi
Milioni 547, Serikali ya Kuwait Shilingi
Milioni 51 na Serikali ya Uingereza iliahidi kutoa Shilingi Bilioni Sita zitakazoelekezwa kwenye ujenzi wa shule.
14. Mheshimiwa Spika, tumepokea vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni
357 yakiwemo maturubai, magodoro, ndoo, mashuka, vifaa tiba, dawa na chakula kutoka Serikali za Japan, China,
Kenya, Pakistan, Burundi na Rwanda.
15. Mheshimiwa Spika, taarifa ya Kikosi Kazi cha Wataalam imeainisha kuwa
takribani Shilingi Bilioni 63.2 zitahitajika
kurejesha hali ya kawaida katika Mkoa wa Kagera kufuatia maafa hayo. Gharama
hii inajumuisha ukarabati wa shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na
taasisi nyingine katika wilaya zote sita za Mkoa huo, ujenzi mpya wa shule za
Ihungo na Nyakato (tayari wafadhili wamejitolea kujenga shule hizi). Aidha, hadi
kufikia tarehe 10 Novemba, 2016
kiasi cha Shilingi 966,898,826 zilitumika katika kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa Shule za Msingi na
Sekondari pamoja na Zahanati katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera. Serikali inaendelea
na ujenzi wa Zahanati mpya (Ishozi) inayojumuisha chumba cha Upasuaji na wodi
ya kinamama na watoto na usimamizi wa ujenzi wa shule za Ihungo na
Nyakato. Aidha, katika kuongeza nguvu ya
urejeshaji hali jumla ya Askari 96 wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakiwemo Wahandisi, Mafundi, Wapishi, na Madereva
waliwasili Mkoani Kagera tarehe 19 Oktoba, 2016 kushiriki katika zoezi
la kurejesha hali ya majengo na miundombinu.
16.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda
kulihakikishia Bunge lako Tukufu na wananchi kwa jumla kuwa Serikali ipo pamoja
na waathirika hawa katika suala hili na ina mikakati madhubuti ya kuhakikisha
tunarejesha hali bora kwa kuendelea kurudisha miundombinu, kutoa huduma za kibinadamu na matibabu
kwa waathirika. Aidha, napenda kuwashukuru wale wote waliochangia katika
kusaidia wenzetu wa Kagera, kwani katika kipindi hiki, tumeonesha umoja wetu,
upendo wa dhati, hali ya kuthaminiana na kujaliana. Mungu awabariki sana na
kuwaongezea pale walipotoa. Kipekee, niwashukuru Nchi marafiki, Balozi, Wadau
wa Maendeleo wa ndani na nje ya Nchi, Taasisi za Kiserikali na zisizo za
Kiserikali, Taasisi za Fedha, Kampuni, Vikundi mbalimbali, pamoja na Wananchi
wote wakiwemo wale waishio nje ya Nchi.
MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2017/2018
17.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu wa tano wa Bunge, Serikali
imewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018.
Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao
mizuri iliyotolewa wakati wa kujadili Hoja hiyo. Maoni na ushauri uliotolewa
utazingatiwa wakati wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha wa
2017/2018.
TAARIFA ZA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE ZA PAC NA LAAC KUHUSU HESABU
ZILIZOKAGULIWA KWA MWAKA 2013/2014 NA 2014/2015
18.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya
kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Taarifa
za Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC kuhusu Hesabu za Serikali Kuu,
Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia
tarehe 30 Juni, 2014 na tarehe 30 Juni, 2015.
Serikali imepokea michango na Hoja za Waheshimiwa Wabunge na itazifanyia
kazi.
19.
Mheshimiwa
Spika, napenda kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2015 hadi 2016, Serikali imetakiwa kuchukua hatua kali na za haraka
kwa wale wote watakaobainika kujihusisha na ubadhirifu
na wizi wa mali ya umma, ukiukaji wa maadili ya Utumishi wa Umma na wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Umma. Kutokana na maelekezo hayo, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali na kuchukua hatua kwa Watumishi wa Umma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za matumizi ya Fedha za Umma. Maafisa Masuuli wote wanakumbushwa kuzingatia kikamilifu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake. Aidha, Maafisa Masuuli wote wanatakiwa kuchukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria kwa Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Serikali wanaofanya malipo yenye mashaka wakati wa kufanya manunuzi ya Umma au kuingia Mikataba na Zabuni tata za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hatua hizo zitapunguza na kuondoa Hoja za ukaguzi na kuimarisha usimamizi wa fedha za walipa kodi.
na wizi wa mali ya umma, ukiukaji wa maadili ya Utumishi wa Umma na wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Umma. Kutokana na maelekezo hayo, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali na kuchukua hatua kwa Watumishi wa Umma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za matumizi ya Fedha za Umma. Maafisa Masuuli wote wanakumbushwa kuzingatia kikamilifu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake. Aidha, Maafisa Masuuli wote wanatakiwa kuchukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria kwa Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Serikali wanaofanya malipo yenye mashaka wakati wa kufanya manunuzi ya Umma au kuingia Mikataba na Zabuni tata za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hatua hizo zitapunguza na kuondoa Hoja za ukaguzi na kuimarisha usimamizi wa fedha za walipa kodi.
SEKTA YA KILIMO
Mwenendo wa Uzalishaji wa Mazao Katika Msimu wa Mvua za Vuli
20.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa
kutoka Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa, kwa kipindi cha Oktoba hadi
Desemba 2016 imeonesha kuwa katika maeneo mengi ya nchi, mvua zinatarajiwa kuwa
chache, kuchelewa kuanza na mahali pengine kunyesha kwa mtawanyiko
usioridhisha. Aidha, kwa maeneo yanayopata mvua za vuli zikiwemo Wilaya za
Kyerwa, Missenyi na Karagwe, mvua zilipoanza kunyesha zilikuwa chini ya wastani
na kusababisha baadhi ya mazao yaliyopandwa kuathirika. Vile vile, taarifa za
Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA zinaeleza kuwa katika maeneo yanayopata msimu mmoja
wa mvua zinazoanza mwezi Novemba hadi Aprili, mvua zitachelewa na kunyesha
chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi isipokuwa katika baadhi ya
maeneo ya Mtwara Lindi na Ruvuma. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwataka
wataalam wa kilimo kuhakikisha wananchi katika maeneo yatakayopata mvua kidogo
wanawezeshwa kupata mbegu za mazao yanayostahimili ukame na zinazokomaa haraka.
Aidha, niwashauri wakulima kuandaa mashamba yao mapema na kutumia mbegu
hizo zinazokomaa mapema na kustahimili ukame. Niwasihi wananchi na wakulima
kuendelea kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula walichovuna au
kununua kwa matumizi katika kaya zao. Nitoe wito kwa Sekta binafsi kuendelea
kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye
ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.
Usambazaji wa Pembejeo za Zao laTumbaku
21.
Mheshimiwa Spika, ili kuondoa kero ya
upatikanaji wa pembejeo kwa zao la tumbaku kwa msimu wa 2016/2017, Serikali
imebadili utaratibu kutoka ule uliohusisha zabuni kwa wauzaji wa kati
(middlemen) na kuweka utaratibu mpya unaohusisha wazalishaji wa pembejeo
kuzisafirisha pembejeo hizo hadi katika Vyama vya Msingi vya Ushirika moja kwa
moja kwa bei ya Dola za Kimarekani 40.45
kwa mfuko wa NPK (ikilinganishwa na Dola za Kimarekani 52.7 za msimu uliopita), na Dola
za Kimarekani 21 pungufu kwa mbolea aina ya Urea na CAN kwa tani moja
ukilinganisha uliopita. Hadi sasa wazalishaji wawili wa mbolea za tumbaku
(Kampuni ya Yara Tanzania na Rosier) wamechukua jukumu hilo. Napenda kuchukua
fursa hii kuvitaka Vyama vya Ushirika kusimamia kikamilifu mpango huu ili
wakulima wazalishe kitaalamu na kuongeza tija katika uzalishaji.
SEKTA YA VIWANDA NA
UWEKEZAJI
22.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe
17 Oktoba, 2016, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji alizindua
rasmi matokeo ya Sensa ya Uzalishaji Viwandani ya mwaka 2013 iliyofanyika kwa
ushirikiano wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS). Zoezi la sensa hii lilitumia taarifa za uzalishaji za viwanda za
mwaka, 2013, yaani viwanda vilivyokuwepo mwaka 2013 na vilivyokuwa vinazalisha. Zoezi la
ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji, za viwanda lilifanyika mwaka 2014 na mwaka
2015 ilikuwa ni kufanya uchambuzi wa kitalaamu na kuandika ripoti.
23.
Mheshimiwa
Spika, matokeo ya Sensa hiyo yanaonesha kuwa, kufikia mwaka
2013 Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda 49,243 ambapo viwanda vidogo vinavyoajiri mtu 1 – 4 vilikuwa ni Asilimia 85.13, viwanda vidogo vyenye watu 5 -
49 ni Asilimia
14.02,
viwanda vya kati vyenye watu 50 - 99 ni Asilimia 0.35 na
viwanda vikubwa vyenye watu kuanzia 100 na kuendelea ni Asilimia 0.5. Hivyo, Asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo.
24.
Mheshimiwa
Spika, katika
utafiti wa mwaka jana ilionekana kuwa mpaka mwezi Oktoba, 2015 kulikuwa na
viwanda 52,579. Aidha, kwa kipindi cha mwaka mmoja tu, yaani kuanzia Novemba,
2015 mpaka Oktoba, 2016 jumla ya viwanda vipya 1,843 vimeanzishwa na
kufanya jumla ya viwanda vyote nchini kufikia 54,422. Ni matumaini ya
Serikali kuwa kutokana na juhudi za uhamasishaji zinazofanyika, kasi ya
uanzishwaji viwanda na hasa viwanda vidogo na vya kati na vikubwa itaongezeka
sana.
25.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara mbalimbali za
Kisekta tayari imebainisha maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchochea uwekezaji kama vile kuendeleza eneo
la Mji wa Kigamboni na kutenga maeneo maalum ya Uwekezaji katika Mikoa
mbalimbali Nchini. Hatua nyingine ni
kuboresha miundombinu
kama vile barabara na reli. Mfano mzuri ni ujenzi wa reli yenye urefu wa
kilomita 4 katika kiwanda kipya cha KILUA GROUP cha kutengeneza nondo kilichopo
Mlandizi, Pwani. Pia, Serikali
inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme
wa uhakika. Kwa viwanda ambavyo vipo karibu na bomba la gesi watasaidiwa
kuunganishwa na gesi. Vilevile, Serikali, imechukua hatua madhubuti za
kuharakisha upatikanaji wa ardhi ambacho ni kivutio muhimu katika kuhamasisha
uwekezaji.
Uongezaji Kasi ya Uwekezaji kwenye
Sekta ya Viwanda Nchini
26.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeweka
mikakati madhubuti ya kuhakikisha kasi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda
inaongezeka ili ichangie Asilimia 15 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2020 Ili
kutekeleza adhima hiyo hatua zifuatazo zinaendelea kuchukuliwa:-
Kwanza: Kutambua sekta za kipaumbele kwa kuzingatia
viwanda vinavyotumia malighafi za ndani,
na hususan kwenye sekta za kilimo na maliasili ili kuchochea uzalishaji vijiini
na kuongeza ajira; viwanda vinavyotumia malighafi za ndani ambazo si za kilimo
kama vile madini na kemikali; na kuweka msukumo kwenye kuanzisha viwanda
visivyotumia malighafi za ndani kama vile uunganishaji wa magari na uzalishaji
wa vifungashio.
Pili: Kuandaa Mpango mahsusi wa uwekezaji kwenye viwanda
kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mpaka sasa, Mifuko ya LAPF, PPF, PSPF, NSSF
na GEPF tayari wameainisha miradi ya uzalishaji watakayoanza nayo.
Tatu: Kuhamasisha
Sekta Binafsi, ya ndani na nje ya Nchi, kuwekeza kwenye viwanda. Kupitia
makongamano ya biashara na uwekezaji nchi mbali mbali zimehamasishwa kuwekeza
nchini. Baadhi ya nchi hizo ni China, Oman, Vietnman, Urusi, Morocco n.k.
Nne: Kuingia
makubaliano ya ushirikiano na Nchi zingine ili kuongeza uwekezaji. Mpaka sasa Nchi
ya China imechagua jimbo la Jiangsu kuleta viwanda nchini na pia kupitia Jukwaa la Ushirkiano la China na
Afrika itawezesha ujenzi wa miundombinu ikiwemo Bandari ya Bagamoyo. Aidha, kwa
utaratibu huu Serikali tayari imeanza utekelezaji wa mradi wa kuunganisha
matrekta 2400 pale TAMCO Kibaha kufuatia ushirikiano na Serikali ya Poland,
uunganishaji wa magari wa Kampuni ya Kitanzania ya SIMBA MOTOR kwa ushirikiano
na Jeshi (NYUMBU) na Kampuni ya China. Vile vile, India kupitia mradi wake wa
kuimarisha uwekezaji Afrika (SITA) inasaidia utekelezaji wa mikakati minne ya kukuza
na kuendeleza alizeti, pamba, ngozi na mazao ya jamii ya kunde.
Tano: Kutoa elimu na mwongozo kwa Serikali ngazi ya Mikoa na Wilaya
kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika maeneo yao. Serikali imegawa Mikoa
katika makundi manane ambayo Watendaji Waandamizi wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji watakwenda kuzungumza na wadau ili kuhakikisha viwanda
vinasambaa Nchi nzima.
27.
Mheshimiwa
Spika, katika kutekeleza jukumu hili mambo muhimu ambayo Mikoa
inatakiwa kuzingatia ni pamoja na Mikoa kuweza kubaini fursa walizonazo na kuandaa taswira ya mkoa
kutegemeana na fursa walizonazo. Aidha,
Mikoa inahimizwa kuhamasisha wananchi juu ya uwekezaji. Vilevile, Viongozi wa
Mkoa wanashauriwa kuongeza kasi ya kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa
kutenga maeneo na kuhakikisha kuwa wanazingatia katika mipango ya Halmashauri za wilaya
ujenzi wa miundombinu wezeshi kwenye
maeneo watakayotenga kwa ajili ya uwekezaji.
SEKTA YA ELIMU
Matokeo ya Mitihani ya Darasa
la Saba 2016
28.
Mheshimiwa
Spika, mwezi Oktoba, 2016 Baraza la Mitihani la Taifa
lilitangaza matokeo ya Mitihani wa Darasa la Saba kwa mwaka 2016. Taarifa hiyo
ilibainisha kuwa katika mtihani huo, kati ya wanafunzi 789,479 waliofanya mtihani, jumla ya wanafunzi 555,291 walifaulu sawa na Asilimia 70.36. Kati yao wasichana ni 283,751
na wavulana ni 271,540. Nitumie
fursa hii kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu na Shule zote zilizofanya
vizuri na hasa wale kumi bora. Napenda kuwaagiza Viongozi wa Mikoa na Halmashauri
kuendelea kukamilisha miundombinu ya vyumba vya madarasa na miundo-mbinu
mingine ili kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na
kidato cha kwanza mwezi Januari, 2017. Kila Mkoa uweke lengo la kuhakikisha
Wanafunzi wote watakaochaguliwa wanajiunga na Sekondari. Serikali kwa upande wake itahakikisha inatoa
ruzuku kwa ajili ya mahitaji ya Wanafunzi watakaojiunga na Sekondari.
Mwenendo wa
utoaji wa mikopo
29.
Mheshimiwa Spika, tangu
mwaka 1994 Serikali ilipoanza kutoa
mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, jumla ya kiasi cha Shilingi Trilioni 2.44 kimekwishatolewa. Jumla ya wanafunzi 324,994 wamenufaika na fedha hizo.
30.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2016/2017 jumla ya wanafunzi 64,441 wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu na orodha yao
kuwasilishwa Bodi ya Mikopo ya Elimu Juu. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia tarehe 3 Novemba, 2016, wakati akitoa kauli ya Serikali Bungeni
kuhusu upangaji na utoaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu, ni kwamba hadi kufikia
tarehe 2 Novemba, 2016 jumla ya
wanafunzi 25,228 wa
mwaka wa kwanza walikuwa wamekwishapewa fedha za mikopo. Kati ya wanafunzi hao,
4,787 ni Yatima, 127 wenye Ulemavu na 94 ni waliosoma Sekondari kwa Ufadhili
wa Taasisi mbalimbali.
31.
Mheshimiwa
Spika, napenda kusisitiza kuwa wanafunzi wote wanaoendelea na
masomo, ambao ni wanufaika wa mikopo na vyuo vyao vimewasilisha Bodi ya Mikopo
taarifa za matokeo wameendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa katika mwaka
uliopita wa masomo.
Changamoto Zilizopo za Mkopo na
Utatuzi Wake
32.
Mheshimiwa
Spika, ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika uratibu wa
mikopo ya wanafunzi, Serikali inafanya
mapitio ya mfumo wa udahili wa wanafunzi vyuoni, utaratibu mzima wa utoaji na
urejeshwaji mikopo kwa lengo la kuwa na mfumo bora zaidi na kuondoa adha
inayowapata wanafunzi wanapofungua vyuo kutokana na mfumo uliopo sasa. Nimeagiza
kazi hii ikamilike mapema ili mapendekezo ya mfumo utakaokuwa na tija zaidi
yaweze kuzingatiwa wakati wa maandalizi ya Bajeti ya 2017/2018.
SEKTA
YA ARDHI
Hali ya Migogoro baina ya Watumiaji wa
Ardhi Nchini:
33.
Mheshimiwa
Spika, nchi yetu imeendelea kukumbwa na migogoro mbalimbali ya
ardhi baina ya watumiaji wa ardhi ikiwemo migogoro mikubwa baina ya wakulima na
wafugaji; migororo baina ya wananchi na wawekezaji; wafugaji na hifadhi za
Taifa na baina ya wakulima na baadhi ya maeneo ya hifadhi za Wilaya mbalimbali.
Juhudi na Mikakati ya Serikali ya Kuondoa Migogoro Mikubwa ya Wakulima na
Wafugaji
34.
Mheshimiwa
Spika, migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya Wakulima na
Wafugaji imeendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na mifugo, na vijiji
kutokuwa na Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi inayoainisha maeneo mahsusi kwa ajili ya
Kilimo na Ufugaji. Aidha, uwepo wa mabadiliko ya tabia
nchi yanayosababisha ukame na ukosefu wa malisho na maji katika maeneo ya
wafugaji kumesababisha uhusiano hafifu baina ya jamii za wafugaji na wakulima
kutokana na mifugo kuingizwa katika mashamba ya wakulima kwa mabavu.
35.
Mheshimiwa
Spika, migogoro hii imesababisha kuwepo kwa vitendo vingi vya
uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha ya wananchi, baadhi ya wananchi kupata
vilema vya maisha, uharibifu wa mali, uharibifu wa mazingira, athari za kijamii
kama watoto kushindwa kwenda shule na wananchi kushindwa kushiriki katika
shughuli za maendeleo kutokana na hofu jambo linaloweza kusababisha njaa na
umaskini miongoni mwa jamii na Taifa.
Hatua za kutatua migogoro mikubwa ya
wakulima na wafugaji
36.
Mheshimiwa
Spika, ili kukabiliana na migogoro na kuwawezesha wakulima na
wafugaji kuendelea na shughuli zao bila migogoro, Serikali inaendelea
kutekeleza mikakati ya kuainisha, kupima, kutenga na kumilikisha ardhi kwa
ajili ya wafugaji na wakulima; na kanda za malisho kwa wafugaji wakubwa na
wadogo itakayohusisha vijiji, Wilaya na Mikoa. Maeneo haya yatakayotengwa
yatalindwa kwa kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali, na matumizi yake
yatasimamiwa ili kuhakikisha wanafuga kwa kuzingatia uwiano wa malisho na
mifugo.
37.
Mheshimiwa
Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuzigawanya Ranchi zilizopo
katika vitalu ili wafugaji wenye ng’ombe zaidi ya 200 wahamie huko, kila kitalu
kimoja kulingana na uwezo wa kitaalamu wa kulisha idadi maalum ya ng’ombe. Wafugaji
wenye mifugo chini ya 200 watagawiwa maeneo katika maeneo yaliyotengwa kwa
ajili yao katika vijiji na watakuwa wanauza mifugo yao katika minada ambapo
wafugaji kutoka Ili katika ranchi watafika kununua mifugo hapo. Kwa mikoa
ambayo haina Ranchi za Taifa, watatenga maeneo yaliyo wazi kwa ajili ya
wafugaji wakubwa.
38.
Mheshimiwa
Spika, ili kuzuia wafugaji kuhamahama kutafuta maji na huduma
nyingine, Serikali kwa kushirikiana na wafugaji itaweka miundombinu ya majosho,
mabwawa ya kunyweshea maji, huduma za ugani zikiwemo matibabu, elimu ya kulima
malisho, unenepeshaji, uwekaji sahihi wa chapa za ng’ombe n.k.
39.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na hatua hizo, jawabu la kudumu la migogoro hii
ni kuhakikisha kuwa tunawawezesha wafugaji kuvuna na kupunguza mifugo bila
kupata hasara, kupitia uwekezaji wa Viwanda vya Kuchakata Nyama na Usindikaji
Maziwa ili kuongeza thamani. Wizara husika zikae pamoja na kubuni Mikakati na
Mipango ya kuvutia wawekezaji katika eneo hili katika miaka mitatu ijayo kuwe
na tofauti.
40.
Mheshimiwa
Spika, aidha napenda kuzikumbusha Halmashauri za Wilaya kote
nchini kuendelea kuweka na kutekeleza mipango madhubuti ya matumizi bora ya
ardhi, na wale wenye Benki ya Ardhi wagawe kwa busara kwa wafugaji, wazuie
wafugaji wengine wasiendelee kuingiza mifugo katika maeneo ya kilimo na watumie
sheria ndogo zilizopo na kama hazipo ziandaliwe na kutumiwa; na ikibidi wahalifu
wapelekwe mahakamani. Aidha, niwakumbushe wafugaji wote kufuata sheria na
kwamba Serikali haitasita kuwachukulia hatua wafugaji watakaoingiza mifugo yao
katika mashamba ya wakulima kwa makusudi.
SEKTA
YA NISHATI
Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme
Vijijini Awamu ya Pili
41.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa nishati ya umeme, Serikali
imeendelea kutoa mkazo katika kutekeleza na miradi mikubwa ya uzalishaji na
usafirishaji umeme pamoja na miradi ya kusambaza umeme vijijini. Ili
kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi
wengi, hususan waishio vijijini, Serikali kupitia REA imeendelea kutekeleza Mradi
Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya
Pili tangu mwaka 2014. Mradi huu unatekelezwa katika wilaya zote za Tanzania
Bara. Hadi kufikia Oktoba, 2016 ujenzi wa kilometa za njia ya msongo wa
Kilovolti (kV) 33 umefikia Asilimia 95.6; ujenzi wa kilometa za njia ya
Msongo wa Volti 400 umefikia Asilimia 89.3; na ufungaji wa
transfoma umefikia Asilimia 87.2. Aidha, jumla ya wateja 146,311 wa
awali sawa na Asilimia 59 ya lengo la wateja 255,000
wameunganishiwa umeme kupitia mradi huo.
Mradi
Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
42.
Mheshimiwa
Spika, Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 katika
vijiji 7,873 vya wilaya zote za
Tanzania Bara. Takriban vijiji 7,697
vitapelekewa umeme wa gridi ya Taifa na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi (Off-grid).
Mpango huu utaongeza wigo wa usambazaji umeme katika maeneo ambayo hayakufikiwa
na miradi ya REA Turnkey Phase I na II. Ili kutekeleza miradi hiyo kwa kasi
zaidi, Serikali ya Awamu ya Tano katika bajeti yake ya mwaka 2016/17 iliongeza
fedha za kupeleka umeme Vijijini kutoka Shilingi
Bilioni 357.117
zilizotengwa mwaka 2015/16 hadi Shilingi
Bilioni 587.61 mwaka 2016/17. Hadi kufikia mwezi Oktoba, Serikali imetoa
jumla ya Shilingi Bilioni 109.8 kwa
ajili ya Mfuko wa Nishati Vijijini kutoka kwenye vyanzo vya fedha za
ndani. Kati ya fedha hizo Shilingi
Bilioni 100.4 ni tozo ya mafuta na Shilingi Bilioni 9.4 ni tozo ya umeme.
43.
Mheshimiwa
Spika, zabuni za kupata wakandarasi wa kutekeleza mradi huu
zilitangazwa tarehe 1 Agosti, 2016. Kwa sasa REA inaendelea na uchambuzi wa
zabuni hizo. Taratibu zote za mradi huo zimepangwa kukamilika mwezi Januari,
2017. Natoa rai kwa viongozi mbalimbali wa Serikali wakimemo Waheshimiwa
Wabunge kuwahamisha wananchi katika maeneo yao kutumia fursa ya kuunganishiwa
umeme wakati wakandarasi wakiwa kwenye maeneo ya miradi. Katika kipindi hicho
bei ya kuunganisha umeme ni Shilingi
27,000 tu kama ilivyotaarifiwa awali katika Bunge hili.
44.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia
imeanzisha Mradi wa Kupanua Wigo wa Upatikanaji wa Umeme Vijijini (Tanzania Rural Electricity Expansion Project).
Mradi huo utagharamiwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia wa Dola za Kimarekani
milioni 209. Mradi ulizinduliwa tarehe 26 Agosti 2016, katika kijiji cha
Kwedikwazu wilayani Handeni Mkoani Tanga na utawezesha kaya takriban 500,000
kupata huduma ya umeme nchini.
SEKTA YA MADINI
Migodi Mikubwa Kuendelea Kulipa
Mrabaha
45.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha kati ya Oktoba,
2015 na Oktoba, 2016 Serikali ilifanya ukaguzi na kuwezesha migodi mikubwa kulipa mrabaha ambapo: Migodi Mikubwa
ya Dhahabu ya Biharamulo, Bulyanhulu, Buzwagi, Geita, New Luika na North Mara
imelipa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni
69.4 ikiwa ni Mrabaha, sawa na Shilingi Bilioni 151.4. Vilevile, Mgodi wa
Makaa ya Mawe wa Ngaka umelipa kiasi cha Dola
za Kimarekani 309,836 na Shilingi Milioni 676 ikiwa ni mrabaha. Aidha,
Mgodi wa TanzaniteOne umelipa mrabaha
wa Dola za Kimarekani 189,731 sawa na
Shilingi Milioni 414.
Kuhamasisha Masoko ya Madini ya Vito Nchini
46.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliandaa mnada wa madini ya vito, hususan
tanzanite uliofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 12 Agosti, 2016 Jijini Arusha.
Katika mnada huo madini yenye thamani ya Dola
za Kimarekani 3,448,050, sawa na Shilingi
Bilioni 7.56, yaliuzwa na kuwezesha Serikali kukusanya Dola za Kimarekani 150,491.06, sawa na Shilingi Milioni 331 ikiwa ni mrabaha kutokana na madini
yaliyouzwa.
47.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia Sekta za Nishati na Madini
ili ziweze kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo ya
Taifa letu.
TAARIFA YA MAKUSANYO YA FEDHA
KWENYE HALMASHAURI KWA MWAKA 2016/2017
48.
Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017
Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya mapato ya Shilingi Bilioni 665.4.
Hadi kufikia Septemba, 2016 Halmashauri zimekusanya Shilingi Bilioni 114.46,
sawa na Asilimia 17.2 ya makisio. Kiwango hiki cha ukusanyaji wa mapato katika
Halmashauri bado hakiridhishi. Hivyo, naomba nitumie fursa hii kuhimiza
Halmashauri zote nchini kuongeza jitihada katika kukusanya mapato ya vyanzo vya
ndani. Nazihimiza Halmashauri kutumia
mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji mapato na pia katika maeneo ya
kutolea huduma za afya ili kudhibiti upotevu wa mapato. Aidha, naelekeza
Mamlaka za Serikali za Mitaa waimarishe mifumo ya udhibiti wa ndani na
kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana katika kila huduma au bidhaa
inayonunuliwa na Halmashauri. Halmashauri hazina budi kuepuka matumizi ya fedha
yasiyo na tija katika shughuli za uendeshaji wa Mamlaka hizo.
49.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinaagizwa zifuatilie
kwa karibu mapato na matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye shule na kwenye
vituo vinavyotoa huduma za afya ikiwemo Hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Ili kufikia azma hiyo, uwekwe utaratibu madhubuti wa ukaguzi wa mapato na
matumizi ya fedha hizo kwa kushirikisha Wakaguzi wa ndani wa Halmashauri.
MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU TAARIFA
YA KAMATI YA BUNGE YA LAAC
50.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ushauri mzuri na
mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya LAAC kuhusu ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na 2014/2015, Serikali
imeshatoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa
zinatekeleza kwa ukamilifu maelekezo yote ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati nyingine ili kuondoa hoja zilizojitokeza
katika taarifa ya CAG. Aidha, Halmashauri zinaelekezwa kuimarisha mifumo ya
uthibiti wa ndani na kutumia vizuri ushauri unaotolewa na Kamati za Ukaguzi ili
kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
51.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwamba Halmashauri zote ni lazima zitekeleze
vipaumbele vilivyoidhinishwa katika mpango na bajeti kwa mwaka 2016/17 kwa
kupanga vema utekelezaji kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha. Halmashauri
ziendelee kuimarisha usimamizi wa mikataba ili thamani ya fedha za Serikali
iweze kupatikana katika miradi na Kandarasi nyingine zilizoingia Mikataba na Halmashauri.
HITIMISHO
52.
Mheshimiwa
Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo, napenda nitumie
nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote
wa Bunge kwa kusimamia vizuri na kwa weledi mkubwa vikao vyote vya mkutano huu.
Niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu. Ninashukuru pia
Watendaji wa Serikali kwa kuwasaidia Mawaziri na Naibu Mawaziri katika kujibu
maswali na hoja mbalimbali za Wabunge. Niwashukuru wanausalama wote kwa kazi
yao nzuri. Niwashukuru madereva wote kwa kuwaendesha Mawaziri, Wabunge na
Watendaji wote kwa usalama kabisa. Niwashukuru pia wanahabari wote kwa
kuihabarisha jamii juu ya mkutano wetu. Kipekee, nimshukuru Katibu wa Bunge
Dkt. Thomas Kashililah na timu yake kwa kutuwezesha kukamilisha shughuli zote
za mkutano huu kwa mafanikio makubwa.
53.
Mheshimiwa
Spika, mwisho, lakini si kwa umuhimu, nitumie muda huu kumwomba
Mwenyezi Mungu awalinde na awaongoze Waheshimiwa Wabunge wote katika safari ya
kurejea majumbani kwenu. Aidha,
nawatakia kila la kheri na fanaka katika sikukuu zijazo za mwisho wa mwaka na kuwatakia
mwaka mpya wa 2017.
54.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda
kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 31 Januari, 2017, siku ya Jumanne, saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.
55.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment