HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 10, 2016

Shaaban Idd aeleza siri ya mafanikio yake Azam FC

STRAIKA kinda anayechipukia kwa kasi katika timu ya Azam FC, Shaaban Idd, ameeleza siri ya mafanikio yake ya hivi karibuni, akidai kuwa kitendo cha Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, kumuondolea uoga na kumpa maelekezo bora ndio mambo makuu yanayombeba hivi sasa.

Kinda huyo aliyelelewa kwenye kituo cha Azam FC Academy, jana alifunga mabao mawili muhimu na kutengeneza moja kwenye ushindi mnono wa Azam FC wa mabao 4-1, wakiifunga Mwadui ya Shinyanga, mengine yakifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Francisco Zekumbawira.

Mabao hayo yamemfanya Idd kutimiza mabao matatu msimu aliyoifungia Azam FC baada ya kupandishwa kwenye kikosi cha timu kubwa huku akitoa pasi mbili za mabao, moja akimpa nahodha Bocco kwenye ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Kagera Sugar na nyingine akiitoa jana kwa straika nyota kutoka Zimbabwe, Zekumbawira.

Idd ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mbali na kocha wa timu hiyo kumuondolea uoga, pia maelekezo mazuri anayompa na kumpa uhuru uwanjani nayo yamechangia kubadilika kwa kiwango chake kwenye mechi za hivi karibuni tofauti na mechi za awali mwanzoni mwa msimu.

“Kitu cha kwanza napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuweza kunijalia kuweza kuisaidia timu yangu kuibuka na ushindi wa mabao 4-1, pia napenda kumshukuru kocha wangu kwa kunipatia maelekezo mazuri ya kunifundisha jinsi mpira unavyochezwa na mimi bila kipingamizi nimetendea haki maelekezo yake na kuweza kuisaidia timu yangu kuibuka na ushindi.

“Kwa kweli ninafuraha sana na hii pia ni siku muhimu kwa ajili ya kiongozi wetu mkubwa ambaye amefariki (Mzee Said Mohamed Abeid) hivi majuzi (Jumatatu iliyopita), hivyo ushindi huu una maana nyingi sana kwetu,” alisema.

Kocha ampa uhuru
Idd aliyeibuka mfungaji bora wa michuano ya Azam Youth Cup yaliyofanyika mwaka huu akifunga mabao matano, alisema kuwa katika vitu vilivyomsaidia kubadilika hivi sasa ni kutokana na kocha kumpa zaidi uhuru uwanjani.

“Kocha kanipa nafasi na kanipa uhuru wa kujiamini nisiwe na uoga wowote tofauti na nilivyokuwa nikicheza mwanzo kwani nilikuwa nacheza na uoga, hivyo kocha kaliangalia hilo na kulitambua na hatimaye akanipa nafasi na kuniambia nicheze nisiwe na uoga wowote, nisiogope kitu chochote na nicheze kwa kiwango change,” alisema.

Alisema kwa kuwa ligi ya msimu huu ni ngumu na huu ukiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza, amesema atazidi kupambana na kujitahidi kuweza kuisaidia zaidi timu yake hiyo katika mzunguko wa pili wa ligi unaokuja na michuano mingine pamoja na yeye kujijengea uzoefu.

Mashabiki nao wamuamini
Straika huyo, 18, alichukua fursa hiyo kuwaomba mashabiki wa Azam FC waendelea kumuunga mkono, kumvumilia na kumuamini zaidi kwani bado ana mambo mengi anayotaka kuifanyia Azam FC.

“Mashabiki wasichoke kutuombea dua na kutusapoti katika hii kazi yetu tunawaahidi tutawapa burudani nzuri na timu yetu kuwa katika nafasi nzuri kwenye mzunguko wa pili,” alimalizia kinda huyo.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola ambacho ni mahususi kabisa kwa ajili ya kuchangamsha mwili wako na kuburudisha koo lako pamoja na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikijikusanyia jumla ya pointi 25 ikizidiwa pointi 10 tu na vinara Simba waliojizolea 35.

No comments:

Post a Comment

Pages