HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 24, 2016

Watoto 3 wa Kike Wakomaa kwenye Nyumba isiuzwe!

. Wamchongea Baba, Baraza la Ardhi-   Ruaha, kwa Lukuvi.


Na Bryceson Mathias


WATOTO watatu (3) wa Kike wa Familia Moja ya Kitongoji cha Nyanvisi, Kata ya Ruaha, wanaodai kutelekezwa na baba yao, Cleopa Daudi Nzali, wamekomaa na kukataa Katakata kuondoka kwenye Nyumba, ambayo Baba yao ameiuza na mnunuzi amefumua Paa na Mabati, huku wao wakiapa kufia humo.

Mbali ya kukomaa ndani ya nyumba hiyo na kulala siku tatu bila Paa Mabati yakiwa yameondolewa, watoto hao wamemchongea Baba yao Nzali, na Baraza la Ardhi la Kata ya Ruaha, kwa kutojali utu wao na kutaka kuwafanyia Figisu ya Nyumba hiyo, wakijua hawana pa kukaa, lakini watoto wao wana pa kukaa.

Watoto hao wamemuomba Waziri wa Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, awasaidie wasihamishwe kwenye Nyumba hiyo pichani,kutokana na kile wanachokiona Baraza la Ardhi la Kata ya Ruaha, linataka wao wapelekwe kwaa Mama yao wa Kambo aliko baba yao, ili mnunuzi achukue Nyumba hiyo, jambo wanalolipinga.

Mabinti hao wenye Msimamo mkali ni pamoja na, Evelina Cleopa (20), aliyehitimu Sekondari ya Iwemba Ruaha mwaka jana, ndiye anayewaongoza wadogo zake, Leonisia Cleopa (17), na Winfrida Cleopa (12), ambao wamedai, Wanawashukuru wasamaria wema kupinga kitendo hicho, na kuwasaidia kurudishia sehemu ya paa na Mabati, baada ya kulala wazi siku tatu.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa niaba ya watoto wenzake hivi karibuni, Evelina ambaye ni mtoto mkubwa alisema, “Mbali ya kututelekeza bila matunzo, tunamshangaa Baba kuuza Nyumba hii (pichani) kimya kimya bila kutushirikisha akishirikiana na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyanvisi, Oswald Mtelela, hali wakijua hatuna Makazi (Baba akiwa na Mama wa Kambo).


“Tuna haki kushirikishwa na Baba au Mama, maamuzi yoyote ya mustakabali wa maisha yetu ili tutoe ushauri! Hivyo Baba kuuza nyumba kinyemala, akishirikiana na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyanvisi ni Ukatili mkubwa dhidi ya Mwanamke tena sisi wenye umri mdogo.


“Hata mnunuzi kununua nyumba yetu akimtumia mwenyekiti wa Kitongoji Mtelela ambaye wameoa Nyumba moja (Dada na Mdogo mtu), asijali uwepo wetu, ni kutudharau kijinsia, tunaitaka Serikali Kuu na tunamlilia Waziri Lukuvi atusaidie ”.alisema Evelina huku akilia machozi akidai wako radhi kufia humo ndani.


Baba wa Watoto hao wa Kike, Cleopa anadaiwa kuuza nyumba hiyo mwaka jana kwa mtu ‘Jina tunalihifadhi’ kwa Mil. 4/- kwa kificho bila kuishirikisha familia, wakiwa na Mwenyekiti wa Nyanvisi, Oswald Mtelela, ambaye mume mwenzie wa Mnunuzi, ambapo alipohojiwa, Mtelela alidai yupo pabaya atapiga simu baadaye, lakini hadi tunakwenda hewani hakufanya hivyo.



Sakata la kuuzwa kwa nyumba hiyo, kulipelekea kwekwa Mahabusu (Polisi), Baba wa watoto hao, Cleopa, Mwenyekiti Mtelela na Mnunuzi, ambapo walipewa dhamana na suala hilo kupelekwe Baraza la usuluhishi la Ardhi Kata ya Ruaha, ambapo Mama mzazi wa watoto hao, Devota Lukasi Bitaki, anapinga akidai hawezi kutendewa haki na Imani na Baraza hilo kutokana na kununuliwa Soda na Mnunuzi wa Nyumba hiyo baada ya Kuahirishwa kwa ikao hicho.


Mwandishi alimtafuta Mwenyekiti wa Baraza hilo kutaka kujua nini kilitokea hadi mama na watoto  hao, kukosa Imani na Baraza, bila mafanikio, ila lilizungumza na aliyekuwa Mwandishi wa wa Baraza hilo, Agness Gowele.


Alipoulizwa kama kuna ukweli kwamba, baada ya Baraza Mwandishi (Gowele) aliomba Soda kwa mnunuzi wa Nyumba hiyo ili wapoze Makoo kwa sababu walikaa muda mrefu kuzungumzia suala hilo, Gowele alikiri kweli yeye alifanya hivyo, jambo ambalo Devota analipinga kuwa ni mgongano wa kimaslahi (Conflict of Interest), hivyo yeye na wanawe hawawezi kutendewa Haki katika usuluhishi wao.


Wakati Mwandishi akifuatilia taarifa hizi za unyanyasaji, alipigiwa simu na Mtu aliyejitambulisha ni Mjumbe wa Baraza hilo akijiita ni ‘Blai’, ambapo alimtukanwa mara kadhaa Mwandishi wa Makala hii, kwa madai haruhusiwi kufuatilia Unyanyasaji huo, hivyo atahakikisha anauliza kwenye vyombo husika ikipidi kumfunga mwandishi.

Mwandishi hakutaka kujibishana naye isipokuwa kumhakikishia kuwa ana ruhusu ya kufuatilia tuhuma hizo isipokuwa kwa kufuata taratibu na sheria zinazotawala! Lakini bado aliendelea kupokea Matusi na kuamua kufunga simu baada ya kung’amua, hofu ilikuwa ni ukiri wa Mwandishi wa Baraza hilo (Gowele), kwamba walinunuliwa Soda na Mnunuzi wa Nyumba.

Mwandishi alipopigiwa tena na aliyejiita Mjumbe wa Baraza kwa kuhoji sakata hilo, akidai Mwandishi haruhusiwi kuhoji kinachofanywa na baraza hata kama ni kibovu, Mwandishi alimtafuta Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Ruaha Longwa, ambapo akikiri kutokea kwa Sakata hilo, akidai ofisi haikubaliani na tukio la kuuzwa kwa Nyumba ya watoto hao na kusema, wananchi wamesaidia kuezeka.


pamoja na Mwandishi kutukanwa, hakuishia hapo alimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adamu Mgoyi, kujifunza iwapo ana taarifa za watoto hao kufanyiwa Ukatili huo wa kuporwa nyumba na kinachotokea kwenye Baraza hilo, ambapo alijibu hana taarifa, isipokuwa aliahidi kufuatilia, na siku ya pili DC alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.

Mapema Novemba 19, Mwaka huu, baraza hilo la Kata liliketi tena kuzungumzia Sakata hilo likisema Watoto hao na Mama Devota wamevamia Nyumba, ambapo Devota alisema, Yeye hamfahamu mnunuzi huyo wa Nyumba aliyejenga na Mumewe, Mnunuzi amfuate aliyemuzia Mbuzi kwenye Gunia.

Baada ya kukalishwa kwa muda mrefu kwenye barza hilo bila maamuzi mnunuzi na Devota wakitolewa Nje, Devota alimpigia Mwenyekiti wa Kijiji Longwa, na Diwani wa Kata ya Ruaha, Isaac maliwa, ambapo maliwa aliwahi kufika na Mama alipolalamika alisema,

“Mama nenda nyumbani ukaendelee na Shughuli zako za kutafuta riziki ili ujikimu na watoto ambao Mume wako amewatelekeza, atakayekuja kukutoa njoo ututaarifu tukamwambie amfuate waliyeuziana naye, na akifika, Serikali itamuhoji dhidi ya tukio hili la Kinyama”.alisema Maliwa.

Aliyekuwa Mwandishi wa Baraza la Ardhi Ruaha (Gowele) alipoingia kwenye Baraza na kumkuta Devota Mama wa Watoto wanaolalamikia kuuzwa kwa Nyumba hiyo, alirudi kwa haraka nje na kuondoka na hakurudi tena, na haikueleweka kwa nini, lakini inadaiwa ni kuhofu kuhojiwa kitendo cha kikao cha awali kuomba Soda kwa Mshitaki (Mnunuzi wa Nyumba).

Kauli ya Mwisho ya watoto wanasema, “Baba yao ana kwao, Mama yao ana kwao, na wao kama watoto kwao ni kwa Baba na Mama yao, Nzali na Devota, hivyo kung’angania Nyumba ambayo wao haiwastahili ila walitakiwa wang’anganie ya Baba na yao ni aibu na fedheha Kijamii, isipokuwa wanapotaka wake nao kwenye Nyumba hiyo, ndiyo wajibu wao badala ya kuiuza.

Karani moja wa Mahakama ya Baraza la Ardhi Dodoma aliyeomba asitajwe jina alipoulizwa iwapo, Waandishi kufuatilia matukio ya Baraza ni Makosa, alipinga Kauli hiyo ya Mjumbe wa Baraza la Ardhi la Kata ya Ruaha na kudai, Waandishi wanaruhusiwa isipokuwa kufuata Sheria na Taratibu ikiwa ni pamoja na kuuliza wahusika kama alivyofanya Mwandishi.

Kutokana na Wananchi kutoelewa Sheria ya Ardhi Namba 4, 5 baadhi ya viongozi wa Vitongoji, Vijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na hata Taifa, wasio na mapenzi mema kwa wananchi, wamekuwa wakiwadhulumu wananchi haki zao, na kuwaacha maskini bila kukemewa, kwa kujifanya kama miungu watu!

No comments:

Post a Comment

Pages