Na Talib Ussi na Mauwa Muhammed Zanzibar
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimesema kitaingia katika kinyanganyiro cha uchaguzi mdogo wa marudio katika nafasi ya Ubunge Zanzibar na Madiwani 22 Tanzania bara bila ya kufuata matakwa ya Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi Tanzania (NEC).
Kauli hiyo alitoa wakati akizungumza na wandishi wa habari huko Afisi ya CUF iliyopo Vuga, mara bada ya kumalizika kikao cha dharura kamati ya utendaji ya chama hicho na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Joram Bashange.
Bashange alieleza kuwa uchaguzi unasimamiwa na sheria na sio matakwa ya mtu binafsi kwa hiyo wao watafuta sheria na kanuni za uchaguzi na sio kauli aliyodai ya kutolewa mfukoni na Ramadhani k. Kailima.
Alisema Chama chake kimeshangazwa na kauli ya ajabu ya mkurugenzi huyo wa tume ya Uchaguzi taifa, kusema kuwa wagombea wa CUF katika uchaguzi huo ni lazma fomu zao za uteuzi zithibitishwe na kutiwa saini na mwenyekiti anaetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa pamoja na katibu mkuu wa chama, jambo alilodai ni kinyume cha sheria na kanuni.
“Eti kinyume na hivyo wagombea wetu hawatatambuliwa na tume ya uchaguzi ya Taifa, tunamwambia sisi tunaingia katika uchaguzi kwa kufuata sheria sio kauli za mfukoni” alieleza Bashange.
Bashange alisema kuwa kauli hiyo ya Kailima inathibitisha kwa mara nyengine kwamba vyombo na tasisi za dola zinatumika kikamilifu kupandikiza ule unaoitwa mgogoro ndani ya CUF kwa lengo la kukihujumu chama hicho.
“masuala ya uteuzi wa wagombea na fomu za uteuzi wa wagombea yanaongozwa na sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi ndugu Kailima amekitoa wapi kifungu cha sheria au kanuni kinachompa uwezo maneno hayo” alieleza Bashange ambaye ni kaimu Naibu Katibu Mkuu CUF bara.
Alifahamisha kuwa tendo hilo, Bashange alidai kuwa ni la ajabu kuweka sharti kwa chama kimoja tuu ambacho halimo katika Vifungu vya sheria.
Alisema moja wapo ya misingi ya sheria ni kutokuwepo kwa ubaguzi katika utungaji na utekelezaji wa sheria na wala huwezi kuwa na sharti linalokihusu chama kimoja tu katika kuthibitisha uteuzi wa wagombea.
“Kwa mujibu wa sheria fomu za uteuzi wa wagombea kutoka tume huthibitishwa kwa kuwekwa saini na Afisa wa chama ambaye ni katibu wa chama wa ngazi inayohusika na kwa ubunge na madiwani imekuwa ni katibu wa wilaya” alieelza Bashange.
Alieleza kwamba sharti alililolitoa Mkurugenzi huyo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi na ni mwenendo wa hujuma za dola na tasisi zake dhidi ya CUF kwa kumtumia mtu anaeitwa Ibrahim Lipumba.
“CUF haitazikubali hujma hizo na italinda na kutetea haki zake za kikatiba na kisheria kwa hali yoyote ile “alisema bashange.
Sambamba na hilo Bashange alieleza kwa sababu CUF ni sehemu ya Ukawa wanafanya mazungumzo vya vinavyounda umoja huo kuona namna gani wataweza kuingia katika uchaguzi na kuwabwaga CCM.
Kikao hicho cha dharura cha siku moja kilikuwa na ajenda ya mandalizi ya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi 22 za madiwani kwa upande wa Tanzania bara na nafasi ya ubunge wa jimbo la Dimani kwa upande wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment