HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 03, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WANAWAKE NA MAENDELEO FOUNDATION


Katika gazeti la Raia Mwema toleo No 486 la Tarehe 30 Novemba, 2016 kumeandikwa habari yenye kichwa kilichosomeka “Mali za Salma Kikwete kuuzwa kwa mnada?”.  Katika habari hiyo kumetolewa madai ati kwamba taasisi ya WAMA inayoongozwa na Mheshimiwa Mama Salma Kikwete inao mzigo mkubwa bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi. Na kwa sababu hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania imepanga kuuza mali hizo.

Kwa niaba ya Taasisi ya WAMA napenda kutoa masikitiko yetu kwamba habari hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote. Kwa maoni yetu gazeti hilo lina dhamira mbaya dhidi ya Taasisi ya WAMA na Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Mama Salma Kikwete. Nia yao ni kupaka matope na kuchafua majina na sifa ya taasisi yetu na kiongozi wake.

Ukweli kuhusu jambo hili ni kwamba, WAMA ilitumiwa maboksi Kumi na Moja (11) ya vitabu vikiwa ni zawadi (grant) kutoka Nakayama Foundation ya Japani ambayo ndiyo iliyofadhili ujenzi wa Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Nyamisati, Kibiti. Maboksi hayo yaliyotumwa kupitia BL 243016002211 yaliwasili bandarini tarehe 27/06/2016. Yalitolewa tarehe 10/8/2016 baada ya WAMA kulipia kodi zote na ushuru wote unaotahili tarehe 26/07/2016.

Vitabu hivyo vimekwishapelekwa shuleni na wanafunzi wanavitumia. Hakuna mzigo wowote wa Taasisi ya WAMA uliopo bandarini unaosubiri kutolewa wala kuuzwa na TRA. Hivyo basi, gazeti hilo kuandika kuwepo kwa mzigo mkubwa wa WAMA bandarini ni jambo la kughushi ambalo limefanywa kwa dhamira mbaya na kwa sababu wanazozijua wao.

Tumelitaka gazeti la Raia Mwema limuombe radhi Mwenyekiti wa WAMA Mheshimiwa Mama Salma Kikwete na kuiomba radhi WAMA Foundation kwa kuandika taarifa za uongo. Gazeti hilo limechafua sifa ya Mwenyekiti wa WAMA na WAMA Foundation kiasi ambacho wanao wajibu wa kuomba radhi na kusafisha majina na heshima zetu mbele ya jamii.

Ikiwa hawatatekeleza haya ndani ya kipindi cha siku Saba, yaani kabla ya tarehe 07 Desemba, 2016, tutalazimika kuchukua hatua zipasazo za kisheria.

Daudi Nasib,
Katibu Mtendaji,
Dar es Salaam,
Tel: +255 22 2781287

info@wamafoundation.or.tz

No comments:

Post a Comment

Pages