WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inahitaji ushirikiano mkubwa na wafanyabiashara, hivyo haitakubaliana na mtumishi yeyote wa umma atakayefanya urasimu kwa lengo la kukwamisha uboreshaji wa sekta binafsi.
Amesema miongoni mwa maboresho yanayofanywa na Serikali katika sekta binafsi ni pamoja na kuimarisha utendaji wa watumishi na kuondoa urasimu katika utendajikazi wa kila siku baada ya eneo hilo limelalamikiwa sana.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Desemba 2, 2016) wakati akizungumza na wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda mkoani Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Ziara hiyo inalenga kuangalia utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,Utendaji wa Serikali, kusikiliza na kujionea kero zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo na kushirikiana na viongozi wa Mkoa ili kuweza kuzipatia suluhisho.
“Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kukuza uchumi wa nchi yetu. Pia mapambano dhidi ya rushwa yanayofanyika ndani ya Serikali na nje yanalenga kuleta maboresho makubwa katika sekta binafsi ,” alisema.
Alisema Serikali inawataka watendaji wake wote watumie lugha nzuri na rafiki katika kutoa huduma kwa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla na haitamvumilia mtumishi yeyote atakayefanya urasimu ili mfanyabiashara atoe rushwa.
“Hatuwezi kuzungumzia maendeleo katika sekta za maji, madini na viwanda bila ya kutaja wafanyabiashara kwa sababu hata viwanda wao ndiyo wamiliki. Wafanyabiashara wameondoa vijana wengi waliokuwa wanakaa vijiweni na kujadili mambo yasiyokuwa na tija na kuwaajiri kwenye viwanda vyao,” alisema.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali itaimarisha mipaka yake na kuzuia uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nje ambazo nyingi zinazalishwa hapa nchini huku lengo likiwa ni kulinda viwanda vya ndani.
“Hatuwezi kuwalinda wazalishaji wetu wa ndani bila ya kuweka doria ya nguvu kwenye mipaka yetu ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa, hususan zinazozalishwa nchini. Lazima Serikali isaidie kulinda masoko ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vyetu,” alisema.
Aliongeza kuwa “Mfano Jiji la Arusha linajenga mradi wa maji na kisha mzabuni anaagiza mabomba kutoka nje wakati viwanda vya ndani vinatengeza kwa viwango sawa au bora zaidi ya yanayoagizwa nje, huko si kutaka kuongeza gharama ya mradi”? Alihoji.
Alisema Serikali haitakubali kuruhusu viwanda vya ndani vife kwa kukosa soko baada ya uingizwaji wa bidhaa za nje. “Ni lazima mitaji ya wafanyabiashara iheshimiwe na ilindwe ili iweze kuleta tija inayokusudiwa,”.
Waziri Mkuu alisema Serikali na sekta binafsi zimefanya jitihada kubwa katika kuhakikisha kunakuwa na uwekezaji kwenye sekta ya viwanda nchini. Na sekta hiyo ndiyo inategemewa katika kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa kati.
Kwa upande wao wafanyabiasha wengi walilalamikia kuwepo kwa wingi wa kodi ambapo wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuzipunguza ili kuwaondolea usumbufu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, DESEMBA 3, 2016.
No comments:
Post a Comment